25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Mv Mbeya kukamilika Septemba

ESTHER MBUSSI-KYELA

UJENZI wa Meli ya abiria ya MV Mbeya II, itakayofanya safari zake katika Ziwa Nyasa, unatarajiwa kukamilika Septemba.

Meli hiyo iliyogharimu Sh bilioni 9.1, yenye uwezo wa kupakia mizigo tani 200 na abiria 200 kwa wakati mmoja, pia inatarajiwa kuwaondolea changamoto ya usafiri abiria wanaoishi katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na Ziwa Nyasa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Bandari ya Itungi, wilayani Kyela jana, Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abeid Galus, alisema kukamilika kwa meli hiyo ya abiria itaenda kuondoa adha ya usafiri ziwani kwa sababu kwa sasa hakuna chombo chochote cha kuaminika kinachofanya kazi ziwani.

“Watu wengi wamekuwa wakitumia maboti au mashua, lakini hakuna chombo madhubuti kinachofanya kazi ziwani, kwa hiyo ujio wa meli ya MV Mbeya II unaenda kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.

“Ziwa hili ni hatari kidogo kwani lina mawimbi makubwa, kwa hiyo inaenda kumarisha usalama wa mizigo na abiria wanaokwenda sehemu mbalimbali,” alisema.

Galus alisema ujenzi wa meli hiyo ulianza Julai mwaka juzi chini ya Kampuni ya Songoro Marine na umefikia zaidi ya asilimia 82 kwa hatua ya kufunga mitambo, kuweka vyumba, kufunga viti na umaliziaji.

Akizungumzia meli zilizopo katika ziwa hilo kwa ujumla, alisema hivi sasa lina meli tatu zikiwamo mbili za mizigo na moja ya abiria.

Alizitaja meli hizo za mizigo kuwa ni MV Njombe na MV Ruvuma ambazo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 na tayari zimeshakamilika na zimeanza kufanya kazi tangu Julai mwaka juzi kwa ukanda wa Ziwa Nyasa na MV Mbeya II ya abiria.

“Hadi sasa meli hizo zimeshafanya safari saba zikiwamo nne za majaribio na tatu za kibiashara ambazo inaendelea nazo,” alisema Galus.

Pamoja na mambo mengine, Galus alisema uwepo wa meli hizo mbili za mizigo na matarajio ya kuanza kazi kwa meli ya abiria ya MV Mbeya II, utarahisisha shughuli za usafirishaji katika mwambao wa Ziwa Nyasa na kuboresha uchumi kwa jamii zinazoishi katika miji ya pembezoni mwa ziwa kwa kuongeza wigo na mwingiliano wa kibiashara na kutoa ajira kwa wakazi wa maeneo hayo.

Aidha, alisema mradi mzima wa meli hiyo na miundombinu mingine inayoendelea katika bandari mbalimbali za Ziwa Nyasa, hususani Itungi na Kiwira, itazifanya Ziwa Nyasa kuanza kujitegemea kiuchumi tofauti na sasa ambapo inategemea ruzuku kutoka serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles