23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NAFASI ZA VIGOGO 12 WALIOONDOLEWA NSSF ZATANGAZWA

Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetangaza nafasi za kazi zilizoachwa wazi na vigogo 12 waliotumbuliwa kwa tuhuma mbalimbali.

Kati ya vigogo hao 12, vigogo sita walikuwa wanatumikia nyadhifa za juu kabisa za utendaji ndani ya shirika hilo.

Vigogo hao ni Yacoub Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha), Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala).

Wengine ni Sadi Shamliwa (Mkurugenzi wa Udhibiti Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).

Tangazo la nafasi za kazi lililotolewa jana na shirika hilo na kuchapishwa na gazeti moja la kila siku(si MTANZANIA) limeorodhesha nafasi 13 ambazo zinatakiwa kujazwa.

Katika nafasi hizo 13, nafasi saba ni wakurugenzi ambazo ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala.

Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Udhibiti Majanga, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Mkurugenzi wa Tehama.

Pia zipo nafasi nne ambazo ni Ofisa Masoko na Uhusiano, Meneja Usalama, Meneja wa Mipango na Uwekezaji na Meneja Miradi. Nafasi nyingine ni Makatibu Muhtasi 12 na Madereva 15.

Tangazo hilo limekuja ikiwa ni takribani  miezi 11 kupita tangu Bodi ya Udhamini ya shirika hilo kuwasimamisha kazi vigogo hao kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma, matumizi mabaya ya ofisi, kukiuka sheria na kanuni za usimamizi wa miradi na manunuzi.

Katika azimio la Bodi ya Udhamini ya shirika hilo la kuwasimamisha kazi watumishi hao, ukiachia mbali Wakurugenzi sita, pia mameneja watano na mhasibu mmoja walisimamishwa ili kupisha uchunguzi.

Mameneja waliosimamishwa kazi  ni Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja Uwekezaji), Mhandisi John Msemo (Meneja wa Miradi), Chedrick Komba (Meneja Kiongozi –Mkoa wa ki-NSSF wa Temeke), Mhandisi John Ndazi (Meneja Miradi) pamoja na Mhasibu Mkuu wa Shirika hilo, Davis Kalanje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles