NA MALIMA LUBASHA, SERENGETI
Mwili wa mtalii raia wa China aliyefariki katika ajali ya gari la watalii juzi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakati yeye na wenzake wakielekea hotelini, umeondolewa leo Julai 31,2024 katika hospitali ya Nyerere DDH Mugumu, Serengeti na kupelekwa Arusha kwa maandalizi ya kusafirishwa kwenda China.
Ajali hiyo imetokea Julai 28,2024 saa 10.00 jioni ambapo ndani ya gali hilo kulikuwa na watalii saba wakati wakirudi kwenye hoteli iliyopo ndani ya hifadhi ya Serengeti.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Ediga Saulo, amezungumza na waandishi wa habari na kumtaja marehemu kuwa ni Wuyi China Liaoningi.
Dk. Saulo amesema Julai 28 kuamkia Julai 29,2024 majira ya saa 5.00 usiku walipokea mwili wa marehemu na majeruhi 5 watalii raia wa china waliofikishwa hapo hospitalini hapo kwa matibabu.
Dk.Saulo amesema kati ya majeruhi watano waliopokea wanne walikuwa wamepata majeraha madogo na moja ndiye alipata majeraha makubwa hivyo baadaye kupewa rufaa kwenda Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo Mganga mkuu huyo amewataja majeruhi kuwa ni Yong Jungzhou,Chen Chen, Guang Chenxin, Yan Yan Chen na Bu Ke Li.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania(TANAPA)ambayo ilisema ajali hiyo imehusisha gari lenye namba za usajili T 603 DCL likiendeshwa na dereva mtanzania likiwa na watalii saba wakiwa njiani kwenda Lobo WildLife.