NA ALLAN VICENT – Tabora
SERIKALI mkoani Tabora imeagiza kukamatwa wazazi na walezi wanaotumikisha watoto wenye miaka chini ya 18 katika kazi ngumu za kiuchumi ikiwemo kilimo cha tumbaku na mpunga.
Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa, Aggrey Mwanri, wakati wa mahojiano maalumu na kituo kimoja cha redio mjini hapa.
Mwanri aliitaka jamii kuwapa malezi mazuri watoto wao na kuacha mara moja tabia za kuwatumikisha katika kazi hatarishi kwa maisha yao.
Alisema mtoto yeyote aliye na umri chini ya miaka 18 hapaswi kuajiriwa au kufanyishwa kazi ngumu, ikiwemo za kilimo bali ahamasishwe kujisomea, hasa katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kutokana na ugonjwa wa corona.
Alisisitiza kuwa mtu yeyote anayetumikisha mtoto mdogo ikiwemo kumwajiri hana akili.
“Kuanzia sasa yeyote atakayebainika kuwatumikisha watoto atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Mwanri.
Aliagiza wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na watendaji wa vijiji na kata kusaka wazazi na walezi wote wanaotumikisha watoto katika shughuli zao za uzalishaji mali na kuwachukulia hatua kali.
“Ma-DC fanyeni msako katika maeneo yote ikiwemo kwenye mashamba ya tumbaku, pamba na mahindi, somba watu wote mtakaokuta wanatumikisha watoto, atakayeleta ubishi ‘tutambamiza’,” alisema Mwanri.
Alisema kuwa ni marufuku kwa mzazi au mlezi yeyote kutumia mtoto mdogo kama kitega uchumi chake, huku akionya kuwa yeyote atakayekaidi agizo hilo na kuendeleza vitendo hivyo akikamatwa atabamizwa kisawa sawa.
Akichangia mada katika kipindi hicho, Mkurugenzi wa Voice of Tabora ya mkoani hapa, Ismail Aden Rage alipongeza uamuzi wa Serikali ya mkoa kulivalia njuga suala hili ili kuokoa kizazi cha viongozi wa kesho.
Ofisa Maendeleo wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Tumaini Mganya aliwataka wazazi na walezi kuacha kutumia watoto kama fursa ya kuwaingizia mapato bali wawape malezi yanayostahili ili nao waweze kufikia ndoto zao.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa manispaa hiyo, Rose Maila alisema kuwa watoto wanaotumikishwa katika kazi za uzalishaji mali wako katika hatari kubwa sana ya kuambukizwa ugonjwa hatari wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).
Wakichangia mada kwa njia ya simu, baadhi ya wananchi walisema kuwa vitendo vya utumikishwaji watoto vimekuwa vikiongezeka huku vikichochewa na wazazi au walezi wasiojali, hivyo wakaomba hatua kali zichukuliwe ili kuvikomesha.
Juma Abdul mkazi wa Ipuli, alisema kuwa baadhi ya wasomi na viongozi ni miongoni mwa watu wanaotumikisha watoto wadogo hususani wa kike katika kazi za ndani, baa, mama ntilie na kuuza mboga mboga mitaani jambo ambalo ni hatari.
Aidha aliomba wanaume wanaotongoza watoto wadogo wa kike wakiwemo wanafunzi, nao washughulikiwe kwa sababu vitendo hivyo vinawanyanyapaa na kuwaharibia ndoto zao kimaisha, ikiwemo kuwakosesha fursa ya kusoma au kuwaingiza katika ndoa na mimba za utotoni.