MGOMBEA Ubunge wa Chadema Mafinga Mjini, William Mungai, amewaomba wananchi kumchagua aweze kuleta mabadiliko ya maendeleo.
Alisema amejitosa kugombea nafasi hiyo kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali kwa kukabaliana na changamoto zilizopo ikiwamo afya, maji, viwanda, miundombinu, elimu na kuimarisha uchumi kupitia taasisi za benki.
Mtoto huyo wa Mungai alisema jimbo hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mapato ya serikali kwa kushika nafasi ya pili mbele ya Temeke hivyo hakuna sababu ya kurudi nyuma katika maendeleo.
Alisema akiwa mbunge atahakikisha anajenga viwanda vidogo na vya kati mazao ya Mafinga yasindikwe tofauti na ilivyo sasa.
“Nitashirikiana na halmashauri yangu kutenga maeneo ya uwekezaji na kuitangaza Wilaya ya Mufundi na jimbo lake la Mafinga kupitia Taasisi za benki ili nazo ziwekeze kwa faida ya wanaMafinga lakini pia Mafinga lazima ijenge viwanda vya mbao vitakavyosaidia kuongeza thamani ya mbao wanazozalisha,”alisema Mungai.
Akizungumzia sekta ya elimu, Mungai alisema yupo tayari kufuata sera ya Chadema ya kufuta michango yote shuleni wanafunzi wake wasome bila ya usumbufu na hivyo kufanya idadi ya wataalamu waongezeke.
Kwa kufanya hivyo baada ya miaka mitano kutakuwa na idadi kubwa ya wananchi wa Mafinga waliopata elimu, alisema.
Alisema atahakikisha changamoto za elimu zilizopo Mafinga kama vile ukosefu wa madawati, nyumba za walimu na kuboresha maslahi yao anazifanya kwa kiwango kikubwa kuwapa molari walimu kufundisha kwa bidii.
Alisema hakuna jambo litakaloshindikana katika uongozi wake.
Hata hivyo, alisema ili kukabiliana na changamoto hizo ni lazima wananchi wa Mafinga wajitokeze kwa ukamilifu kumchagua katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu aweze kuleta mabadiliko.
Aliwataka waache kusikiliza propaganda za wapinzani wanaotaka kuchukua madaraka kwa mabavu.