27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MZEE WA UPAKO ACHUNGUZWA

*Ushahidi ukipatikana kufikishwa mahakamani

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM


 

mzee-wa-upako POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inaendelea kufanya upelelezi dhidi ya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, anayetuhumiwa kufanya fujo na kutukana.

Mzee wa Upako, ambaye yuko nje kwa dhamana, alidaiwa kuwatukana baadhi ya majirani zake waliosema kuwa aliwazibia njia kwa kupaki gari lake eneo la kupita.

Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema upelelezi wa tukio hilo la ugomvi wa majirani unaendelea kwa kuwahoji mashuhuda.

“Ni kweli alikamatwa na polisi baada ya majirani kupiga simu kuwa aliziba njia, alipewa dhamana na mashahidi wapo wanahojiwa. Ni ugomvi wa majirani na majirani. Alikuwa amezuia na gari nyumba ya jirani kiasi hawezi kutoka na lugha za matusi, wapelelezi watatuambia,” alisema Sirro.

Pia alisema iwapo ushahidi wa kutosha ukipatikana, watamfikisha Mzee wa Upako mahakamani kujibu shitaka lake.

Kuhusu madai kuwa wakati Mzee wa Upako anafikishwa polisi alikuwa na kiwango kikubwa cha ulevi, Sirro alisema hana taarifa za uhakika kuhusu hilo.

“Siwezi kulizungumzia hilo, sina uhakika nalo, sikumpima, wenzangu wa Kinondoni walimpima, hadi nicheki nao,” alisema Sirro.

Mzee wa Upako alikamatwa juzi maeneo ya Kawe, wilayani Kinondoni, akidaiwa kufanya fujo kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa tatu asubuhi alipochukuliwa na polisi wa Kituo cha Kawe.

Taarifa za Mzee wa Upako kufanya vurugu zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, huku video aliyorekodiwa eneo la tukio, ikimuonyesha gari ikiwa imepaki barabarani huku akizungumza kama aliyelewa chakari.

Chanzo cha tukio hilo kilidaiwa ni kulipiza kisasi kwa jirani zake hao wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348, ambao alidai wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.

Ilidaiwa kuwa, baada ya purukushani hizo, polisi kutoka Kituo cha Kawe walifika na kumchukua Mzee wa Upako, kisha wakampeleka kituoni na kupimwa kiwango cha ulevi kilichogundulika kufikia 131, kinachoelezwa kuwa ni kikubwa.

Ilipofika saa tano asubuhi juzi, Mzee wa Upako alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana kushuka hadi kufikia 121.

Jana MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Mzee wa Upako kwa njia ya simu ya mkononi lakini hakupatikana na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu. Lilipofika asubuhi katika kanisa lake lililopo Ubungo Riverside, kulikuwa na ukimya tofauti na siku nyingine ambazo kwa wakati huo huwa kuna ibada inaendelea.

Juni 5, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alikwenda kusali katika kanisa hilo na kuahidi kumjengea barabara inayoingia kanisani hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles