25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Maafa kwa Mwamposa

 WAANDISHI WETU– KILIMANJARO/DOM

MTUME na Nabii Boniface Mwamposa (Buldoza), amekamatwa na Jeshi la Polisi akiwa jijini Dare s Salaam, kwa madai ya kusababisha vifo vya watu 20 na wengine 16 kujeruhiwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kutokana na utelezi wa ‘mafuta ya upako’ aliyowaelekeza kuyakanyaga kwenye ibada ya maombezi.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana na ilielezwa kuwa baada ya maafa hayo, mtume na nabii huyo aliondoka na kurejea Dar es Salaam, ambapo jana aliendelea na ibada katika Viwanja vya Tanganyika Packers, ambapo ndipo anapoendeshea ibada zake kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alithibitisha kwamba wamemkamata Nabii Mwamposa jijini Dar es Salaam, alipokuwa amekimbilia mara baada ya kutoroka mkoani Kilimanjaro kutokana na tukio la waumini wake kugombea kukanyaga mafuta ya upako na kusababisha vifo hivyo vya watu 20.

Alisema wanaendelea na upelelezi utakapokamilika wanatarajia kumpandisha kizimbani.

“Katika maeneo yale hakupatikana kirahisi, tulikuwa tuna taarifa kwamba atasafiri kwa ndege, sasa tulifuatilia tukaambiwa aliondoka na usafiri wa gari kwa muda mchache alioondoka tumefanikiwa kumkamata alfajiri jijini Dar es Salaam.

“Kwa hiyo Mchungaji au Mtume Boniface Mwamposa baada ya tukio hili alitaka kukimbia lakini hivi ninavyozungumza yuko katika mikono ya Jeshi la Polisi na tunafikiria kumtoa Dar es Salaam kumrudisha Kilimanjaro ili aende akawajibike na kosa au madhara haya ya maafa ambayo kwa kweli kwa uwazi yeye na wenzake wamesababisha.

“Kwa hiyo niseme wengine wote wanaofanya shughuli kama hizo au kusababisha mkusanyiko wahakikishe kwamba hawasemi maneno au kusababisha maneno yatakayosababisha msisimuko kwa waumini au kwa wafuasi wao na hata kupoteza maisha kwa hiyo tuchukue tahadhari na hata watu wanatoka salama katika mikusanyiko,” alisema Waziri Simbachawene.

Alisema Mwamposa alikuwa na kibali cha mkutano huo ambacho kilimtaka amalize saa 12 jioni lakini alipitisha muda kinyume cha sheria inavyotaka.

“Mchungaji au Mtume Boniface Mwamposa au kwa jina maarufu ‘Buldozer’ alikuwa akiendesha mkutano wa injili ambao ulikuwa na kibali cha kufanyika kati ya tarehe 30 Januari hadi tarehe 1 Februari 2020, lakini ilipofika majira ya saa kati ya saa 1:30 hadi 2:00 usiku jana (juzi) usiku aliwaelekeza waumini wake ambao walikuwa wamekusanyika mahala hapo. 

“Ambao ni wengi kwamba wapite katika sehemu ambapo kulikuwa na turubai lililomwagwa mafuta ili waweze kupata nafuu ya matatizo au shida zao kwa kadiri walivyoaminishwa na kusababishwa mkanyagano uliopelekea vifo vya hawa watu 20 na wengine 16 kujeruhiwa,” alisema Simbachawene

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya, sura Namba 337 na hasa kifungu cha 9 na cha 19, Waziri wa Mambo ya Ndani, ndiye anayesajili jumuiya hizi za kijamii lakini pia madhehebu ya dini na shughui zote za taasisi za watu binafsi.

“Hivyo jukumu la kuhakikisha kwamba amani inakuwepo katika taasisi hizo za kidini na hivyo ndiyo maana nimesema niseme na niwape pole sana familia hizi za watu 20 waliofariki na wale waliojeruhiwa.

“Lakini ni lazima kama Serikali tuchukue hatua stahiki kwa sababu inasikitisha watu kwamba una idadi kubwa ya watu umewakusanya mahali, mwenye jukumu la kuhakikisha usalama wao ni wewe uliyewakusanya hapo pamoja na jukumu la Serikali la kuhakikisha kwamba watu wanakuwa salama lakini kwa idadi kubwa ya watu watu wa namna hiyo.

“Unapotoa maelekezo au maneno ambayo yanaweza kusababisha mhemuko na watu wakaweza kukimbizana na kufikia hatua ya kuumia basi unawajibu wa kuwajibishwa katika kosa hilo.

 “Kwa hiyo nitoe rai kwa viongozi, kwamba dhehebu na shughuli za kidini na mikusanyiko mbalimbali kujua kwamba wana wajibu wa kuhakikisha usalama wa watu kwa sababu kwanza kibali kilikuwa kinatoka saa 6:00 hadi saa 12:00 lakini tukio limetokea kati ya saa 1:30 hadi saa 2:00.

“Inaonyesha namna ambayo masharti ya kibali yalikuwa yamekiukwa lakini kuwaelekeza watu zaidi ya 10,000 waliojazana mahali kwamba wapite sehemu moja pia inaonyesha kutokuwajibika katika kuwa na dhamira ya kwamba unajua jukumu la kuhakikisha hawa watu wanakuwa wako salama,” alisema.

JPM ATUMA SALAMU

Rais Dk. John Magufuli jana aliungana an wafiwa kwa kutuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wakitoka katika Ibada hiyo.

Rais magufuli pia alituma salamu hizo kwa familia za watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha kutokana na madhara ya mvua kubwa zinazonyesha mkoani Lindi na mikoa mingine hapa nchini.

Katika salamu hizo zilizotolewa kupitia taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa ilieleza kuwa watu hao 20 waliofariki dunia mjini Moshi na wengine 16 kujeruhiwa, na wenguin zaidi ya 20 wal;iofariki dunia mkoani Lindi na katika mikoa mingine hapa nchini ambayo imekumbwa na madhara yatokanayo na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.

“Rais ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo, na amewaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao,” alisema.

Pia, Rais Magufuli alitoa wito kwa Watanzania wote kuchukua tahadhari katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha vinasimamia ipasavyo tahadhari za kiusalama.

MASHUHUDA WAZUNGUMZA

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya waumini walionusurika na tukio hilo, walisema ibada hiyo ilihitimishwa na mtume huyo majira ya saa 12 jioni ambalo waliambiwa wakanyage mafuta hayo kwaajili ya kupata upako na baraka katika Maisha Yao.

“Ibada ilikuwa nzuri na yenye baraka sana kwetu ila baadae iligeuka kilio kitokana na watu kuangukiana na kukanyagana wakati tulipoenda kukanyaga mafuta ya upako,” alisema Ester Mrema mkazi wa majengo.

“Mbaya zaidi watu walikufa wengi kutokana na ule utelezi…watu wakati wanakanyaga walikuwa wakiteleza na kuanguka kambo ambalo sisi tuliona ni upako na sio utelezi hivyo wengi wakapata shauku ya kuyakanyaga na ndiyo walipoangukiana wakati huo mimi nilikuwa nimeshatoka,” alisema Mrema.

Naye Angle Peter, alisema wakati tukio hilo likoendelea alishuhudia maiti mbili za watoto wa dogo zikitolewa na kwamba wengi wao hawakujua kama wamefariki bali walijua kuwa walipagawa na mapepo jambo ambalo shughuli hiyo iliendelea mpaka polisi walivyofika.

GARI ZA POLISI, WAGONJWA ZASAIDIA

Juzi, MTANZANIA ilifika eneo la tukio majira ya saa mbili usiku ambapo ilishuhudia magari ya polisi pamoja na yale ya kubebea wagonjwa ikizitoa baadhi ya maiti zilizokiwa zielala katika lango kuu la kuingilia uwanjani hapo.

Magari hayo yalionekana kurudi zaidi ya mara sita katika eneo hilo ambapo walichukua majeruhi na maiti.

Hata hivyo maelfu ya wafuasi wa Mwamposa walitoka katika viwanja vya Majengo mjini Moshi kuanzia majira ya saa moja na kumalizika saa nne usiku huku kukiwa na wingi wa magari, bajaji pamoja na pikipiki.

Mbali na eneo hilo kuonekana kuwa na malango ya kutokea manne wafuasi wengi walielekea katika lango hilo kuu peke la kutokea kutokana na kukimbilia usafiri haswa ikizingatiwa ilikuwa ni usiku.

Wanawake na watoto wadogo walionekana kuwa ni wengi zaidi huku kukiwa hakuna utaratibu mzuri wa kukanyaga mafuta hayo.

MAITI 20 KUAGWA ENEO LA TUKIO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alikiri watu hao kufariki ambapo alisema wote wataagiwa katika viwanja hivyo.

“Ni kweli watu 20 wamefariki na wengine 16 wamejeruhi ambapo kati ya miili 20 miili miwili imetambuliwa na kwa Sasa serikali inaandaa utaratibu wa kuwasialiana na viongozi wa dini ili tuwaage ndugu zetu katika viwanja hivyo kwa siku ya kesho (leo),” alisema.

Aidha, alisema hadi jana mchana miili iliyotambuliwa ni ya watu 14 huku miili mingine ndugu zao wakiwa bado hawajajitokeza na kwamba majeruhi wanaendelea vizuri.

Aidha alisema uchunguzi wa awali uoonyesha lango kuu moja ndiyo lililofunguliwa licha ya kuwepo kwa malango manne katika uwanja huo na kwamba Mtume huyo baada ya kuona hali hiyo alikimbia.

AKEMEA MAFUNDISHO

Alisema jambo hilo ni la kusikitisha ila aliwataka Watanzania na wananchi kuwa makini na mafundisho ya aina hiyo yanayolenga utajiri na uponyaji.

“Nasikitika kwa jambo hili kutokea katika mkoa wetu na aina hii ya mafundisho ambayo yanakanganya watu kwa kutoa ahadi za utajiri, kuponywa magonjwa na mafanikio…zimeanza kuwa na adhari mbaya kwetu,” alisema.

KAMANDA WA POLISI ANENA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni, alisema hadi jana mchana watu waname walishakamatwa na wanashikiliwa kutokana na tukio hilo.

“Uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na tumewakama watu wanane ikiwemo mchungaji kiongozi wa huduma hiyo ya Inuka na Uangaze Elia Mwambapa,” alisema

KAULI ZA WAUMINI

Baadhi ya waumini waliokuwa katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dare s salaam jana, walizungumza na MTANZANIA na Anitha Meero alisema Mwamposa aliongoza ibada jana asubuhi, muda mfupi baada ya tukio la Moshi na katika ibada ya kwanza walisali ibada maalumu inaitwa keki ya upako.

“Ibada ya kwanza leo (jana) iliendeshwa haraka haraka na kuisha mapema na baadaye ibada ya pili lakini ghafla tukaona Mtume anakatiza ibada na anashuka kutoka kule juu, hatukujua anapokwenda, binafsi sikuona mwisho wa pale, alisema Meero.

Scolastika Athanas, alisema hata wale wa ibada ya kuhiji nao kuna baadhi wanakufa kwa sababu ya kuabudu kwa hiyo lililofanyika aun lililotokea huko Moshi nalo ni sehemu ya ibada, ingawa halikupangwa.

KANUNI MPYA

Hata hivyo, akielezea hatua wanazochukua, Waziri Simbachawene alisema kutokana wingi wa makanisa wanafikiria kuja na kanuni ama mwongozo kwa ajili ya kuyasimamia makanisa.

“Yapo mambo mengi yanafanyika katika suala la imani sisi tunaheshimu uhuru wa kuabudu lakini lazima uangaliwe makosa kama haya yanaanza kutupa fundisho hata sheria na kanuni zetu zinatakiwa kuwekwa sawa.

“Kwa sababu huyu anakuja na sabuni ya kuogea anasema inaponyesha huyu anakuja na maji huyu mafuta mwingine maziwa lakini ni vizuri wawepo watu wanasimamia,” alisema

LEMA ATOA NENO

Kwa upande wake, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema alisema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Simbachawene na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, RPC Kimanjaro na OCD Moshi wanatakiwa kujiuzulu kutokana na vifo 

 vya watu 20 waliokuwa wakigombea mafuta.

“Simbachawene (Waziri wa Mambo ya Ndani) wakati anaapishwa alipewa wajibu mmoja ukiisikiliza kauli ya Rais aende akalete mahusiano mazuri na viongozi wa Jeshi la Polisi na mimi naamini Kangi (Lugola) ametolewa sababu ya kutokuwa na mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi, sasa Simbachawene alimeambiwa aende akarekebishe kwa sababu kuna uchaguzi Mkuu mwaka huu hivyo wanatakiwa kushinda.

“Polisi Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, RPC, OCD, IGP na Simbachawene kama wanajali mauti yaliyotokea na watu ambao wamekufa pale mshitakiwa namba moja sio Kanisa ni Polisi walitakiwa kuhakikisha usalama,” alisema.

Pia Waziri Kivuli huyo alitoa pole kwa waliofariki na majeruhi pamoja na kwa 

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles