26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

Pinda: Nachafuliwa vita ya urais

Mizengo-Pinda

Na  Walter Mguluchuma, Katavi
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema hahusiki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Pinda alisema watu wanaomtuhumu kuhusika na kashfa ya Escrow, wana lengo la kumchafulia mbio zake za kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Alisema yeye ni mtu mwadilifu, hajawahi kupokea au kutoa rushwa kwa mtu yeyote katika maisha yake.
“Sijawahi kutoa wala kupokea rushwa maishani mwangu, hata tuhuma zinazoelekezwa kwangu kuwa nilipewa mgawo kwenye kashfa ya IPTL hazina ukweli.
“Nina uhakika hata siku moja haitatatokea nikakamatwa kwa kosa la rushwa,” alisema Pinda.
Alitoa kauli hiyo juzi mjini hapa, wakati akihutubia wananchi wa Mkoa wa Katavi katika sherehe za kuaga mwaka 2014 na kukaribisha mwaka 2015 zilizofanyika kwenye Hoteli ya Lyambalyamfipa.
Alisema wapo baadhi ya watu ambao walipanga kumchafua wakati wa kikao cha Bunge kilichomalizika Novemba, mwaka jana.
“Kikao kilichopita cha Bunge pale Dodoma, kuna watu walipanga kunichafua, kulikuwa na kitimoto kwelikweli, sitasahau,” alisema Pinda.
Alisema kwa vile katika maisha yake amekuwa mwadilifu, hataraji kupokea rushwa iwe ndani ya nchi au nje.
“Nawahakikishia Watanzania kwamba mimi ni mtu safi na mwadilifu, haya mengine ni nambo ya watu ambao wana maslahi yao binafsi,” alisema Pinda.
Alisema baada ya kumalizika kikao cha Bunge mwaka jana, makundi mbalimbali ya watu wa ndani na nje ya nchi yamekuwa yakimpa pole.
Pinda alisema makundi hayo yamemsaidia moyo wa kulitumikia zaidi taifa.
“Hata nilipofika kijijini kwangu Kibaoni kwa ajili ya mapumziko ya Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, nimekuwa nikipokea watu mbalimbali kutoka mikoa ya Katavi na Rukwa, wanakuja kunipa pole,” alisema.
Alisema miongoni mwa watu hao, ni viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini.

KUHUSU SETHI
Alisema anashangazwa kuhusishwa na mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Singh Sethi akisema hamfahamu wala hajawahi kumwona katika maisha yake.
“Simjui Singh, sijawahi kukutana naye… iweje leo anipatie fedha zake? Huu ni uzushi,” alisema Pinda.
Alisema licha ya kuwapo na kashfa hiyo, yeye ataendelea kumtii Rais Jakaya Kikwete.
“Kila siku najitahidi kumsaidia Rais Kikwete kufanya kazi, nitaendelea kuwa mwadilifu kwake, Serikali na kwa wananchi wa Tanzania,” alisema.

DIWANI CHADEMA
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Makanyagio, katika Halmashauri ya Mji wa Mpanda, Idd Nzguye (Chadema), amemwahidi Waziri Mkuu Pinda kuwa atamlipia fedha za kuchukua fomu ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu, mwaka huu.
Nzguye alitoa ahadi hiyo juzi, wakati wa sherehe za kuaga mwaka 2014 na kukaribisha mwaka 2015.
Alisema ameridhishwa na utendaji kazi wake, hivyo haoni sababu ya msingi ya kushindwa kumlipia gharama hizo.
Nzguye alisema kwa vile Pinda anaishi Kata ya Makanyagio na yeye ndiye diwani, litakuwa jambo la busara akiumuunga mkono.
Alisema ni jambo la kujivunia kwake kuona mgombea urais anatoka eneo lake analotawala.
“Sioni sababu yoyote ya kutomlipia kutokana na mchango mkubwa wa kusimamia shughuli za maendeleo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2008,” alisema Nzguye.

DODOMA
Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati, Amon Kinyunyu, amemtaka Rais Kikwete kuchukua hatua kali kwa watu wote wanaotuhumiwa kuchota fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Askofu Kinyunyu alitoa kauli hiyo jana wakati wa ibada ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2015.
“Nawataka Wakristo mwaka 2015 waanze kwa jina la Bwana, wakimtanguliza Yesu kwa kufanya hivyo, utakuwa ni mwaka wa amani.
“Lakini kubwa ni rais wetu asikae kimya kwenye mambo mazito na kuyafumbia macho.
“Anatakiwa atoe ufafanuzi kwa sababu wapo watu waliochota fedha, lakini wapo mitaani wanaendelea kudunda na kutamba kwamba hawafanywi kitu,” alisema.
Alisema bila hatua madhubuti kuchukuliwa, nchi inaweza kujikuta katika matatizo makubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles