25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mshtakiwa ugaidi aonyesha alivyolawitiwa

Watuhumiwa wa kesi ya ugaidi, akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed (kushoto), wakitoka kwenye chumba cha mahakama baada ya kesi yao kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Picha na Jumanne Juma
Watuhumiwa wa kesi ya ugaidi, akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed (kushoto), wakitoka kwenye chumba cha mahakama baada ya kesi yao kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Picha na Jumanne Juma

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MMOJA wa watuhumiwa wa ugaidi katika kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), amevunja ukimya mahakamani baada ya kuonyesha suruali ilivyolowa kwenye makalio akisema ni madhara ya kulawitiwa na kuingizwa miti na polisi.

Mshtakiwa huyo, Salum Ally Salum, aliamua kufanya hivyo jana ili kuithibitishia mahakama kile walichodai ni unyama waliotendewa na polisi wakati wakihojiwa.

“Mheshimiwa hakimu, angalia (anageuka na kuinua suruali katika eneo la makalio), haya ndiyo madhara niliyopata kwa kuingiliwa nyuma na kuingizwa jiti,” alidai.

Baada ya mshtakiwa huyo kuzungumza, Hakimu Hellen Riwa alimshauri kutoa taarifa kwa uongozi wa Magereza ili aweze kupata matibabu ya haraka kwani akiendelea kukaa hivyo anaweza kupata madhara makubwa.

Kwa upande wake, Sheikh Farid, alimuomba Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya kuchunguza vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa.

Sheikh Farid aliieleza mahakama kuwa Tanzania hakuna ugaidi, na kwamba balaa hilo lisiombwe kutokea hapa nchini.

Alisema kuwa yanayowakuta hivi sasa ni kutokana na kudai mamlaka ya nchi yao kwani kuna mgogoro mkubwa unaoendelea.

Sheikh Farid alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, wakati kesi yake na wenzake 19 ilipokuwa ikitajwa na kuunganishwa na washtakiwa wengine wawili, Sheikh Mselem Ali Mselem na Abdallah Said Ali.

“Mheshimiwa Hakimu, naomba mahakama ikunjue kifua itusikilize tunayotaka kusema, tunataka ufafanuzi kutoka kwako, kwanza nathibitisha kwamba madhila, unyanyasaji, ukatili tulifanyiwa na polisi wakati wa mahojiano.

“Tatizo letu mheshimiwa ni matibabu, gerezani hakuna matibabu, kuna wenzetu tangu tulipoingia humo miezi miwili sasa, wanalala hospitali, dawa hakuna, inafikia hatua tunaagiza kutoka nje.

“Mheshimiwa hali ni mbaya, watu wanatokwa hadi na usaha, yote hayo ni kwa sababu ya ukatili waliotufanyia polisi, tutakapokwenda katika Mahakama Kuu ya Tanganyika iliyovaa koti la Tanzania tutazungumza mengi.

“Tunahitaji iundwe Tume Huru ya Uchunguzi, tunaomba Rais Kikwete aunde tume yenye haki, tume ndiyo itatoa ukweli, hiki ndicho kilio chetu.

“Niliuliza hapa mahakamani Zanzibar ni nchi? Yule rais ni rais wa timu ya mpira?” alihoji Sheikh Farid.

Alidai sheria ya ugaidi ni sheria ya dhuluma ambayo ipo kwa ajili ya kuwanyonga Waislamu na kwamba kuna mgogoro mkubwa wa Utanganyika.

“Tanzania hakuna ugaidi hapa, tusiombe balaa hilo, sisi kosa letu ni kudai mamlaka ya nchi yetu,” alidai.

Hakimu Riwa akijibu hoja ya Sheikh Farid, alisema mahakama imewaruhusu kuandika barua kuomba kuundwa kwa tume huru kisha mahakama itajua pa kuipeleka.

Kabla ya kuwasilisha hoja hizo za malalamiko, washtakiwa walibadilishiwa mashtaka na kusomewa upya mashtaka manne na mawakili wa Serikali, Peter Njike na George Barasa.

Inadaiwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote kwa pamoja kati ya Januari 2013 na Juni 2014 maaeneo mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, walikua njama na kuingiza watu nchini kushiriki vitendo vya kigaidi.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wote wanadaiwa kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi huku wakijua ni kosa.

“Mheshimiwa, shtaka la tatu linamkabili mshtakiwa Farid na Mselem, mnadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mliwaajiri Sadick Absaloum na Farah Omary kushiriki kutenda vitendo vya kigaidi.

“Shtaka la nne linamkabili Farid, unadaiwa kuhifadhi watu waliotenda vitendo vya kigaidi, huku ukijua ni kosa. Ulimuhifadhi Sadick Absaloum na Farah Omary huku ukijua kwamba walitenda ugaidi,” alidai Balasa.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote, upelelezi wa kesi haujakamilika. Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally, Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro, Said Sharifu, Sheikh Mselem Ali Mselem na Abdallah Said Ali.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. hawa waliojiriwa kutenda vitendo hivi vya kigaidi (Sadick Absaloum na Farah Omary) mbona siwaoni kwenye hii list ya washtakiwa? na pia sijawahi kusoma sehemu kuwa walikamatwa na kushtakiwa kisha kufungwa baada ya kukiri kuwa hao wanaoshtakiwa sasa ndio waliowaajiri na kuwaficha?

    hii kesi isije ikawa kama ile ya abdallah zombe ambayo alishinda baada ya kuonekena kua waliotenda maauji hawakuwepo kwenye kushtakiwa kwa hio Zombe aliediwa kutoa amri akashinda kwa kukosa ushahidi.

    muheshimiwa hakimu badala ya kutoa amri kwa magereza wawatibu hao washtakiwa wewe unatoa ushauri watoe tarifa kwa uongozi wa magereza, hivi muheshimiwa hakimu unadhani hao watu wazima wapate madhara kama hayo na mpaka leo wawe hawajatoa taarifa kwa uongozi wa magereza ili wapate matibabu? mbona unatoa ushauri usiokua na faida yoyote? mpaka kufikia kukwambia wewe ina maana walishawasiliana na magereza na hakuna hatua ilichukuliwa sababu hivyo vitendo wamefanyiwa makusudi na tasisi mojawapo ya serekali na hao wote wanabebena maana wote wapo chini ya waziri mmoja.
    wameshasema madawa hakuna na matibabu hawapatiwi ungetoa amri wapelekwe sehemu yenye matibabu.

  2. Kama kweli polisi wanafanya matendo kama haya yaliyotajwa na walalamikaji basi nchi yetu si huru maana matendo kama haya na zaidi walikuwa wanafanyiwa waafrika wakati wa utawala wa kikoloni. Yaani polisi wakati wa ukoloni kilikuwa chombo cha kutenda ukatili. Kama matendo haya yapo ni wazi polisi wananajisi ardhi ya Tanzania na Mungu anaweza kuilaani ardhi hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles