Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
MWALIMU wa Shule ya Sekondari Charlotte katika Manispaa ya Morogoro, Heriman Manase anadaiwa kuachishwa kazi akituhumiwa kujihusisha na masuala ya siasa kwa kumshabikia aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vilipo kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Inadaiwa kwamba mwalimu huyo alikuwa akimpigia debe Lowassa, ndani na nje ya shule hiyo.
Mwalimu huyo pia anadaiwa kuhudhuria mkutano wa Lowassa jijini Arusha siku mwanasiasa huyo alipotangaza nia ya kugombea urais wakati huo akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
MTANZANIA lilizungumza na mwalimu huyo ambaye alisema uongozi wa shule umemweleza kuwa mkataba wake hautaongezwa utakapomalizika Januari mwakani.
Mwalimu huyo alidai kuwa uongozi wa shule ambayo ni ya binafsi, ulimweleza kuwa hataongezewa mkataba kwa vile masomo ya mchepuo wa biashara anayofundisha yamefutwa.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, Mwalimu Mkuu  wa shule hiyo aliyemtaja kwa jina la Sr Dorothea Lazaro alimwita ofisini kwake na kumwambia kuwa bodi ya shule imekubaliana kufuta mkataba wake.
Manase alisema mwalimu mkuu alimweleza kuwa  shule ilikuwa tayari kumlipa haki zake zote na ndiyo maana hadi sasa anaendelea na kazi shuleni hapo akisubiri Januari mwakani mkataba utakapomalizika.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Zakaria John alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa suala hilo liko polisi, ingawa alisisitiza kuwa  anachojua yeye ni kwamba Manase bado  ni mwalimu halali wa shule hiyo.
Mwalimu  Manase alithibitisha kuwa amekwisha kuitwa polisi ambao walitaka  kujua chanzo cha barua hiyo kusambaa katika mitandao ya jamii.