NA KAMUGISHA RWECHUNGURA
DUNIA ya sasa inaongozwa kwa kiasi kikubwa na biashara za kimataifa. Ni jambo la kawaida katika dunia ya leo kuona bidhaa inayozalishwa katika nchi moja inauzwa katika nchi nyingine.
Baadhi ya bidhaa kwa mfano mafuta na gesi ambazo zinazalishwa katika nchi chache duniani, lakini hupatikana kila pembe ya dunia. Pia vifaa tunavyovitumia katika maisha yetu ya kila siku kama vile magari, simu, kompyuta na kadhalika vinatoka katika pembe zote za dunia na hutufikia kwa sababu ya biashara ya kimataifa.
Biashara hii ni muhimu duniani kwa sababu hakuna nchi duniani inayoweza kujitosheleza kwa kila bidhaa na huduma. Kununua au kuuza bidhaa yoyote ni kushiriki katika uchumi wa dunia.
Takwimu kutoka shirika la biashara la kimataifa (World Trade Organization) zinaonyesha kuwa moja ya tano ya biashara katika soko la dunia (World Global Trade) uhusisha huduma mbalimbali kama za kibenki, bima, usafirishaji, mawasiliano, utalii na nyinginezo nyingi.
Kwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine nyingi duniani; serikali na watu wake (binafsi, makampuni na taasisi) hujihusisha katika biashara ya kimataifa kwa kununua na kuingiza nchini ama kwa kuuza nje bidhaa zetu.
Hii inapelekea watumiaji wa biashara hizo kutuma fedha za kigeni nje ya nchi pindi wanaponunua bidhaa zao au kupokea fedha za kigeni pale wanapouza bidhaa zao nje ya nchi. Ni muhimu sana kwa watumiaji wa biashara za kimataifa na wanaotarajia kutumia kuwa na uelewa wa kutumia mifumo ya kibenki katika kufanya malipo pindi wanaponunua au kupokea malipo pindi wanapouza bidhaa zao nje ya nchi.
Benki zina nafasi kubwa na ya muhimu katika biashara ya kimataifa. Ukiachilia mbali kuwa benki zinatoa mikopo ya muda mfupi (ya kabla na baada ya kusafirisha bidhaa) kwa wauzaji wanje pia zinawasaidia wauzaji na wanunuzi katika kutambua fursa za masoko katika nchi za kigeni.
Benki hutoa pia dhamana (guarantee) kwa wauzaji kuwa malipo yatafanyika endapo makubaliano ya mkataba wa mauziano yatatekelezwa. Baadhi ya benki hapa nchini zimeingia kwenye makubaliano na benki nyingi duniani kuwa benki rafiki (corresponding bank) kwa ajili ya kuwahudumia wateja wake wanaojihusisha na biashara ya kimataifa. Hizi benki rafiki husaidia kufanya na kupokea malipo nje ya mipaka ya nchi kwa niaba ya benki iliyoko nchini.
Kwa hiyo, kwa msaada wa benki, mnunuzi anakuwa amehakikishiwa kupata malipo ya bidhaa alizoziuza na vile vile mnunuaji anakuwa amehakikishiwa kupokea bidhaa alizozilipia.
Biashara ya kimataifa ina tofauti sana na biashara ya ndani. Inaweza kumhusisha mfanyabishara kutoka Tanzania na mwingine kutoka katika nchi za Mashariki ya Mbali. Kuna uwezekano pia wa kukuta mnunuzi na muuzaji hawajuani tabia kwa undani au hawajawahi kuonana kabisa.
Kwa mfano, watu wengi hapa nchini wananunua magari kutoka katika kampuni za kuuza magari kutoka Japan. Wengi wa wanunuzi hawa wanakuwa hawafahamiani na mtu yoyote kutoka katika kampuni hizi zinazouza magari.
Katika hali hii, mnunuzi anataka uhakika kuwa atapokea bidhaa aliyoiagiza na kuilipia na pia muuzaji anataka uhakika kuwa atapokea malipo ya bidhaa aliyoiuza na kuisafirisha.
Muuzaji anatamani apokee malipo kabla ya kupakia na kusafirisha bidhaa na wakati huo huo mnunuzi anatamani apokee na kuikagua bidhaa aliyoiagiza na kujiridhisha kuwa makubaliano yote ya mkataba wa mauziano yametimizwa kabla ya kufanya malipo.
Katika mkanganyiko huu, ndipo nafasi ya benki katika kusaidia kwa kuwezesha biashara ya kimataifa huonekana bayana. Benki huingia kama kiunganishi baina ya muuzaji na mnunuzi na huhakikisha usalama na usafirishaji wa nyaraka zihusuzo bidhaa na fedha.
Njia ambayo inatumika sana katika biashara ya kimataifa kuhakikisha mnunuzi anapokea nyaraka za bidhaa alizozinunua na muuzaji anapokea malipo yake baada ya kutimiza makubaliano yote ya mkataba wa mauziano ni barua ya dhamana, yaani “letter of credit”.
Mnunuzi huiomba benki yake itoe dhamana kwa mfumo wa letter of credit ikimhakikishia muuzaji kuwa endapo atatimiza makubaliano yote ya mkataba wa mauziano, basi benki itafanya malipo. Kwa kitendo hiki, muuzaji anakuwa amehakikishiwa malipo endapo atatekeleza makubaliano yote ya mkataba.
Baada ya benki ya mnunuzi kuandika barua hii, hutumwa kwenye mfumo wa kibenki kwenda kwa benki mshauri (advising bank) ambayo inakuwa ni benki rafiki (corresponding bank). Benki mshauri mara nyingi huwa ipo katika nchi ambayo muuzaji wa bidhaa anapatikana.
Benki mshauri hujiridhisha na uhalali wa barua ya dhamana na kumjulisha mnufaika ambaye ni muuzaji juu ya uwepo wa barua hiyo. Benki mshauri inaweza pia kuongeza dhamana (guarantee) juu ya ile iliyotolewa mwanzo na benki ya mnunuzi kuwa itafanya malipo endapo muuzaji atatimiza makubaliano yote ya mkataba.
Hii humsaidia muuzaji kuwa na uhakika wa malipo kutoka katika benki ya nchini kwake endapo atatimiza makubaliano yote ya mkataba. Benki za biashara husaidia na hufanya malipo kupitia nyaraka na si bidhaa zenyewe.
Kwa hiyo, baada ya bidhaa kukaguliwa na mamlaka husika na nyaraka kuwasilishwa, ile benki iliyotoa barua ya dhamana humlipa muuzaji wa bidhaa kupitia benki rafiki (corresponding bank) iliyoko katika nchi ya muuzaji.
Huduma nyingine zitolewazo na benki kwa lengo la kusaidia biashara ya kimataifa ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa wauzaji kabla na baada ya kusafirisha bidhaa (pre and post shipment financing).
Mikopo hii mara nyingi hutolewa kwa watu, makampuni na taasisi zilizoidhinishwa na mamlaka husika kuwa zinajihusisha na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi. Mikopo ya muda mfupi itolewayo kwa wauzaji kabla ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi (pre-shipment financing) hulenga kuwasaidia wauzaji hao katika kuzalisha na kuandaa bidhaa hizo.
Mara nyingi mkopo huo huwa ni sawa na thamani ya ankara (invoice) ya pesa inayotarajiwa kupatikana katika mauzo ya bidhaa hizo. Na mara nyingi, malipo ya mkopo huu hutokana na fedha inayopatikana baada ya mnunuzi kufanya malipo.
Kwa maana nyingine ni kuwa, mkopo huu hulipwa kutokana na mapato ya bidhaa zilizouzwa. Pre-shipment financing humsaidia muuzaji kuweza kumudu gharama za uzalishaji na uandaaji wa bidhaa kwa kipindi chote ambacho anakuwa anangojea malipo yake.
Kwa upande mwingine, mkopo wa muda mfupi utolewao na benki kwa wauzaji baada ya kusafirisha bidhaa huitwa post-shipment financing. Mkopo huu hulipwa pia kutokana na malipo anayoyapokea muuzaji baada ya mnunuzi kufanya malipo. Mikopo yote hii kwa pamoja humsaidia muuzaji wa bidhaa kuendesha biashara zake kwa ufanisi zaidi bila kukabiliwa na ukata wa fedha.
Siyo siri tena kuwa ili wafanyabiashara wa hapa nchini waweze kufanikiwa katika biashara ya kimataifa ni lazima wawe na uelewa wa mchango wa benki katika biashara zao. Wafanyabishara watakao elewa na kutumia fursa zipatikanazo kwa kutumia benki, watazidi kujiimarisha katika kukuza biashara zao.
Ni vema wafanyabishara wanaojihusisha na biashara ya kimataifa au wanaotegemea kujihusisha na biashara hizo, watembelee benki zao ili wapewe maelekezo ya huduma wanazoweza kupatiwa na benki zao katika kukuza biashara zao kimataifa.