*Achukizwa January kutumia picha aliyopiga naye mitandaoni
Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema kitendo cha makatibu wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kuandika waraka kuhusu hali ya kisiasa nchini, ni utoto.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa zimepita siku chache tangu viongozi hao walipoandika waraka kwenda Baraza la Viongozi Wastaafu na kuzua gumzo kwa viongozi na wananchi wa kada mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa Mwinyi hakubaliani na jambo hilo.
“Kuhusu waraka ulioandikwa na makatibu wakuu wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kwenda kwa Baraza la Viongozi Wastaafu, ni utoto,” alisema Mwinyi.
Alipongeza majibu yaliyotolewa na Katibu wa Baraza hilo, Pius Msekwa na kusema walioandika waraka huo wameshindwa kufuata katiba na taratibu za chama.
“Viongozi wastaafu hawawezi kupoteza muda wao kwa masuala ya kitoto,” alisema.
Aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya za kuleta maendeleo kwa muda mfupi.
Alisema ukiondoa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, viongozi wengine waliofuata akiwemo yeye, wamefanya juhudi za kuipeleka nchi mbele, lakini kasi ya Rais Magufuli ni kubwa zaidi.
JANUARY MAKAMBA
Katika hatua nyingine, Mwinyi ameelezea kutofurahishwa kwake na kitendo kilichofanywa na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba kutumia picha yake katika mitandao ya kijami muda mfupi baada uteuzi wake kutenguliwa.
Alisema picha iliyotumiwa na January katika mitandao ya kijamii, ikimuonesha yeye ameketi naye wakicheka muda mfupi baada ya kufukuzwa uwaziri imemkwaza kutokana kutumiwa katika mazingira na wakati usiostahili.
Mwinyi alisema picha hiyo ilipigwa zamani wakati January alimpomtembea kupata uzoefu wake kwa kuwa naye aliwahi kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira.
“Alikuja kuniomba niandike dibaji katika kitabu chake, sasa picha yangu imetumika vibaya katika hili,” alisema.
WARAKA WA KINA KINANA
Makamba na Kinana waliopata kushika nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM kwa kufuatana wakati wa Serikali ya awamu ya nne, walitoa taarifa ya maandishi kwa umma wiki iliyopita wakilalamika kudhalilishwa na mmoja wa makada wa chama hicho, huku wakiweka bayana kwamba wamezingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122.
“Tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.
“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo,” walisema katika barua hiyo.
Vilevile walisema wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu taarifa wanazodai za uzushi kwa nyakati mbili tofauti.
Walisema kwa sasa Watanzania wanajua kuwa yanayosemwa na mtu huyo si ya kwake.
Kwamba mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo (wamemtaja, lakini jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma) anatumwa na nani.
“Pili anakingiwa kifua na nani? Tatu anatumika kwa malengo gani? Na nne nini hatima ya mikakati yote hii.
“Tafakari yetu inatupeleka kupata majibu yafuatayo; kwanza kwa ushahidi wa kimazingira mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.
“Pili zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu,” walisema katika barua hiyo.
Katika hoja yao ya tatu, walisema mtu huyo anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha viongozi, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa.
“Nne, kuna kila dalili kuwa lengo na hatima ya mkakati huu ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.
“Tumeamua kutochukua hatua za kisheria kwa sasa kwa sababu kwanza jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwa hiyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa.
“Pili, unapochafuliwa, unachokwenda kudai mahakamani ni fidia. Kwetu sisi, heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia,” walisema.
Wakizungumzia kuhusu chanzo cha tuhuma hizo, wazee hao walisema wanaamini kuna sehemu zinatoka.
“Yeye anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu. Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu. Katika mazingira hayo, hatuwezi kukaa kimya,” walisema.
Hata hivyo baada ya viongozi hao kutoa waraka huo wamekuwa wakipingwa na watu wa kada mbalimbali wakiwamo wabunge wa chama hicho tawala.