NA TUNU NASSOR,-DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Platinum Credit Ltd kwa kushirikiana na Hospitali ya Mwananyamala wanatoa bure huduma za uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake wa Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Lufunyo Gideon, alisema wameamua kufadhili uchunguzi huo, ikiwa ni zawadi ya Sikukuu ya Krismasi na kurudisha kile walichokipata kwa jamii.
Alisema uchunguzi huo umeanza kufanyika katika Hospitali ya Mwananyamala, iliyopo Kinondoni, kuanzia Desemba 16, mwaka huu.
“Tunawaomba wanawake wajitokeze kwa wingi katika kufanyiwa uchunguzi ili waweze kutambua afya zao mapema na kupata ushauri,” alisema Gideon.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Daniel Nkungu, alisema ni fursa kwa wanawake kujua afya zao ili kama wana dalili za awali za ugonjwa huo wapate matibabu mapema.
“Tatizo lililopo kwa sasa ni watu kuchelewa kugundua dalili za awali za ugonjwa huo, hivyo kugundulika ukiwa katika hatua mbaya ambayo mara kadhaa umesababisha vifo,” alisema Dk. Nkungu.
Alisema wahudumu wa hospitali hiyo wamejipanga vizuri kuendesha uchunguzi huo.
“Niwaombe wanawake wajitokeze kwa wingi kupima kwa kuwa tumejipanga vizuri katika kuwapokea na kuwafanyia uchunguzi kwa haraka,” alisema Dk. Nkungu.