Na Ramadhan Hassan, Dodoma
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), Benki Kuu Tanzania (BoT), Wizara ya Fedha na Mipango na Wafanyabiashara wamesema mwenendo wa viashiria vya kiuchumi vya muda mfupi Januari –June 2021 umeendelea kuimarika kutokana na vichocheo mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Septemba 8, jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Takwimu za Kiuchumi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa, wakati akitolea ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu viashiria vinne vyenye mchango kwenye uchumi wa nchi.
Amevitaja viashiria hivyo kuwa ni  idadi ya watalii kuongezeka, uzalishaji wa saruji, huduma za mawasiliano na uzalishaji wa Nishati ya umeme.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa idadi ya watalii imeendelea kuongezeka ambapo kati ya Januari hadi Juni 2021, kiwango cha watalii walioingia nchini kiliongezeka kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na kiwango hasi cha asilimia 43.6 kipindi kama hicho Mwaka 2020.
Amesema idadi ya watalii walioingia nchini mwezi Juni 2021 walikuwa 57,689 ikilinganishwa na 9,671 walioingia nchini mwezi Juni 2020,” amesema Masolwa.
Kwa upande wa Uzalishaji wa Saruji nchini ameeleza kuwa umeendelea kuimarika ambapo ukuaji umeongezeka kwa kiwango hasi cha asilimia 0.6 kutoka kiwango hasi cha asilimia 5.1.
“Pamoja na kwamba huduma nyingi za kiuchumi ziliathiriwa na UVICO-19, huduma za Mawasiliano zimeendelea kuongezeka kutoka dakika za kuongea bilioni 31.3 kipindi cha Januari hadi Juni Mwaka 2019 hadi dakika bilioni 42.9 kipindi kama hicho Mwaka 2021,” amesema.
Pia, amesema katika sekta ya mawasiliano viashiria vimeongezeka kutokana na watu wengi kutumia  matumizi ya video Conference  wakati wa UVICO-19 kuendesha mikutano kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi huyo wa Takwimu za kiuchumi ameeleza kuwa uzalishaji wa Nishati ya umeme mwenendo wake umeendelea kuwa imara ambapo uzalishaji umeongezeka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Takwimu za Sensa na Takwimu za Jamii, Luth Minja amesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa Mwaka ulioishia mwezi Agosti,2021 umebaki kuwa asilimia 3.8 kama ilivyokuwa kwa Mwaka ulioishia mwezi Julai, 2021 .
Amesema kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti ,2021 imekuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Julai,2021.
Naye,Mwenyekiti wa Soko Kuu la Majengo la Jijini hapa,Eliaman Mollel amesema ongezeko la bei katika soko hilo zimepungua hususani kwenye vyakula ambapo amedai kwa sasa vyakula vipo vingikutokana na wakulima kulima kwa wingi.
Kwa upande wake,Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mbayani Sabuni amesema hali ya mfumuko wa bei nchini ipo vizuri ukilinganisha na Nchi zingine.
Mchumi Mkuu kutoka Benki kuu ya Tanzania (BoT) Stanslaus Mrema amesema kúwa kazi yao ni kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa bei kwenye mzunguko wa biashara.
“Mfumuko wa bei uliotulia ndio unaoleta maendeleo kwa wananchi.Tunafanya kazi kutekeleza malengo ambayo Serikali imejiwekea kwa kuzingatia viwango vya ukuaji wa uchumi,tumepewa jukumu la kusimamia mfumuko wa bei na lengo la kukuza uchumi,”amesema.