Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, amewataka wataalamu wa afya kufanya utafiti zaidi wa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
Alisema hatua hiyo inaweza kurahisisha utoaji wa matibabu ya ugonjwa huo nchini.
Mwinyi alikuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa Hospitali ya JPM, mtaa wa Kagera Dar es Salaam jana.
Alisema kupatikana kwa dawa za wagonjwa wa moyo kutasaidia kupunguza gharama za matibabu nchini.
Idadi ya wagonjwa wa maradhi hayo inaongezeka siku hadi siku jambo ambalo limewafanya watalaamu kuhangaika waweze kupata tiba itakayowasaidia wagonjwa hao.
“Maradhi ya moyo ni miongoni mwa maradhi yanayowasumbua wananchi wengi hivyo basi watalaamu wanapaswa kufanya utafiti waweze kupata tiba ambayo itawasaidia wagonjwa hao,” alisema Mwinyi.
Alisema kwa sababu hiyo, wadau wa afya wanapaswa kushirikiana na serikali kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.
Lengo la wananchi ni kupata huduma bora ya matibabu kwa gharama nafuu, alisema.
Aliwataka wamiliki wa hospitali hiyo kutoa huduma ya gharama nafuu ili wananchi wasio na kipato kikubwa waweze kwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Ameir Binzoo, alisema hospitali hiyo itatoa huduma bora ya afya na kwa gharama nafuu ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunatoa huduma bora ya afya na kwa gharama nafuu wananchi wengi waweze kujitokeza kupatiwa huduma ya matibabu, jambo linaloweza kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali za serikali,”alisema Binzoo.
Aliiomba serikali kushirikiana na hospitali za watu binafsi ili kubadilishana uzoefu kusaidia kuwaunganisha katika hospitali za kimataifa kwa ajili ya kupata wafadhili watakaoweza kuchangia gharama za huduma za matibabu.