21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makachero polisi wafanya kazi miezi 30 bila mshahara

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi

Na Mwandishi Wetu – Mwanza

SIKU chache baada ya kachero wa Jeshi la Polisi kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Manga Msalaba kufukuzwa, imebainika alikuwa akifanya kazi bila ya kulipwa mshahara kwa kipindi cha miezi 30 mfululizo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi hilo, mbali na Msalaba, pia wapo makachero wengine sita wanaoendelea na kazi, ambao nao hawajalipwa mshahara kwa kipindi hicho, hali inayowalazimu kuishi katika mazingira magumu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amethibitisha kuwapo kwa madai hayo, lakini aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa jana alikuwa nje ya ofisi na kuomba atafutwe Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustino Senga kwa taarifa zaidi.

Akizungumzia suala hilo, Senga alisema kitendo cha Msalaba na makachero wengine kutolipwa mshahara pamoja na stahiki nyingine, kulitokana na matatizo ya utendaji ndani ya jeshi hilo.

Akifafanua zaidi, Senga alisema kusitishwa kwa mishahara hiyo kulitokana na matatizo ya kiofisi yaliyohusu utendaji, yaliyojitokeza ndani ya jeshi hilo kipindi cha nyuma na tayari yalikuwa yakishughulikiwa na ofisi ya jeshi hilo makao makuu Dar es Salaam.

Taarifa zaidi kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kuwa Msalaba alitimuliwa kazi mwezi huu kwa madai ya kujipatia fedha kiasi cha Sh 500,000 kwa njia ya udanganyifu, huku yeye akidai kuwa aliundiwa mashtaka hayo kama sehemu ya kutimuliwa kutokana na kubaini kuwa mshahara wake ulikuwa ukiendelea kutoka na kuliwa na baadhi ya vigogo wa polisi.

Kwamba Msalaba aliamua kufuatilia malipo yake na wengine kwa kutoa barua ya taarifa ya kusudio lake la kufungua kesi mahakamani dhidi ya jeshi hilo kwa kitendo cha kumsitishia mshahara wake pasipo sababu za msingi.

“Kilichomponza Msalaba ni kufuatilia na kuandika waraka wa kueleza kuwa atashtaki, hii ndiyo ilisababisha kuandaliwa makosa na kutimuliwa kazi. Ndani ya Jeshi la Polisi kuna mambo mengi na uonevu mkubwa, lakini hatuwezi kusema kwa sababu tunapaswa kuonyesha utii kwa wakubwa hata wakikosea,” alisema mmoja wa askari ambaye pia ana tatizo la kutolipwa mshahara.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotangazwa na Kamanda Msangi, ilielezwa kuwa Msalaba na kachero Bernard Faru walifukuzwa kazi Oktoba 28, mwaka huu kwa kosa la kujipatia Sh 500,000 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wananchi.

Katika taarifa yake, Msangi, alisema makachero hao walienda Magu mkoani Mwanza na kuwakamata wananchi ambao idadi yao haijajulikana, wakidanganya wanatoka Simiyu, kisha wakawapeleka Kituo Kidogo cha Polisi Kisesa wilayani Magu na kuwaweka mahabusu baada ya kumuomba mkuu wa kituo hicho ili kesho yake waje kuwachukua na kuwapeleka Kituo cha Polisi Nyamagana.

Pia alisema makachero hao waliwalazimisha wafanyabiashara hao kutoa fedha na kuchukua mabati 20 waliyonunua wakidai ni ya wizi.

Alisema wafanyabiashara hao waliamua kupeleka malalamiko ya makachero hao ofisini kwake na waliwatambua katika gwaride la utambulisho.

Hata hivyo, Msalaba aliyapinga madai hayo na kusema anatambua yaliandaliwa kwa nia ya kumwondoa kazini kutokana na msimamo wake, na anao ujumbe mfupi wa maandishi ukitoa maelekezo ya yeye kushughulikiwa ili suala la madai yake lisichafue baadhi ya vigogo wa polisi.

“Nimekuwa kachero kwa muda mrefu, natambua mkakati wa kunitimua kazi umetokana na hatua zangu za kufuatilia madai yangu na kuwasaidia wengine, suala hili linalindwa kwa nguvu kwa kuwa linawahusu vigogo wa polisi,” alisema Msalaba.

Katika hatua nyingine, Senga, alikanusha madai ya Msalaba na kueleza kuwa hakuna uhusiano wa kutimuliwa kwake kazi na suala la madai yake ya mshahara na stahiki zake nyingine.

“Kuna matatizo ya kiofisi yaliyohusu utendaji yalijitokeza ndani ya Jeshi la Polisi kipindi cha nyuma na kusababisha baadhi ya watumishi kusitishiwa mshahara, katika kundi hilo yupo Msalaba na wengine, ila sababu ya askari huyu kufukuzwa kazi haihusiani na hili la mishahara, hivyo asisingizie,” alisema Senga.

Aliendelea kusema kuwa haiwezakani asilipwe stahiki zake anazodai kwa kuwa suala lake linafahamika na alifukuzwa akiwa anadai baada ya kukiuka baadhi ya taratibu za jeshi hilo.

Januari 8, mwaka huu kupitia kwa wakili wake kutoka Kampuni ya Uwakili ya Rwelu, Msalaba aliyekuwa askari mwenye namba F. 5421, aliandika barua yenye kumbukumbu namba Rwelu/Mang/Dem/2015/1 kwa Msangi, kumtaarifu nia yake ya kufungua shauri mahakamani.

Barua hiyo ilieleza kuwa Msalaba alianza kazi mwaka 2003 jijini Mwanza katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa na mwaka 2012 alihamishiwa Wilaya ya Ilemela katika Kituo cha Kirumba.

Mwaka 2013 akiwa katika majukumu yake ya kawaida alisomewa simu ya uhamisho akitakiwa kwenda Kituo Polisi Ukerewe na alifanya taratibu zote ili kuhamia katika wilaya hiyo, lakini katika hali ya sintofahamu, hakulipwa stahili zake kwa wakati hali iliyomlazimu kuendelea kufanya kazi Kirumba akisubiri kulipwa.

Barua hiyo iliongeza kuwa miezi mitatu baadae Msalaba alilipwa Sh 387,500 kama fedha ya kufunga mizigo na aliendelea kusubiri stahili zake ili aweze kuhamia kituo chake kipya cha kazi.

“Kwa mujibu wa maelezo tuliyoyapata toka kwa Msalaba, badala ya kumlipa stahili zake za uhamisho ofisi yako iliandika barua Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na kusababisha kusitisha mshahara wake na stahili nyingine pasipo sababu za msingi tangu Aprili, 2014,” ilieleza barua hiyo.

Pamoja na kusitishwa kwa mshahara wake na stahili nyingine, Msalaba alilazimika kuripoti katika kituo kipya cha kazi wilayani Ukerewe na kupangiwa majukumu mengine, akiahidiwa kuwa atalipwa stahili zote pamoja na mishahara yake yote hali iliyoendelea hadi alipofukuzwa kazi.

Msalaba pia alihamishiwa tena Wilaya ya Magu akitokea Ukerewe pasipokuwa na mshahara, posho wala stahili nyinginezo na kutokana na hali hiyo aliamua kumwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi kutaka kujua hatma ya suala lake, lakini hakupata majibu.

“Kwa mazingira hayo, mteja wetu amekuwa mtumishi wa umma asiye na mshahara wala stahili nyinginezo kuanzia Aprili, 2014 hadi Januari 8, 2016 ikiwa ni zaidi ya miezi 30 pasipo sababu za msingi na kumfanya kushindwa kumudu gharama za maisha na kugeuka kuwa ombaomba,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles