31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Harufu ya sumu kwa meya yazua taharuki

James Bwire
James Bwire

Na Peter Fabian, Mwanza

KIKAO cha Kamati ya Fedha na Uongozi cha Halmashauri ya Jiji la Mwanza jana kilivunjika baada Meya wa Jiji, James Bwire,  kurudi ofisini kwake na kukuta hewa nzito yenye harufu kali inayodhaniwa kuwa sumu.

Kutokana nataharuki hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watumishi wawili wa ofisi ya Meya akiwamo Katibu Muhutasi wake, Gladys Chiduo na mhudumu wa ofisi hiyo,  Selestine Mtobesha.

Tukio hilo    ambalo limekuwa gumzo katika Jiji la Mwanza, lilithibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa jiji hilo, Adamu Mgoyi.

Alisema wakiwa wametoka  katika ziara ya kukagua maeneo ya wafanyabishara ndogondogo katika eneo la Sinai na Community Centre walirejea ofisini  ambako Meya Bwire  aliingia ofisini kwake na kutana na hali hiyo.

“Baada ya kuingia ofisini kwake  alikuta hali hiyo… alituita mimi (Mgoyi), mbunge  (Stanslaus Mabula), Naibu Meya Bikhu Kotecha  a na Diwani wa Kata ya Mhandu,  Lucas Wambura (CCM), tulikuta hewa nzito na kali.

“…kutokana na hali hiyo baada ya kushauriana na wenzangu, nililazimika kuwasiliana na polisi  na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa jambo hilo,” alisema Mgoyi.

Alisema pamoja na kuwapo   harufu hiyo nzito pia kulikuwa na vitu vinavyofanana na unga  ambao ulizua taharuki na kuonakana  huenda ndiyo ulichangia kuwapo   harufu hiyo kali waliyodai huenda ilikuwa  ni sumu.

“Kwa kuwa jambo hilo lipo kwa vyombo vya dola kwa uchunguzi, kwa sasa nadhani tusubiri watatueleza nini kilisababisha hali hiyo na hicho kitu kama unga ni nini, niwaombe tuvute subira,” alisema.

MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi   kupata ufafanuzi wa tukio hilo ambako   wasaidizi wake walisema alikuwa katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama tangu asubuhi.

Akisimulia tukio hilo, Meya Bwire alisema tukio hilo lilitokea jana saa 8:30 mchana baada ya kuingia ndani ya ofisi yake na kukuta hali ambayo ilimshtua na kuamua kuwaita viongozi wengine kushuhudia.

Alisema awali alifika ofisini hapo saa 4:00 asubuhi na alikutana na wajumbe wa Kamati ya Fedha na uongozi na kukubaliana kuanza   ziara ya kutembelea maeneo ya majengo Comminity Centre na Sinai na waliporudi mchana   alipoikuta hali hiyo.

“Niliporudi kutoka ziara niliomba wenzangu kwenda ofsini kwangu   kujisaidia haja ndogo lakini nilipoingia ndani ya ofisi hiyo nilihisi kuwapo hewa nzito ikiambatana na harufu kali utadhani kumepuliziwa dawa ya kuua wadudu.

“Nilianza kuhisi kifua kujaa hivyo nililazimika kutoka haraka na kuwaarifu wajumbe wenzangu,”alisema.

Machi 6, mwaka huu, Meya Bwire, aliugua ghafla muda mfupi baada ya kutoka katika ofisi hiyo na kuzidiwa huku ikiaminika kuwa aliugua ugonjwa wa shinikizo la damu na kukimbizwa katika hospitali binafsi ya Uhuru jijini Mwanza. Baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibubu na vipimo.

Akiwa Bugando familia yake ilikubaliana kumpeleka Nairobi   Kenya Machi 7, mwaka huu kwa matibabu zaidi na uchunguzi wa kina ambako inadaiwa   ilibainika kuwa alikuwa amevuta kiwango kikubwa cha sumu.  Alitibiwa na kurejea nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles