BENJAMIN MASESE-MWANZA
Siku chache baada ya Serikali mkoani Mwanza kuweka maazimio 14 kwa walimu wakuu, maofisa elimu wa kata na taaluma ili kuinua ufaulu kwa shule za msingi 2019/2020, imeanza kutekeleza kwa vitendo kwa wanafunzi wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa taifa katia ya Septemba 11-12, mwaka huu.
Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola kwa kushirikiana na maofisa elimu taaluma wa wilaya wamelazimika kutunga mtihani unaofanana na ule wa taifa na kuwakutanisha wanafunzi wa shule mbalimbali katika kituo kimoja ili kujipima.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Ligola, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Longino Ludovick amesema lengo la Serikali ya mkoa ni kuhamasisha, kuboresha taaluma na kuwaandaa wanafunzi kuelekea mtihani wa taifa.
“Leo kama unavyoshuhudia tumezikutanisha shule nne ambazo ni Butimba A na B, Bwiru na Gedeli ambazo zimetoka Ilemela na Jiji la Mwanza, hizi shule tumezikutanisha kwa sababu katika mtihani wa mock zilifanya vizuri hivyo tunataka kuona ipi inaongoza, shule itakayofaulisha wanafunzi wengi watapata zawadi ya pesa na mbuzi ya kwa ajili ya kitoweo cha mahafali,” amesema.
“Kwa wiki moja au mbili zilizobaki tutaendelea katika shule nyingine na changamoto zitakazojitokeza tutazifanyia kazi haraka kabla ya mtihani wa taifa, mitihani hii imetungwa na jopo la maofisa elimu kutoka mkoani na wilayani ndio maana unatuona hapa tukishughulika katika kituo hiki cha Shule ya Msingi Nyanza,”alisema.
Amesema utaratibu uliowekwa katika mtihani umezingatia masharti yote kama ilivyo ule wa taifa ambapo wanafunzi wa shule hizo walichanganywa pamoja huku kila mmoja na dawati lake.