27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli awabeba wazee, wajawazito

 NORA DAMIAN – SONGWE

RAIS Dk. John Magufuli amepiga marufuku kuwatoza fedha wajawazito wanaochelewa kuanza kliniki, utaratibu ambao umekuwa ukifanywa kupitia kampeni ijulikanayo ‘Mama Komandoo’.

Kampeni hiyo ni mojawapo ya kero zilizolalamikiwa na baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao walidai wamekuwa wakitozwa Sh 50,000 kama adhabu ya kuchelewa kuanza kliniki.

Akizungumza kwa nyakati tofauti jana katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika mji mdogo wa Vwawa na Tunduma, Dk. Magufuli alisema kumtoza mjamzito Sh 50,000 ni kumwonea na akamwagiza kamanda wa polisi kuwakamata watakaobainika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Hii kampeni ya Mama Komandoo ya kutoza Sh 50,000 kwa wanawake wanaochelewa kuanza kliniki naifuta kuanzia leo, pasitokee mtu yeyote anawatoza wajawazito.

“Kumtoza Sh 50,000 ni kumwonea mwanamama ambaye anahangaika na mtoto miezi tisa tumboni… na mimi bado ni rais, kampeni ya Mama Komandoo ni marufuku kuanzia leo, ongezeni idadi ya Watanzania muongeze uchumi wa nchi,” alisema Dk. Magufuli. 

Aliwaasa wajawazito kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na kuhudhuria kliniki kwa wakati ili kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi.

“Lakini nawaomba kina mama nendeni kliniki kwa ajili ya kupunguza vifo vya kinamama na watoto,” alisema Dk. Magufuli.

WAZEE

Dk. Magufuli pia aliahidi kuendelea kuwalinda wazee na kutatua changamoto zao ili kuhakikisha wanafurahia maisha kama makundi mengine ya kijamii.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, idadi ya wazee nchini imeongezeka kutoka 213,000 (mwaka 2015) hadi kufikia milioni 1.042.

“Tumeboresha makazi ya wazee Ngorangoto, Nunge, Magugu Manyara na Fungafunga, pia tumedhibiti mauaji ya wazee, hii ni kuthibitisha kwamba sisi tutaendelea kuwa na wazee, hawajapitwa na wakati,” alisema Dk. Magufuli.

SILINDE

Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa Tunduma kuacha kumpiga vita mgombea ubunge Jimbo la Tunduma, David Silinde, badala yake wamchague aweze kuubadilisha mji huo.

“Ninawaomba wana Tunduma nileteeni Silinde, ninafahamu matunda yake na uzuri wake, hata CCM wapo waliokuwa wanampiga vita, acheni mambo ya ubaguzi, yamepafanya hapa mahali pasiwe salama.

“Acheni mihemko ya kisiasa, hatuwezi kuichafua Tanzania kwa kuanzia Tunduma, siasa si mwisho wa maisha. Vyama vipo lakini visitugawe, hasa vijana tuache jazba, tuwe wavumilivu.

“Hizi chaguzi ni za miezi miwili tu zinaisha, tusipelekwe na mihemko ya siasa, tunahitaji maendeleo na maendeleo hayana chama,” alisema Dk. Magufuli.

MAPINDUZI YA KILIMO

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mji mdogo wa Vwawa, Dk. Magufuli aliahidi kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuhakikisha pembejeo na zana zote za kilimo zinapatikana kirahisi na kwa gharama nafuu.

Alisema pia wameanzisha kiwanda cha kuunganisha matrekta kilichopo Kibaha na kwamba wakulima watawezeshwa kwa kununua kwa fedha taslimu, mikopo bila riba au kwa masharti nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Dk. Magufuli alisema kutokana na changamoto iliyojitokeza katika zao la pamba, kiwanda cha nguo cha Mbeya kimebadilishwa na kwa sasa kitazalisha wanga, mafuta na chakula cha wanyama ambapo kwa siku kitahitaji tani 45 za mahindi. “Songwe ni mkoa wa mwisho kuanzishwa, niseme kwa dhati naupenda sana, ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji chakula nchini, unashika nafasi ya tatu kwa Tanzania nzima.

“Ndiyo maana nilimteua Hasunga (mgombea ubunge Vwawa, Japhet Hasunga) kuwa waziri wa kilimo, nilifanya hivyo kwa makusudi kwa kutambua ninyi wana Songwe ni wakulima wazuri… nataka niwaahidi mkoa wangu wa mwisho kuzaliwa sitawaangusha, nitawatumikia vizuri kwa nguvu zote,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema pia wataendelea kushughulikia tozo mbalimbali zinaloleta kero kwa wakulima na wafanyabiashara ili kuwawezesha wafanye shughuli zao kwa uhuru.

MIRADI YA MAENDELEO

Dk. Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa mkoani Songwe, ikiwemo ujenzi wa soko la mazao la kimataifa la Kakozi kwa gharama ya Sh bilioni 8.65.

Miradi mingine ni ujenzi wa vihenge sita kwa thamani ya Sh bilioni 11.4 vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na kuongeza uwezo kutoka tani 17,000 hadi 37,000.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, vihenge hivyo pia vinajengwa katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Rukwa, Katavi, Shinyanga, Manyara na Dodoma na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao hadi kufikia tani 190,000.

Alisema pia yanajengwa maghala yatakayokuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 na kwamba uwezo wa kuhifadhi mazao utaongezeka kutoka tani 251,000 hadi 501,000.

Dk. Magufuli alisema kutokana na kuanzishwa kwa Kituo cha Kanda cha NFRA cha Songwe – Mbeya bei ya mahindi kwa kilo ni Sh 550 ambayo ni juu ya bei ya soko na kwamba kwa mwaka 2020/21 wakala huo unatarajia kununua tani 30,000 katika mkoa huo kwa gharama ya Sh bilioni 16.5.

Alisema kutokana na kuanzishwa kwa mnada wa kahawa mkoani humo, kwa msimu huu tayari zimeuzwa kilo 50 kwa Dola kati ya 76 hadi 153 kwa kilo moja ambayo ni juu ya bei ya soko la dunia yaani Dola 116.

Dk. Magufuli alisema pia zimejengwa skimu tatu za umwagiliaji kwa Sh milioni 730 na kwamba nyingine zimepangwa kujengwa Iyula, Ipanga na Jikomboe kwa Sh milioni 190.

“Tunataka wakulima wafanye biashara zao wasisumbuliwe na mtu yeyote,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema pia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imetoa mikopo ya Sh bilioni 2.66 kwa vyama vinane vya msingi vyenye wakulima 744 wa mahindi na kahawa.

Kwa upande wa miundombinu, alisema wamejenga barabara ya Mpemba – Isongole kilomita 50.5 kwa gharama ya Sh bilioni 107.55, Daraja la Kamsamba kwa Sh bilioni 17.72 pamoja na madaraja mengine Igagula, Ndambo na Lugwiza.

Kuhusu maji, alisema unatekelezwa mradi wenye thamani ya Sh bilioni 10.4 yakiwemo maeneo ya Iyula – Itaka katika Wilaya ya Mbozi na Mkwajuni, Kapalala, Kaloleni katika Wilaya ya Songwe.

Kwenye umeme alisema vijiji 182 vina umeme na kuahidi kumalizia 125 vilivyobaki ndani ya muda mfupi.

 Kwa upande wa sekta ya afya, alisema wanajenga hospitali ya rufaa ya mkoa kwa gharama ya Sh bilioni 4.7, hospitali za wilaya za Songwe na Tunduma kwa Sh bilioni 4.89, ukarabati wa hospitali ya Wilaya ya Ileje (Sh bilioni 1.8), ujenzi wa vituo vinne, kukarabati vituo sita na ujenzi wa zahanati mbili (Sh bilioni 4.55).

“Tunataka hii hospitali huduma zote ziwe zinamalizikia hapa, tutaleta manesi, madaktari na ‘ma-specialist’ wa kutosha katika magonjwa mbalimbali,” alisema Dk. Magufuli.

Pia aliahidi kukamilisha ahadi aliyoitoa ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi na soko la kisasa na kwamba upembuzi yakinifu umeshaanza kwa ushirikiano wa Wakala wa Majengo (TBA) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles