Beatrice Kaiza
Waumini wa dini zote watakiwa kuliombea Taifa la Tanzania ili kuepuka majanga.
Wito huo umetolewa na mtumishi wa Mungu, Nabii Joshua ambapo amesema wakati mwengine taifa linapofikwa na majanga yanayohatarisha maisha ni muhimu waumini wote kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuliombea taifa kuepuka majanga na maafa.
“Tumeungana kwa pamoja kuwaombea watu wa Moshi kwa kupoteza ndungu zao huu ni msiba wa taifa lakini kwa uwezo wa Mungu ametupa wasaa wa kumshukuru kwa kila jambo na kumuomba amani,” amesema Nabii Joshua.
Amesema Watanzania wanatakiwa kuitumia amani kama tunu ili kujipatia maendeleo.
“Amani haiwezi kudumu pasipo kumuomba Mungu aendelee kutujaalia amani hiyo, waumini wote tuungane tuombe Mungu ili pasitokee mtu, kikundi kitakachoweza kuvuruga amani hii tuliyoachiwa na mababu zetu,” amesema Nabii Joshua.
Hata hivyo amempongeza Rais John Magufuli kwa kuendelea kutetea wanyonge na kuimarisha uchapakazi hasa kwa vijana.
“Rais Magufuli ni Kiongozi wa kipekee anaependa usawa kwa watu wote ndio maana anaitwa rais wa wanyonge hivyo tumuunge mkono na tumuombee pia kwa maana kazi anayofanya sio ndogo hasa linapokuja suala la kuliongoza Taifa,” amesema Nabii Joshua.