22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

MZEE MIAKA 76 ATUMIA MADALALI KUSAKA MKE

gari

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MZEE Athuman Mchambua (76) ambaye anatafuta mwanamke wa kuoa amesema anafikiria kutumia madalali nchi nzima ili kuweza kumrahishia kazi ya kupata mke anayemtaka kwa mujibu wa vigezo alivyoweka.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam,  alisema baada ya kufikia ukomo wa tangazo la awali Desemba 10 (kesho),  anatarajia kutumia madalali ili kuharakisha mchakato huo.

Mzee huyo mwenye watoto 15 kati yao wa kike wanne na wa kiume 11, alisema anafikiria kutumia madalali ambao atawasambaza sehemu mbalimbali nchini, ili kufanikisha azma yake.

“Kila dalali atakuwa na sifa ambazo ninahitaji japo mpaka sasa sijajua ni kiasi gani nitakachowalipa lakini nitaangalia ni kwa jinsi mtu atakayeleta mwanamke mwenye sifa ninazohitaji basi nitamlipa pesa nyingi zaidi,” alisema mzee huyo.

Alisema anaamini ni lazima zoezi hilo litafanikiwa, ingawa hadi sasa kati ya wanawake waliojitokeza wapatao 30 inaonekana kigezo cha kilimo kwao imegeuka mwiba.

“Nimeamua kuweka kigezo hiki cha kilimo kutokana kwamba maisha yanabadilika kwani hata hizi nyumba nilizonazo linaweza kutokea la kutokea zikavunjwa au hata maisha yakayumba hivyo nikalazimika kurudia shamba hivyo ni lazima kuwa na mwanamke aliyetayari kuishi maisha ya namna yoyote,” alisema.

Akizungumzia juu ya kufikia ukomo kwa tangazo hilo hapo kesho, Mchambua alisema licha ya kufikia tamati lakini bado ataendelea na utaratibu wa kupokea maombi ya simu iwapo yatajitokeza.

“Kwa sasa tangazo hili litafikia ukomo Desemba 10 (kesho) ambapo itakuwa ni mwisho wa kutangaza lakini endapo simu zitamiminika mimi nitazipokea kama kawaida, lakini kwasasa nataka nifanye mchujo wa hawa niliowapata,”alisema Mchambua.

Katika hatua nyingine mzee Mchambua alisema jambo lililomsukuma hadi aweke tangazo la aina hiyo kuwa ni msiba wa marehemu mke wake aliyefariki dunia mwaka huu na kwamba iwapo angekuwa hai basi asingehangaika kusaka mke.

“Najua kuwa umri wangu umekwenda lakini hii haina maana kuwa sistahili kuwa na mke kwani ndiyo naishi na watoto wangu lakini hawawezi kunifanyia kila kitu.

“Mimi ni mtu na nguvu zangu na niko imara hivyo siwezi kuacha kusaka mke kwani nahitaji mtu atakayeniangalia mimi pamoja na familia yangu,” alisema.

Atoa ushauri kwa wazee

Alisema mfumo huo wa kusaka mke kwa njia ya matangazo unapaswa kuigwa na wazee wengine kama yeye kwani unasaidia kumpata mwanamke ambaye ni chaguo sahihi.

“Nawashauri pia wazee wengine na wanaume kwa ujumla kutumia mfumo huu wa matangazo ili tuweze kuendana na teknolojia ya kisasa inavyotaka, hili siyo jambo la ajabu bali nilakuungwa mkono na wengine,” alisema.

Watoto

Mmoja wa watoto wa mzee huyo, Damiya Athuman alisema wao kama watoto wanamwunga mkono baba yao huyo na kwamba wako nyuma yake katika kuhakikisha kuwa jambo hilo linafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Upande wetu tumepokea vizuri sababu mlezi wetu ameshaondoka hivyo hata akija mwingine siyo mbaya sababu sasahivi sisi tushazaa, lakini mpaka sasa kwa wote waliokuja bado hatujapata anayefaa.

Maisha yake

Mzee Mchambua alisema kuwa maisha yake kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakitegemea kilimo kwani ndicho kinachomwingizia kipato.

“Mimi ni Mndengereko, naishi na baadhi ya wanangu napenda wanawake sina kazi nyingine zaidi ya kilimo na udereva wa gari yangu mwenyewe kilichosalia ni kula na kulala pekee hivyo sina shughuli nyingine.

“Lakini pia kama hiyo haitoshi ninavibanda vya biashara ambavyo vimekuwa vikiniingizia hela ya kula kwani kipato changu kwa siku siyo chini ya 5,000,” alisema.

Mali alizonazo

Mzee Mchambua alisema kuwa mali alizonazo ni nyumba tatu ambazo zipo jijini Dar es Salaam, mashamba ambayo yapo wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani pamoja gari moja ambalo humsaidia katika shughuli zake.

“Nyumba zangu tatu ambazo zote zinafanya biashara kwa kuniingizia kipato cha kila siku, lakini sitaki kusema mali nyingine nilizonazo maana wanawake wanaweza kuumizana hapa kwa kufuata mali badala ya kufuata ndoa kama ninavyohitaji,” alisema.

Akumbuka mwenza wake

Mzee Mchambua alisema, awali kabla ya kuingia kwenye mchakato huo wa kutafuta mke mwingine wa kuoa tayari aliwahi kuwa na wake wawili japo mke wake mkubwa, Hadija Bakari alifariki duania mwanzoni mwa mwaka huu na kubaki na mke mdogo ambaye yuko anaishi shamba.

“Najua kuwa iwapo ningemwambia mke mdogo kuwa nahitaji kuongeza mke mwingine kwa vyovyote lazima asingenikubalia badala yake nimeamua kufanya maamuzi mimi mwenyewe.

“Lakini nachoshukuru ni kwamba mke mdogo ambaye nimeishi naye kwa miaka 10 sasa anajua kama nilikuwa na mpenda sana mke wangu mkubwa kwani yeye amekuwa ni mtu wakunipikia chakula pindi ninapokuwa shamba na kuangalia mazao ila huyu ninayemtafuta sasa hivi yeye atakuwa ni wa huku,” alisema.

Aliopoulizwa iwapo mke wa kwanza naye alimpata kwa njia hiyo ya matangazo alisema hakutumia njia hiyo na badala yake alifuta utaratibu wa kawaida ikiwemo kutuma mshenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles