NA TUNU NASSOR , DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imekumbwa na uhaba wa damu hali ambayo imeulazimu uongozi wa hospitali hiyo kuomba msaada wa dharura kwa Serikali na watu binafsi.
Uongozi huo pia umewaomba Watanzania, mashirika ya umma, makampuni na watu binafsi kujitokeza kusaidia kuchangia damu kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopelekwa katika hospitali hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha, ilieleza kuwa kwa siku hospitali hiyo huhitaji wastani wa chupa za damu 70 hadi 100 kwa siku.
Alisema hali hiyo inachangiwa na ongezeko la mahitaji ya damu ambayo hutumika zaidi hasa kwa wagonjwa wa dharura, kina mama wajawazito, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, watoto na wagonjwa wa saratani.
“Kila mgonjwa wa upasuaji wa moyo anahitaji kiasi cha chupa tano mpaka sita za damu. Matumizi haya yanafanyika kabla, wakati na baada ya kufanyiwa upasuaji,” alisema Aligaesha.
Alisema kwa wiki hii wamelazimika kufungua kambi maalumu za Madaktari Bingwa wa Moyo kutoka nchi mbalimbali ambao wanashirikiana na madaktari wa hapa nchini kufanya upasuaji wa moyo, kati ya wagonjwa watano hadi sita kwa siku.
“Wagonjwa wa moyo pekee huitaji chupa 30 hadi 36 kwa siku. Kambi hizi zimeanza mapema Aprili mwaka huu na tunatarajia kuwa nazo katika miezi mitatu ijayo kama njia ya kuwafanya madaktari hawa waendelee kuja na kufanya upasuaji wa moyo kwa ufanisi ambako damu huhitajika zaidi,” alisema Eligaesha.
Alisema hospitali hiyo ya taifa hutegemea kupata damu kutoka vyanzo vikuu viwili ambavyo ni ndani ya hospitali na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS).
“Makusanyo ya damu kutoka vyanzo vya ndani ni kati ya chupa 20 hadi 40 kwa siku huku matumizi yakiwa chupa 70 hadi 100.
“Mathalani kuanzia Aprili 17 mwaka huu hatukuweza kupata damu hata chupa moja kutoka Mpango wa Taifa Damu Salama hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa damu hospitalini hapa ikilinganishwa na mahitaji,” alisema.
Alisema Hospitali ya Taifa Muhimbili imejipanga kupitia kitengo chake cha Uchangiaji Damu kilichopo Maabara Kuu kuwapokea watu watakaojitokeza kuchangia damu.