23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mtikisiko wa uchumi wayakumba mabasi ya abiria nchini

img_20150820_113421-002

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM,

ANGUKO la uchumi ambalo limeonekana kuathiri sekta ya fedha kupitia mabenki na majengo, sasa limegeukia usafirishaji ambako tayari mmiliki wa kampuni maarufu ya Muro Investiment Co. Ltd, Maggid Muro, ametangaza kuuza mabasi na vituo vyake vya mafuta.

Uamuzi wa Muro aliyetangaza juzi kuuza mabasi yake 18 pamoja na vituo vyake vya mafuta zaidi ya viwili, umetokana na kile ambacho yeye mwenyewe amekiita hali ya uendeshaji wa biashara kuwa mgumu.

Akizungumza jana kwa njia ya simu na MTANZANIA Jumapili, lililotaka kujua kilicho nyuma ya uamuzi huo baada ya kuona tangazo la uuzaji wa mali hizo, Muro alikiri kuuza mali hizo huku akisisitiza idadi ya abiria imezidi kuporomoka tofauti na siku za nyuma.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, watu wanaosafiri hivi sasa ni wachache na wanafanya hivyo kwa shughuli maalumu ikiwamo vifo vya wazazi.

Muro alisema kutokana na hali hiyo, anatarajia kupunguza wafanyakazi 60 kati ya 110 wanaofanya kazi kwenye kampuni yake.

“Ni kweli tunauza, naondoa magari kama 18 hivi na vituo vya mafuta viwili au vitatu, inategemea na bei nitakayoipata, bei ikiwa nzuri nitauza vituo vitatu.

“Biashara hakuna, biashara imekuwa ngumu sana, yaani hakuna kinachowezekana, sasa unaumia kichwa, unahangaika na vitu vingi, pesa hakuna, sasa tunajaribu kupunguza baadhi ya wafanyakazi pamoja na biashara, napunguza wafanyakazi kama 60,” alisema Muro.

Muro ambaye anamiliki magari zaidi ya 40, alisema kwa ujumla biashara zimekuwa mbaya, kwamba basi la abiria 60 wakati mwingine linasafiri na abiria 20.

“Na basi la kupeleka ruti tatu au nne kwa siku linaondoka halijahi, nafikiri sasa hivi mtu akifiwa na mzazi ndio anasafiri, lakini sijui mama mdogo, wanaambiana nenda tu, wanachangiana,” alisema Muro.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, ‘booking’ (kukata tiketi mapema) nyingi zilikuwa zikifanyika kwa ruti kama Bukoba, Musoma na Mwanza na zilikuwa zinajaa mapema hadi tarehe za mwanzoni mwa mwezi wa 12 kuelekea sikuku za Krismasi na Mwaka Mpya, lakini kwa sasa hakuna.

“Sasa hivi hakuna watu wa ‘booking’, mtu anafanya ya nini wakati gari zinakuja tupu,” alisema.

Muro alisema anatarajia watu watajitokeza kununua magari yake siku za kazi kwa kuwa walitoa tangazo hilo wikiendi.

Kuhusu bei ya magari hayo, alisema inategemeana na aina yake kwa sababu yapo aina ya Zhotong, Yutong, Marcopolo na Higer.

Mwandishi alipomhoji Muro iwapo anayauza magari hayo ili kufidia mkopo benki, alisema yapo magari zaidi ya 10 aliyoyachukua kwa mkopo, lakini mengine ni ya kwake.

“Yapo ambayo ni mkopo, yapo ambayo hayana mkopo ni ya kwangu, yote mchanganyiko. Mfano haya mapya zaidi ya 10 yana mkopo katika benki tofauti tofauti, yapo NBC, Stanbic,” alisema Muro.

Pia alizitaja ruti ambazo amekuwa akifanya huduma ya usafiri kuwa ni pamoja na Mkoa wa Bukoba, Musoma, Mwanza, Mbeya, Tunduma, Arusha na Dodoma.

Kuhusu vituo vya mafuta anavyoviuza ambavyo vyote vinapatikana Mkoa wa Pwani, alisema uendeshaji wake umekuwa mgumu.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustafa Mwalongo, alizungumza na gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) na kusema wapo wanachama wake ambao hali zao zimeyumba, lakini bado chama hicho hakijakutana kujadili hali zao na jinsi ya kuwasaidia.

“Suala hilo liko wazi, tunalijua. Tutakutana kujadili nini cha kufanya ili kuwanusuru wafanyabiashara wenzetu,” alikaririwa Mwalongo na gazeti hilo.

Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la watu kuuza mali zao ikiwamo mahoteli, majengo, viwanja, huku wengine wakilalamika kukosa wateja.

Si hilo tu, hatua ya Serikali kuhamisha fedha zake kutoka katika benki za kibiashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kile ilichosema kuwa mfumo huo ulikuwa ukitumika kufanya ufisadi, imeonekana kuziathiri taasisi hizo za kifedha.

Tayari benki kadhaa zimeonyesha kushindwa kujiongoza na nyingine kupata hasara kutokana na hali ngumu ya uendeshaji.

Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, Kilindi Auction Mart pia ilitangaza kwa niaba ya Benki ya Maendeleo (TIB) kupiga mnada viwanja vilivyowekwa dhamana katika maeneo ya Kunduchi Mtongani, Tegeta na Kyela.

Lakini, athari ni kubwa zaidi kwa benki ya Twiga Bancorp ambayo Oktoba 28 iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu (BoT) baada ya kufikia mtaji hasi wa Sh bilioni 21, ikiwa ni chini ya kiwango cha kisheria, sababu mojawapo ikiwa ni wakopaji kutorejesha fedha.

“Uamuzi huu umechukuliwa baada ya kubaini kuwa benki ya Twiga ina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa Benki ya Twiga kutahatarisha usalama wa amana za wateja,” ilisema sehemu ya taarifa ya Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu.

Pia, BoT iliwaalika watu binafsi na kampuni zenye nia ya kununua hisa katika Benki ya Twiga Bancorp ili kupata mtaji utakaowezesha kutatua tatizo la fedha linalohatarisha amana za wateja na wadai wengine.

Mtikisiko huo pia uliigusa Benki ya CRDB ambayo hivi karibuni ilitangaza hasara ya takribani Sh bilioni 2 katika hesabu zake za robo mwaka.

Taarifa za fedha za benki hiyo zilionyesha kuwa mikopo mingi haijalipwa, lakini pia CRDB walikuwa wana limbikizo kubwa la deni la kodi la muda mrefu.

Mwaka 2015, kwenye taarifa yake ya robo mwaka muda kama huu, CRDB ilipata faida ya Sh bilioni 37.9 baada ya kulipa kodi na tozo nyingine.

Septemba mwaka huu, Hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo, Dar es Salaam ilibadilishwa matumizi na kufanywa hosteli kutokana na sababu kama hizo.

Hoteli nyingine zilizofungwa ni pamoja na JB Belmont iliyopo katika majengo ya Benjamin Mkapa na Golden Jubilee, Kiromo View ya mkoani Pwani  ambayo ilizinduliwa Aprili 11, mwaka 2009 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles