25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MTI WA AJABU WAUA WATANO WA FAMILIA MOJA

Nyumba iliyoangukiwa na mti katika Kijiji cha Ng’eresi

 

 

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

MAJONZI tena Arusha. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mti mkubwa kuserereka umbali wa takribani mita 200 ukiwa umesimama kabla ya kuiangukia nyumba walimokuwa wamelala ndugu watano wa familia moja na kuwaua wote.

Tukio hilo limewakumbusha watu wa mkoa huo  machungu ya kupoteza wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wa gari la Shule ya Lucky Vincent ya mjini hapa waliokufa kwa ajali ya gari wiki iliyopita baada ya basi lao kuacha njia na kutumbukia korongoni  wilayani Karatu.

Ikiwa ni siku moja tu miili hiyo iagwe Uwanja wa Sheikh Amri Abedi mjini hapa, ghafla watu watano wa familia ya Jonathan Kalamwia (55) mkazi wa Kijiji cha Ng’ires, Kata ya Sokoni II wilayani Arumeru walifariki dunia kwa   kuangukiwa na mti mkubwa wakiwa wamelala usiku.

Ajali hiyo iliyoacha simanzi na maswali mengi kwa wananchi wa Kijiji cha Ng’ires na maeneo jirani, ilitokea saa 7.00 usiku wa kuamkia jana   wakati mvua ikiendelea kunyesha.

Kwa takriban wiki ya tatu sasa mvua nyingi  imeendelea kunyesha mkoani hapa   yakiwamo maeneo ya milima na miinuko ya Mlima Meru ambako kipo Kijiji cha Ng’ires.

  Vyanzo vya habari kutoka eneo la tukio vilisema  iliwachukua zaidi ya saa 5.00 waokoaji kuitoa miili iliyokuwa imefunikwa na udongo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema mti huo pamoja na miti mingine, ni wa asili na wa siku nyingi na ulikuwa umeota kwenye  Mlima Lakemana.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo,  alisema wakati tukio hilo linatokea, Mzee Kalambwia ambaye ni  mlinzi katika Hospitali ya Dk. Mohamed, alikuwa kazini. 

“Juzi Mei 9, mwaka huu usiku wakati mvua ikiendelea kunyesha katika Kijiji cha Ng’eresi Kata ya Sokoni II, mti mkubwa uliserereka na kifusi cha udongo na  kufunika nyumba ya Kalambwia,” alisema Kamanda Mkumbo na kuongeza:

“Ndani ya nyumba walikuwa wamelala watoto wake watano ambao ni Gilead Jonathan (31), Lazaro Namnyaki (26), Best Jonathan (20), Miriama Jonathani (16) mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule Sekondari Enaboishu   na Gloria Jonathani (11) mwanafunzi darasa la tatu  wa Shule ya Msingi Ng’iresi.

“Haya ni majonzi makubwa, huyu bwana kupotolewa na watoto wake wote. Mvua ni baraka lakini kwa tukio hili limekuwa ni tatizo kubwa.

Nyumba iliyokumbwa na ajali ipo kwenye bonde kwa hiyo mti ulitelemka ukiwa umesimama na   kuiangukia nyumba wakati familia ikiwa imelala.

“Niwaombe wananchi kuchukua tahadhari mvua inayoendelea kunyesha ni wiki ya tatu inanyesha mfululizo. Ni vema kila familia ichukue tahadhari ikiona nyumba imelegalega ni muhimu waiimarishe, ikiwamo kupunguza miti inayoonekana ni hatari”.  

  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Wilson Mahera aliyekuwa kwenye eneo la tukio hilo akishirikiana na wananchi, aliliambia MTANZANIA kuwa mti huo ulisafisha kila kilichokuwa mbele yake, ulipokuwa ukiserereka.

“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha sana, ule mti umeng’oa kila kitu na kutengeneza njia yenye upana kama wa mita 15 na ulisafisha kila ulichokikuta njiani, tena ukiwa wima.

“Ulipofika kwenye nyumba walimolala ndugu uliiangukia nyumba …miili ya wanawake wawili imeharibika kutokana na kuangukiwa na mti huku wanaume wawili wakiangukiwa na kuta na kukosa hewa akiwamo mmoja,” alisema Mahera.

Alisema kutokana na tukio hilo kutokea usiku huku mvua ikiwa inaendelea kunyesha,   jeshi la polisi wakishirikiana na wananchi walifanikiwa kutoa miili mitatu saa 11 afajiri huku miili mingine miwili ikitolea saa 2 asubuhi.

“Kule milimani kuna miti mikubwa ya asili na kwa sasa katika eneo lile imebakia mingine mitatu na wananchi wameomba kibali cha kuikata isije kuleta maafa mengine kipindi hiki cha mvua nyingi.

“Lakini pia  Serikali tumewaomba wananchi wote hasa waliojenga chini ya milima kuwa kuwa makini zaidi.  

“Kutokana na tatizo hili sisi halmashauri tutapeleka wataalamu wa washauri wananchi namna ya kujenga nyumba zao hasa waliopo kwenye miinuko ya milima,” alisema Mahera.

KAYA 80 ZAKOSA MAKAZI TANGA

Zaidi ya kaya 80 nyumba zao zimezingirwa na maji huku nyingine zikihifadhiwa katika shule kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kwa saa 24 jijini Tanga.

Madhara zaidi yamezikumba kata za Magaoni, Mzizima, Masiwani, Msambweni na Mzingani.

Wakazi wa maeneo hayo wamelazimika kuhama nyumba zao na kujihifadhi shuleni na wengine wakijihifadhi kwa ndugu zao.

MTANZANIA lilishuhudia kata za Magaoni  na Tangasisi ambazo   awali zilikuwa maarufu kwa uchimbaji wa mchanga,  zikiwa zimeathiriwa  kwa kiasi kikubwana mafuriko wakati wa mvua.

Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Mohamed Haniu (CUF),  alisema mvua hiyo imesababisha  athari zaidi kwenye   madaraja ambayo mengi yamesombwa na maji.

Mwenyekiti  wa Magaoni B, Pendeza Hashim alisema  athari imezidi kutokana na mifereji kuzidiwa na maji ya mvua.

Alisema   licha ya kuwapo   miundombinu hiyo, l imeshindwa kusukuma maji ikizingatiwa  maji hayo yalikuwa mengi kushinda uwezo wa miundombinu hiyo.

“Katika eneo langu tayari kaya 20 tumeweza kuzihifadhi katika shule ya msingi Magaoni baada ya nyumba zao kujaa  maji.

“Baadhi ya wananchi waliiomba serikali kuharakisha msaada wa kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo,” alisema.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo,  Zainabu Ramadhani alisema   hawakuweza kuokoa chakula

wala nguo vyote vimekwenda na maji.

  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magaoni, Arafa Kibaya alisema wamelazimika kusimamisha masomo jana kwa kuwa shule hiyo ilizingirwa na maji.

UMEME, MAJI HAKUNA

Wakati huohuo, wakazi wa Jiji la Tanga walikosa huduma ya umeme na maji kwa zaidi ya saa nane kwa sababu ya mvua hiyo.

Ofisa Habari wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira, Dora Kilo,  alisema    huduma ya maji imekosekana  kutoka na kukosa umeme.

MAJI YAFUNIKA BARABARA

Kutokana na mvua hiyo, jana barabara na madaraja katika maeneo ya Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani yalifunikwa na maji ambayo yalikuwa yakikatisha kwa kasi na kufanya usafiri kusimama kwa muda.

Mbali na eneo pia mvua ilisimamisha shughuli kwa muda katika eneo la Mombo wilayani Korogwe, ambako barabara ilifunikwa na  maji huku baadhi ya magari yakisombwa.

PEMBA HALI TETE

Kutokana na mvua   inayoendelea katika ukanda wa Pwani, hali katika Visiwa vya Zanzibar imezidi kuwa tete baada ya mvua ya   kuangusha miti, madaraja na nyumba kisiwani Pemba jana.

Hali hiyo inaelezwa kuwa ilisimamisha shughuli za uvuvi ambayo ndiyo kazi kubwa ya wananchi, baada ya bahari  kuchafuka  hali ambayo  ilisababisha  kitoweo hicho  kuwa adimu.

Nyongeza ya habari Amina Omari (Tanga) na Gustaf Haule (Pwani)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles