23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mtanziko kanisani kwa Mzee wa Upako

Anthony Lusekelo
Anthony Lusekelo

Na FARAJA MASINDE – Dar es Salaam

BAADHI ya waumini wanaosali katika Kanisa la Maombezi (GRC) la Mchungaji Kiongozi, Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako, wamekumbwa na hali ya mtanziko baada ya kiongozi huyu kutuhumiwa kufanya fujo na kutukana majirani zake waliosema aliziba njia kwa kupaki gari lake.

Waumini hao wamekumbwa na hali hiyo baada ya kuwapo kwa sintofahamu miongoni mwao tangu Mzee wa Upako kukumbwa na tuhuma hizo, huku Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likimchunguza na kama likipata ushahidi lilisema litamfikisha mahakamani.

Juzi jioni, MTANZANIA Jumapili lilifika katika kanisa hilo lililopo eneo la Ubungo Kibangu, Dar es Salaam wakati wa ibada ya Ijumaa iliyokuwa ya kwanza kwa Mzee wa Upako kuiongoza tangu akamatwe na polisi Alhamisi wiki hii maeneo ya Kawe wilayani Kinondoni akidaiwa kufanya fujo kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa tatu asubuhi alipochukuliwa na polisi wa Kituo cha Kawe, huku akionekana amelewa chakari.

Taarifa za yeye kufanya vurugu zilisambaa katika mitandao ya kijamii huku video aliyerekodiwa eneo la tukio, ilimuonyesha amepaki gari barabarani na inadaiwa alifanya hivyo kwa nia ya kulipiza kisasi kwa majirani zake wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348 aliodai wamekuwa wakimkejeli kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.

Baada ya vurugu hizo, polisi walifika na kumchukua wakampeleka kituoni na kupima kiwango cha ulevi kilichogundulika kufikia 131 kinachoelezwa kuwa ni kikubwa, na ilipofika saa tano asubuhi alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi, ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana kimeshuka hadi kufikia 121.

Katika kile kilichoshuhudiwa na MTANZANIA Jumapili juzi, waumini hao wameonekana kugawanyika huku baadhi yao wakiwa wanajadiliana kwa kukaa kwa makundi baada ya ibada hiyo iliyoanza saa 11 jioni na kumalizika saa moja na nusu jioni, huku wengine walikuwa hawajui kilichomtokea kiongozi wao.

“Hivi kuna kitu gani kimetokea maana tunasikia tu kwenye vyombo vya habari kuwa Mzee wa Upako amefanya vituko,” alihoji mmoja wa waumini hao.

Baada ya kuhoji hivyo, ndipo iliwalazimu miongoni mwa waumini waliokuwa katika kundi hilo kuwatoa hofu wenzao kwa kuwaambia kuwa kilichokuwa kinaendelea dhidi ya Mzee wa Upako hakihusiani na uwapo wao kanisani hapo.

“Ni kweli kwamba kuna taarifa zimetoka katika vyombo mbalimbali vya habari, lakini sidhani kama tuna haja ya kuumiza vichwa na kujadili jambo hili.

“Kwa sababu kufanya au kutokufanya hakuwezi kubadilisha imani zetu, hivyo kikubwa ni wewe kama muumini kuhakikisha kuwa unaishikilia imani yako na si kumfuata mtu mwingine.

“Kwa sababu ni imani yako ndiyo itakayokuponya na si mtu kama wengi tunavyodhani, hivyo kusema sijui uache kuabudi kwa kigezo cha tukio hili ni sawa na kuikana imani yako,” alisema mmoja wa waumini hao.

Mbali na majadiliano hayo, pia wapo wengine wanaoabudu kanisani hapo ambao walisikika wakisema kuwa hiyo imekuwa ni kawaida tu kwa kiongozi wao huyo kuchafuliwa, lakini hakuna ukweli wowote.

“Kwani hii ni mara ya kwanza? Mbona wamekuwa wakimchafua vibaya tu kuwa mara kalewa, sijui katukana, lakini unakuta ni uongo tu na hayana ukweli wowote.

“Hivyo kama mtu anasali asali tu, lakini sio kusema eti aache au abadili dhehebu kwa sababu zisizo za msingi, Mzee wa Upako ni kitu kimoja na imani yako ni kitu kingine, hivyo cha msingi ni kushikilia imani yako,” alisema mmoja wa waumini hao.

Akihubiri katika ibada hiyo juzi jioni, Mzee wa Upako alisisitiza suala la imani.

“Nawasihi zishikeni sana imani zenu, mtangulizeni Mungu katika maisha yenu na kwenye kila mnachokifanya.

“Hata unapokuwa unatoka hapa kanisani nakusihi mtangulize Mungu, usikubali imani yako irudi nyuma wala watu kukurudisha nyuma,” alisema Mzee wa Upako wakati akielekea kufunga maombezi hayo ambayo kwa mujibu wa watu wa karibu wa kanisa hilo, kwa juzi hayakuwa na idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na siku za nyuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles