24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwarobaini wa Lugumia kuanza leo

HILALYNa Bakari Kimwanga, Dodoma

KAMATI ndogo ya Bunge ya uchunguzi wa mkataba tata kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises, leo inaanza kuchimbua figisufigisu zilizojificha   kwa kuanza kukagua mashine na kuwahoji vigogo wanaotajwa kuhusika.

Kamati hiyo  inayoongozwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), pamoja na wajumbe wake wanane, itakwenda kila pembe ya nchi kukagua mashine hizo za kuchukua alama za vidole.

Kamati hiyo mbali na kufanya uchunguzi huo, itawahoji vigogo wote waliotajwa katika mkataba huo tata wa Sh bilioni 37 na baada ya kazi hiyo kukamilika itawasilisha matokeo bungeni kwa ajili ya uamuzi.

Uamuzi wa kuundwa kamati hiyo, ulitangazwa juzi mjini hapa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aeshi Hilaly,  baada ya kupata kibali cha Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye aliagiza iundwe  kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Wajumbe wa Kamati hiyo ndogo ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ni Dk. Haji Mponda (Malinyi-CCM), Mbunge Dimani, Hafidhi Ali Tahir (CCM), Mbunge wa Nyamagana, Stanlaus Mabula (CCM).

Wengine ni Mussa Mbaruku (Tanga Mjini-CUF), Tunza Malapo (Viti Maalumu-Chadema), Naghenjwa Kaboyoka (Same Mashariki-Chadema) na Mbunge wa Viti Maalumu, Khadija Nassor Ali (CUF).

Kamati hiyo ambayo inaanza kazi leo, itafanya kazi zake kwa siri  kwa   mwezi mmoja,   na pamoja na mambo mengine, itakabidhiwa hadidu rejea ya namna itakavyofanya kazi  hiyo,

Wajumbe wa kamati  watakwenda katika kila kituo kilichofungwa mashine hizo nchi nzima  kubaini ukweli na  thamani ya fedha kama inalingana na uhalisia wa mashine hizo.

“Kama mnakumbuka awali tuliomba taarifa ya utekelezaji wa mkataba na tumeletewa na Jeshi la Polisi lakini bado kuna baadhi ya maeneo yanahitaji maelezo ya kina. Watakapokamilisha kazi yao hii taarifa itawasilishwa Bungeni zikiwamo   hatua za kuchukuliwa kama mapendekezo ya Kamati yetu na kisha Bunge litaamua,” alisema Aeshi.

Alisema baada ya kuwasilishwa   taarifa hiyo, walihojiwa   viongozi wa Jeshi la Polisi   na wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  ambao  walidai mashine hizo za kuchukua vidole zimefungwa maeneo yote lakini   kamati hiyo inataka kujiridhisha kwa kina.

“Hatua ya kuundwa kamati ndogo imetokana na hoja yetu ambayo tuliwasilisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye naye aliridhia kuundwa   kamati hii,” alisema Aeshi.

Taarifa kutoka ndani kamati hiyo zinaeleza kuwa licha ya wajumbe hao wa kamati ndogo kukagua mashine hizo, pia watawahoji vigogo wote waliotajwa kuhusika katika mkataba huo yakiwamo makampuni yaliyoshiriki.

Katika mkataba huo, pia wanatajwa Waziri wa Rais Dk. John Magufuli  na kigogo mmoja wa Mamlakka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuwa sehemu ya wahusika wa mkataba huo tata.

Chanzo chetu kilisema   katika kikao hicho cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, wajumbe walihoji taarifa hiyo ya utekelezaji wa mkataba huo  na kuonyesha hofu ya kuwapo   ‘wingu la ufisadi’.

“Zabuni ilitangazwa Septemba 22, mwaka 2011 na mkataba  ukasainiwa Septemba 23  mwaka huo huo… ndani ya siku moja mkataba ukasainiwa jambo ambalo ni hatari.

“Halafu jambo jingine linaloshtua, tangu wakati huo mashine zote wanasema zipo lakini hazifanyi kazi.

“Swali ambalo wajumbe walikuwa wanahoji ni inakuaje wanatoa zabuni  bila kufanya ‘fiacibility study’ ya kina  kujua uwezo wa hii kampuni ya Lugumi kama ilishawahi kufanya kazi ya aina hii ama laa?” aliuliza.

Kamati hiyo pia imebaini tofauti ya fedha katika mkataba huo ambako wakati taarifa ya Jeshi la Polisi inaonyesha  walitoa Sh   37,163,940,127.7, taarifa ya Ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  inaonyesha fedha zilizotolewa ni Sh   37,742,913.007 ikiwa na tofauti ya Sh milioni 500.

Vigogo hao wa Jeshi la Polisi walipotakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusu zilipo Sh  milion 500, walishindwa hali iliyofanya  wajumbe wa PAC wageuke mbogo na kutaka suala hilo litolewe maelezo ya kina.

Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd inadaiwa kupewa tenda na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 tu vya polisi wakati  kampuni hiyo imekwisha kulipwa Sh bilioni 34 ambazo ni   asilimia 99 ya fedha za mkataba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles