WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KIJANA Alex Suke (17), anayedaiwa kupigwa risasi na polisi ameeleza jinsi shambulio hilo lilivyozima ndoto yake ya kurudia mtihani wa kidato cha nne, mwaka huu.
Alex amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke, wodi namba saba akitibiwa majeraha aliyoyapata kifuani na kwenye mkono wa kulia baada ya polisi waliokuwa wakituliza ghasia katika eneo la Buguruni Relini kumpiga risasi mkononi na begani.
Katika mahojiano na MTANZANIA yaliyofanyika jana hospitalini hapo, Alex alisema risasi hiyo iliyompiga kifuani na kwenye mkono wa kulia na kuuvunja.
Kwamba imerudisha nyuma azma yake ya kurudia mtihani wa kumaliza kidato cha nne kwa sababu mkono uliovunjika ndiyo anautumia katika kuandika.
“Risasi hiyo ilinipiga kifuani na kuuvunja mkono wangu wa kulia ambao ndio nautegemea katika mambo mengi ikiwamo kuandikia,” alisema Alex.
Akisimulia tukio hilo, Alex alisema anakumbuka Machi 9, mwaka huu akiwa Buguruni Relini akimsaidia babu yake kuuza mbao ndiko alikopatwa na mkasa huo.
“Ilikuwa kama saa sita, waendesha bodaboda walikuwa wakikimbizana na dereva wa gari aina ya Carina lililodaiwa kugonga wanafunzi huko lilikotoka.
“Walipofika eneo tulilokuwa walikuta kuna mkokoteni umeegeshwa barabarani hivyo ukazuia lile gari, dereva wakamkamata.
“Polisi wa usalama barabarani walikuja na kumchukua dereva huyo lakini kukawa na mabishano kati ya waendesha bodaboda kuwa kwa nini alichukuliwa bila kupigwa.
“Ikabidi askari wawapigie simu polisi wengine kuja kutuliza ghasia ndipo walipofika na kuanza kuwatuliza bodaboda,” alisema Alex.
Aliseama akiwa umbali wa hatua 30 kutoka eneo la tukio alisikia milio ya risasi.
“Nilishangaa ghafla natoka damu huku natetemeka mwili mzima kisha nikaanguka chini, baada ya dakika kama tano nilihisi maumivu makali sana.
“Waliokuwapo hapo walinisaidia kuniingiza katika gari la babu yangu na kunileta hapa hospitali,” alisema Alex.
Mama mzazi wa Alex, Agatha Mwangambi naye amefanya mahojiano na MTANZANIA na kuiomba Serikali imsaidie kugharamia matibabu ya mwanaye.
Alisema matibabu ya majeraha aliyoyapata mwanaye yanatumia gharama kubwa hivyo ndugu wanalazimika kuchangishana .
“Hapa unavyoniona natoka kununua dawa kwa ajili ya upasuaji ambao anaenda kufanyiwa muda si mrefu, hivyo naiomba Serikali itusaidie kupata fedha za matibabu,” alisema Agatha.
Alisema Alex anatakiwa kurudia mtihani wa kidato cha nne mwaka huu hivyo anaomba msaada huo ili afya ya mwanawe iimarike haraka aweze kuendelea na masomo.
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula kupitia simu yake ya kiganjani alisema yuko kwenye kikao na kuahidi kupiga simu baadaye kulizungumzia, lakini hadi tunakwenda mtamboni hakupiga.