22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Nabii Mwingira amtabiria Nyalandu ukuu

Lazaro-Nyalandu1Na Ratifa Baranyikwa, Dar es Salaam
SIKU chache baada ya kutangaza kujitosa rasmi kuwania ukuu wa dola, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameadhimisha sherehe za mwaka mpya wa 2015 katika Kanisa la Efatha huku Mchungaji wa Kanisa hilo, Josephat Mwingira, akimtabiria ushindi wa safari aliyoianza.
Zaidi Mwingira alisema neno hilo ni la kinabii na kusisitiza hakuna wa kumzuia Nyalandu kwa sababu ukuu umeamriwa juu yake.
Katika ibada hiyo ya mkesha wa mwaka mpya ambayo Nyalandu alikuwa mgeni rasmi, Mchungaji Mwingira mbali na kumtabiria hayo, pia alisema sasa utawala wa majini umefika mwisho.
Bila kufafanua juu ya utawala huo wa majini, Mwingira alisisitiza kuwa utawala wa kipepo hautakaa utawale tena hapa nchini.
“Umefika wakati wana wa Mungu kuwa na haki yao, umefika wakati wana wa Mungu kupumua… ninazo salamu kutoka kwa bosi, salamu za kinabii siku ya kwanza ya 2015 mwaka ambao una kindumbwendumbwe cha uchaguzi,” alisema.
Mwingira ambaye alisema neno hilo limetoka kwa Bwana, alisisitiza kuwa vikwazo juu ya Nyalandu havitakuwapo tena.
“Hakuna atakayekuzuia tena badala yako ni wakati wa wana wa Mungu kuinuka, hakuna atakayekukandamiza tena, mimi Baba yako nitatangulia mbele yako niseme kitu, neno hili la kinabii litasababisha yale yaliyokuwa mbali yawe karibu na yaliyokuwa hayawezekani yawezekane,” alisema Mwingira.
Katika hilo, Mwingira pia alisema anataka kuliweka jambo hilo katika agano na Nyalandu kwa maana ya kukubaliana baadhi ya mambo ambayo atakwenda kuyatekeleza wakati atakapokuwa Rais, mojawapo ni kuirudisha Tanganyika huru.
Awali kabla Mwingira hajasema hayo, alimuita Nyalandu mbele ya madhabahu ya kanisa hilo kwa ajili ya kutoa salamu za mwaka mpya, ambapo alitumia fursa hiyo kulieleza kanisa juu ya azma yake ya kuwania ukuu wa dola mwaka huu.
Zaidi aliliomba kanisa hilo kumuunga mkono huku akisisitiza kuwa mwezi wa 11 ambao kimsingi ataapishwa Rais mpya, patatokea jambo ambalo atahitaji kwaya ya kanisa hilo kwa ajili ya kutumbuiza kwa ajili yake.
“Mwezi wa 11 patatokea jambo nitahitaji kwaya hii (Kwaya ya Kanisa ambayo ilikuwa ikitumbuiza kabla hajaanza kutoa salamu hizo).
Katika ibada hiyo ya mwaka mpya iliyokuwa na ujumbe; ‘Mwaka wa kibali kwa aliowaridhia’, Nyalandu aliahidi kuitoa Tanzania kwenye hofu na umaskini.
“Mtakapoona maono msisite kunionya…safari hii ambayo ninaianza ya maono itakwenda kuibadilisha Tanzania, kama ilikuwa inaenda kwa hofu, hofu itaondoka, kama ilikuwa na umaskini, utaondoka, ninaomba Mungu akaiguse nchi kupitia mlango wa Efatha” alisema.
Nyalandu pia alitumia fursa hiyo kuanza kuomba kura kutoka kwa waumini hao akitumia mfano wa mmoja wa wanasiasa kutoka Kenya, Joseph Kamotho, ambaye aliupata ubunge na hatimaye uwaziri kwa hisani ya Rais Daniel arap Moi.
Alisema Kamotho ambaye kwa nyakati tofauti wakati wa utawala wa Rais Moi alipata kuwa Waziri wa Elimu, kisha Biashara na hata Mazingira na Utalii, alikuwa ni mtu wa karibu na kiongozi huyo baada ya kumdokeza juu ya kuwako kwa njama za kutaka kuuondoa uhai wake.
“Kamotho alimweleza Moi juu ya habari hizo, baada ya hapo walikuwa ni watu wa karibu sana na wakati wa uchaguzi ulipofika alimwambia agombee ubunge, lakini alishindwa baada ya watu wa eneo alilokuwa akigombea kumkataa, lakini Moi alimteua kuwa mbunge na kisha Waziri wa Elimu,” alisema.
Alisema wakati fulani ikaandaliwa hafla katika jimbo ambalo Kamotho aligombea ubunge na mgeni rasmi alikuwa Rais Moi, na kwamba alipotakiwa mtu wa kutoa hotuba, alisimama na kusema kuwa yeye alinyimwa kura zote, lakini alipitishwa kwa kura moja tu ya Moi.
“Na mimi ninaomba kura moja ya Efatha…kura ya Yesu wa Nazarethi itakuwa kura ya mlango wa nchi hii, kupitia kura moja ambayo huwezi kuamua kwa pesa za lumbesa, kura moja sio ya wale wanaotoa rushwa,” alisema Nyalandu.
Nyalandu ambaye katika ibada hiyo alionekana akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Jinsia, Watoto na Wanawake, Pindi Chana, alisema kama vile anavyowafikiria watoto na mke wake, ndivyo anavyoifikiria nchi hii.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Nyalandu ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, alitangaza kuwania urais kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ilongero, ndani ya jimbo lake la uchaguzi.
Akihitimisha fununu zilizokuwa zikimtaja miongoni mwa wanaCCM wanaotaka kukalia kiti hicho kitakachoachwa na Rais Jakaya Kikwete, Nyalandu alisema baada ya kutafakari kwa muda mrefu na kujikagua kwa kina, ameona anao uwezo wa kutosha wa kupokea kijiti kutoka kwa Rais anayemaliza muda wake mwakani kwa mujibu wa Katiba.
Mbali n Nyalandu, wengine ambao wametangaza kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Ambao hawajajitangaza, lakini wanatajwa kuusaka urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles