31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AMKUNA TENA JPM

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM


 

paul-makondaPAMOJA na kuingia katika mgogoro mzito wa kikazi na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameonekana kumkuna Rais Dk John Magufuli kupitia ziara aliyoianzisha wiki hii ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Makonda, ambaye  jana alikuwa katika Wilaya ya Ubungo, wakati akisikiliza kero za wananchi, Rais Magufuli alimpigia simu kumpongeza kwa  ziara  hizo anazozifanya katika maeneo mbalimbali na amewataka wakuu wengine wa mikoa kuiga mfano huo.

Makonda  amepewa  pongezi hizo  wakati kukiwa na hisia tofauti tofauti, baada ya kuingia katika mgogoro na viongozi wa juu wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Hivi karibuni Makonda aliwashtaki kwa Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Suzane Kaganda, akiwahusisha na kupokea rushwa kutoka kwa wauzaji wa kilevi cha shisha, baada ya kushindwa kudhibiti biashara hiyo.

Akizungumza na Makonda kwa njia ya simu ambayo iliunganishwa moja kwa moja kwenye vipaza sauti na hivyo wananchi kumsikia, Rais Magufuli alisema:

“Natamani wakuu wa mikoa wangekuwa wanafanya kazi kama wewe ya kusikiliza wananchi kero zao na kutoa ufafanuzi,  nakupongeza wewe na wakuu wako wa wilaya, endelea hivyo kutembelea wananchi, kutoa ufafanuzi maana ungetolewa mapema watu wasingeuliza,” alisema Magufuli, huku Makonda akimuitikia.

Alisema Makonda anatakiwa kuwasikiliza wananchi hao bila kujali vyama walivyotoka, dini, kabila wala uwezo walionao kifedha, kwakuwa wana shida nyingi zinazohitaji utatuzi, huku  viongozi wakijifungia ofisini.

“Sisi viongozi tumejifungia mno ofisini, mwiko huu wewe umeutatua, hatua unazochukua kwa kushirikiana na wakuu wako wa wilaya endelea nazo hivyo hivyo, una support yangu, endelea kutumbua huko huko kuanzia chini,” alisema Rais.

Rais Magufuli alitumia pia nafasi hiyo kukumbushia msimamo aliowahi kuuweka tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi wa kubomoa majengo yote yaliyopo katika hifadhi za barabara, likiwemo jengo la Shirika la Umeme (Tanesco) lililopo Ubungo.

Alisema bomoa bomoa hiyo ambayo Serikali haitotoa fidia kwa mtu yeyote, itafanyika katika eneo la Ubungo kwa   lengo la kujenga barabara za mchepuko  mbili hadi tatu ili kurahisisha usafiri.

“Wananchi wa Ubungo wanapaswa wajue kuvunja kupo pale pale kwa sababu tumepata Sh bilioni 67 za kujenga interchange (barabara za mchepuko) katika eneo la Ubungo itakayokuwa na  ghorofa mbili mpaka tatu ili kurahisisha usafiri.

“Katika ujenzi huo majengo yatavunjwa bila fidia, hata kama litakuwa jengo la Tanesco kwa sababu ni lazima tuzingatie sheria, wananchi wakiona wanaonewa waende mahakamani, maana  ndiyo sehemu pekee pa kutafsiri sheria,” alisema  Rais Dk. Magufuli.

Alisema Serikali inafanya uamuzi wa kubomoa nyumba zilizopo katika hifadhi za barabara kwakufuata uamuzi wa kesi iliyoshinda namba 137, ambayo iliwahusu walalamikaji waliojenga katika maeneo hayo.

Alisema kesi hiyo ilitolewa  uamuzi na Mahakama Kuu mwaka 1997, ambayo hayawezi kubatilishwa na hakimu yeyote nchini.

“Baada ya ushindi tulichukua hatua ya kubomoa nyumba zote zilizopo katika hifadhi ya barabara kwa sheria hiyo, ilianza tangu za ukoloni amendment (marekebisho) 1946 na 1954 na marekebisho ya mwisho yalifanyika 1965,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kupitia kesi namba 167 yalifanyika mabadiliko sheria namba 13 ya 2007, ambayo inazungumzia hifadhi ya barabara.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, sheria ya watu kuzuiwa kujenga katika hifadhi za barabara ipo tangu mwaka 1932, hivyo wananchi kutokujua sheria si sababu ya kutokutekeleza sheria.

Alisema mbali na hiyo, katika sheria ya ardhi namba nne ya mwaka 1999 na ya Vijiji namba 1999 pamoja na ile sheria ya Mipango Miji na Matumizi ya Ardhi ya 2007, yote inatambua hifadhi za barabara.

“Kwa barabara ya Dar es Salaam  kwenda Kibaha iliachwa kutoka Ubungo hadi Askari Monument, upana wake ni  mita 22.5 kila upande, baada ya Ubungo pale jengo la Tanesco upana unapanuka, ndiyo maana  siku moja nilizungumza hata Tanesco lipo katika hifadhi ya barabara,” alisema Magufuli.

Aliwataka wananchi wazingatie sheria  zilizotungwa na endapo wataziona hazifai walishauri Bunge kuzibadili ili barabara ya Ubungo iwe na sentimeta tano ambayo itakuwa na uwezo wa kupitisha bajaji tu.

“Lakini tofauti na hapo, sheria ndiyo hiyo, watakwenda kwa wanasheria hakuna kitakachobadilika.

“Na tukifanya hivyo ipo siku tutajikuta hatuna barabara, ndiyo maana ofisi iliyokuwa ya Wakala wa Barabara (Tanroads) pale Ubungo nilikwenda kuivunja mwenyewe kwa sababu niliona ipo kwenye hifadhi ya barabara,” alisema Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles