24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MVIWATA watakiwa kutatua changamotoza wakulima

Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ameagiza uongozi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora na mikopo kwa wanachama wake husasan walioko vijijini kwa kushirikiana na wizara.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa MVIWATA Mkoa wa Dodoma leo Desemba 8, Kusaya amesema hafurahishwi kusikia malalamiko ya wakulima wadogo kukosa mbolea na mbegu bora au kusikia wakiuziwa kwa bei ghali wakati umoja waoupo.

“MVIWATA tumieni umoja wenu kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja kupitia Wakala wa mbolea (TFRA) ambapo mtanunua kwa bei nafuu na kusambaza kwa wana chama wenu vijijini. Wizara ipo na itasimamia kwa karibu ili kuleta unafuu kwa wakulima,” amesema Kusaya.

Kusaya ameongeza kuwa, mtandao huo una jukumu pia la kutafuta mbegu bora za gharama nafuu za mazao ya mahindi, alizeti, mpunga na mengine kwa kuwasilisha mahitaji yao kwenye Wakala wa Mbegu wa serikali (ASA).

Aidha wakulima hao katika risala iliyosomwa na mwenyekiti wa mtandao huo mkoa wa Dodoma, Said Matonya waliiomba serikali kupitia wizara ya kilimo kusaidia upatikanaji wa mbegu za mazao ya chakula na biashara mapema kabla ya msimu kuisha na mbegu hizo ziuzwe kwa gharama nafuu.

Matonya ametaja mbegu za mahindi mfuko wa kilo mbili zinauzwa vijijini kwa gharama ya kati ya Shilingi 10,000 hadi 12,000 hatua ambayo inakwamisha wakulima wadogo kununua hivyo kujikuta wakipanda mbegu za asili na zisizo na ubora.

“Wakulima tunakabiliwa na ukosefu wa pembejeo, mbegu bora, mafunzo na mikopo kutokana na kuwa za gharama kubwa, hivyo serikali itusaidie tupate huduma hizi kwa gharama nafuu” alisema Matonya .

Akijibu hoja hiyo Kusaya alisema serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli inawathamini wakulima ndio maana hatua mbalimbali ikiwemo Wakala wa Mbegu (ASA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea wameelekezwa kufikisha huduma zao vijijini kwa bei elekezi ya serikali.

“Uwepo wangu hapa leo ni uthibitisho kuwa serikali inawathamini na kuwajali wakulima wadogo nchini. Naagiza tena Wakala wa Mbegu nchini (ASA) ahakikishe mbegu bora za mahindi zinafika Dodoma na mikoa mingine yote na kuuzwa si zaidi ya Sh 6,000 kwa mfuko wa kilo mbili” ameagiza Kusaya.

Katika hatua nyingine Kusaya ametoa wito kwa MVIWATA kutumia uwepo wa vyuo 14 vya mafunzo ya kilimo vya serikali (MATI) na vituo 4 vya mafunzo ya wakulima nchini kupeleka wakulima na wanafunzi (vijana) kujifunza mbinu za kisasa ili wafanye kilimo biashara na cha kisayansi.

Ametaja kituo cha wakulima wadogo Bihawana kilichopo Dodoma kama sehemu muhimu ambapo MVIWATA wanaweza kutumia kufundisha wanachama wake namna ya kuongeza tija na ujuzi wa kuendesha kilimo biashara.

Kusaya amewashauri na kuwasisitiza wakulima kupitia MVIWATA kutumia uwepo wa Mfuko wa Pembejeo (AGITF) unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo kwani utawezesha kupata zana bora za kilimo kama trekta, powertiller, na pembejeo kwa riba nafuu.

“Mfuko wa pembejeo ni maalum kwa ajili ya kukopesha wakulima na riba zake ni nafuu kwani kikundi hukopeshwa kwa riba ya asilimia 6 na mkulima binafsi hukopeshwa kwa asilimia 7 na kufanya marejesho kwa muda wa miezi 72” amesisitiza Kusaya.

Mkutano huo wa mwaka wa wanachama wa Mtandao wa Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoa wa Dodoma umehudhuriwa na wakulima 100 kati ya 800 kutoka wilaya za Dodoma Mjini, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Bahi na Kondoa ambapo pia tafanya uchaguzi mkuu.

Mkutano huo unafanyika ukiwa na kauli mbiu isemayo “MVIWATA Sauti ya Mkulima, Mtetezi wa Mkulima ni Mkulima Mwenyewe”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles