Janeth Mushi -Arusha
MWANAFUNZI wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Arusha Meru, Faisal Salim (19), anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi katika paji la uso kwa madai ya kuwa na msongo wa mawazo uliotokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana alidai tukio hilo lilitokea jana saa 11 alfajiri katika nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), iliyopo Plot namba 3 na 4, eneo la Soko Kuu, Kata ya Kati.
Kamanda Shana alidai siku ya tukio, mwanafunzi huyo alijifyatulia risasi moja katika paji la uso akiwa chumbani kwake.
Alidai kuwa mwanafunzi huyo alijiua kwa kutumia bunduki aina ya Rifle Winchester, inayomilikiwa na baba yake, Salim Ibrahim (56) aliyekuwa akiishi naye.
“Chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliotokana na matumizi ya dawa za kulevya, na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru kwa uchunguzi zaidi wa daktari.
“Natoa wito kwa taasisi, kampuni na watu binafsi wanaomiliki silaha kuzitumia kwa umakini mkubwa na kuzitunza sehemu sahihi ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza endapo zitachukuliwa au kuibiwa na kutumika vibaya.
“Tutawachunguza wote watakaotumia silaha hizo kinyume na utaratibu uliowekwa na ambao watabainika kushindwa kuzitunza hatua zitachukuliwa,” alisema.