25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi waongeza wakunga vijijini

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

MRADI wa kuongeza wakunga bora vijijini na maeneo yasiyofikika ‘More and Better Midwives’, umesaidia kuongeza idadi ya watoa huduma hao wa afya kwa asilimia 13 katika maeneo ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.

Uwepo wa mradi huo uliofadhiliwa kwa ushirikiano wa mashirika zaidi ya moja kwa kushirikiana na Serikali, umesaidia kuongeza idadi ya wakunga kwa kusomesha wauguzi na wakunga zaidi walioondoa uhaba uliokuwepo, hususani maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

Mradi huo unaomaliza muda wake, ukiwa umezalisha wanafunzi takribani 2,037 waliohitimu mafunzo ya uuguzi na ukunga, ulianza Aprili 2016 na unatarajiwa kumalizika Machi, mwakani.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa mradi wa ukunga salama kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Jhpiego, Dk. Julius Masanika alisema mradi huo ulishirikisha kanda mbili ya Ziwa na Kanda ya Magharibi na kwamba ulihusisha mikoa nane na wilaya 19 katika vituo vya kufundishia 19.

“Wakati mradi huu unaanza kulikuwa na upungufu wa wakunga kwa asilimia 54 waliokosekana eneo hili, lakini kwa sasa upungufu umeshuka mpaka kufikia asilimia 41 na hata katika vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vimepungua,” alisema Dk. Masanika.

Alisema wakati mradi huo unaanza, waliuelekeza maeneo yenye changamoto huku wakizingatia mahali ambako vyuo vya uuguzi na ukunga vinapatikana.

Dk. Masanika alisema lengo la mradi ilikuwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Kanda ya Ziwa na Magharibi ni maeneo ambayo yalikuwa na tatizo la vifo kwa ukubwa, kulikuwa na asilimia ndogo ya kinamama wanaopata huduma kutoka kwa wataalamu wenye mafunzo.

“Tulilenga pia kuongeza idadi ya wakunga, kuimarisha vyuo vya uuguzi na ukunga viweze kutoa wahitimu wenye weledi wa kutosha kwani wakiwa na uwezo watapunguza vifo kwa kiasi kikubwa, pia kuweza kutoa huduma katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi,” alisema Dk. Masanika.

Akielezea wigo wa mradi huo, Dk. Masanika alihakikisha wanawajengea uwezo wakufunzi zaidi ya 168 ambapo kati yao kulikuwa na wanawake 92 na wanaume 72, kuboresha miundombinu katika vyuo na hospitali zilizopo karibu zinazowapatia mafunzo kwa vitendo na kuweka maabara za kufundishia.

“Mbali na maabara hizo, pia tuliweka vyumba vyenye vifaa vya kufundishia ikiwemo midoli ‘mankin’ ambazo ziliwezesha mafunzo kwa vitendo kabla mkunga hajamfikia mama au mtoto ambao ni binadamu,” alisema Dk. Masanika.

Alisema mradi ulikuwa na changamoto kadhaa ikiwemo kutotolewa vyeti kwa wakati kwa wahitimu na hiyo ilisababisha wengi washindwe kuajiriwa.

 “Tumejitahidi kutoa mafunzo bora kwa wahitimu hawa wanaojkwenda kutoa huduma ya mama na mtoto lakini wanaoajiriwa pia ni wachache kwa kuwa ajira zinachelewa hasa kwa kipindi cha mwaka 2018 hadi 2020,” alisema Dk. Masanika.

Mbali na wahitimu 2,037, mradi pia ulisaidia kutoa mafunzo kwa watumishi wa hospitali 113, rasilimali watu 31, wakufunzi 168, watoa huduma kwa mama na mtoto 175, wasimamizi 67, wauguzi na wakunga wapya 850 na kuwafikia wanafunzi wa sekondari 6,956.

Mmoja wa wanufaika, Grace Mliambate kutoka katika chuo cha uuguzi na ukunga cha St Magdalene mkoani Kagera, alisema kukosekana kwa vifaa vya kufundishia ilikuwa ni chanzo cha upungufu wa watoa huduma hao nchini.

Mradi huo wa ukunga salama, umeshirikisha  taasisi isiyo ya kiserikali JHPIEGO ,wawakilishi kutoka Chama cha Wakungwa  Canada (CMA) na Chama cha Wakunga  Tanzania (TAMA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles