27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwakyembe: Waziri mkuu hateuliwi kwa mtandao

Dr-Harrison-MwakyembeNa Mwandishi Wetu, DODOMA

MBUNGE mteule wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM) amesema waziri mkuu wa Serikali ya awamu ya tano atatokana na uteuzi  wa Rais Dk. John Magufuli na kuinidhishwa na Bunge na wala si taarifa zinazozagaa katika mitandao ya kijamii.

Dk. Mwakyembe ambaye, alikuwa Waziri wa Afrika Mashariki katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ameyasema hayo mjini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, waliotaka kujua namna alivyopokea taarifa za jina lake kutajwa na wananchi kwa nafasi ya waziri mkuu.

Alisema kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi,  waziri mkuu anateuliwa na rais ambaye huwasilisha jina hilo kwa Spika wa Bunge na baadaye kupigiwa kura na wabunge.

“Mimi siwezi kuwasemea wananchi na siwezi  kusema kuna watu wengi wanasema hivi,  kwani nafasi ya uwaziri mkuu haiji kwa njia ya kura ya maoni, wala kwa  njia ya mitandao ya kijamii ni nafasi ya uteuzi inayoidhinishwa na Bunge na ni mamlaka ya rais wa nchi,” alisema Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe,  aliwataka Watanzania bila kujali itikadi za dini na vyama vyao wamuombee Rais Magufuli, ili aweze kuteua viongozi watakaowajibika na ambao wataendana na kasi yake.

Wabunge kadhaa wamekuwa wakitajwa katika nafasi hiyo ya juu serikalini na kupewa nafasi huenda mmoja wao akawa waziri mkuu katika Serikali hii ya awamu ya tano.

Wengine wanaotajwa ni Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo na Mbunge wa Bumbuli January Makamba.

Wakati mjadala ukiwa hivyo, jina la Kachero namba moja mstaafu wa Jeshi la Polisi, Adadi Rajabu, nalo limechipuka kuwa ni miongoni mwa majina ya wanasiasa machachari yanayopewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Kachero Rajabu ambaye alistaafu utumishi katika Jeshi la Polisi akiwa na cheo cha Kamishna na baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, aligombea ubunge wa Muheza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda na hivi sasa anatajwa kuwamo kwenye orodha ya watu ambao Rais John Magufuli anapendezwa na utendaji kazi wake wa kujituma.

Adadi ameingia katika orodha ya wanasiasa wanaofikiriwa kuteuliwa kushika wadhfa huo ambao kiuhalisia ni watendaji zaidi zikiwa zimesalia siku nne kabla Rais Magufuli hajawasilisha jina la waziri mkuu mteule bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa na Bunge..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles