21.4 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu mbaroni akidaiwa kumtia mimba mwanafunzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa

NA ABDALLAH AMIRI, IGUNGA

MWALIMU wa Shule ya Msingi Simbo wilayani Igunga,   Edward Kashuma, anashikiliwa na polisi   kwa tuhuma za kumtia mimba mwanafunzi.

Mwanafunzi huyo ana umri wa miaka 15 na yuko kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Simbo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa, alithibitisha kukamatwa kwa mwalimu huyo akisema upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Babu wa mwanafunzi huyo, Luteni Kanali mstaafu, Thadeo Mgoso, aliiambia MTANZANIA jana  kwamba aligundua mjukuu wake huyo kuwa na mimba baada ya kumuona haendi shuleni.

“Mimi naishi Dar es Salaam na nilikuja hapa Tabora kuhani msiba. Nilipofika hapa na kukaa siku kadhaa, nilishangaa mjukuu wangu haendi shule. Nilipomuuliza hakunijibu lakini nilipomuuliza dada yake aliniambia amefukuzwa shule kwa sababu ya ujauzito.

“Baada ya majibu hayo niliamua kwenda shuleni  kuonana na mkuu wa shule ambaye alinithibitishia mjukuu wangu ni mjamzito.

“Kwa hiyo  tulipombana huyo mjukuu wangu alikiri kuwa na ujauzito aliopewa na Mwalimu Kashuna.

“Kwa hiyo  nilikwenda kituo kidogo cha polisi kutoa taarifa   mwalimu aweze kukamatwa, lakini haikuwezekana. Baadaye, yule mkuu wa kituo cha polisi alinishawishi tumalize masuala hayo kienyeji kwa kile alichosema kama yatafikishwa katika mkondo wa sheria  mtuhumiwa atafukuzwa kazi,” alisema Luteni Kanali Mgoso.

Pamoja na kukataa suala la kumalizana kienyeji, Luteni Kanali Mgoso  alisema baadaye mwalimu huyo alimfuata nyumbani kwake   kutaka suala hilo lisifikishwe katika vyombo vya sheria.

“Alinifuata nyumbani na kukiri kumpa mimba mjukuu wangu lakini alitaka tuyamalize kinyemela.

“Mimi nilikataa, nikapiga simu polisi na walifika askari wawili waliomtia mbaroni  kwa ajili ya hatua zaidi za sheria,” alisema.

Naye Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Simbo, Felician Musiba, alikiri Mwalimu Kashuma kukamatwa na kuwataka walimu waache tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles