MAMLAKA ya Maji Safi na Majitaka na Usafi wa Mazingira mjini Moshi (Muwsa), imetumia zaidi ya Sh milioni 669 kutekeleza miradi mipya ya kusambaza maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Joyce Msiru, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini Moshi.
Alisema kwamba, miradi hiyo imetekelezwa kufuatia kuwapo kwa uhaba mkubwa wa maji katika baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Moshi.
“Fedha hizo zimetumika kufanya upanuzi na kutekeleza miradi mipya ya maji, ikiwa ni pamoja na kutumika katika ujenzi wa mradi wa chemchem ya Kaloleni iitwayo Njoro ya Goha, uliogharimu zaidi ya Sh milioni 397.
“Mradi huo unategemea kuhudumia wananchi zaidi 13,141 katika vitongoji vitano vilivyoko Shabaha na Sanya Line B, Kata ya Mabogini, Wilaya ya Moshi Vijijini,” alisema Msiru.
Kwa mujibu wa Msiru, kazi iliyofanyika katika utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na ujenzi wa ukuta mpya wa chanzo cha maji, ujenzi wa chumba cha kuweka dawa, ulazaji wa bomba la kusafirishia maji na ulazaji wa mabomba ya kusambazia maji yenye urefu wa kilomita 5.25.
“Kutokana na hatua hizo, Muwsa tayari imepokea maombi ya wananchi 501 wanaohitaji kuunganishiwa maji safi na salama ambapo tayari wateja 66 wameshalipia huduma hiyo na 35 wameshaunganishiwa na wameanza kunufaika na huduma hiyo.
“Nao mradi wa chemichemi ya Mkashilingi iliyopo Shiri Njoro, wilayani Hai, uligharimu zaidi ya shilingi milioni 272 na awamu ya kwanza utahudumia wananchi wapatao 15,000,” alisema.