22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa Timiza Malengo kuwafikia Wasichana balehe kote nchini kuzuia maambukizi ya VVU

Na Mwandishi Wetu, Iramba

Serikali imejipanga kuhakikisha inawafikia wasichana balehe na wanawake vijana kote nchini kupitia mradi wa Timiza Malengo ambao unatekelezwa kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU na kupunguza ushawishi kwa wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 24.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Wenyeulemavu), Jenista Mhagama wakati akizungumza na wakazi wa Iramba mkoani Singida katika ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, walipo tembelea Mradi wa Timiza Malengo kuona utekelezaji wake.

Amefafanua kuwa serikali imelenga kundi hilo kwa kuzingatia takwimu za viashiria vya utafiti wa viashiria vya Virus vya UKIMWI (THIS) za mwaka 2017 ambapo zinaeleza vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40 na kati ya vijana hao asilimia 80 ni vijana wa kike, hii ni dhairi kwamba mapambano lazima azidishwe kwa vijana wetu ili tuendelee kuwakinga.

Waziri Jenista Mhagama(mwenye koti la bluu) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI wakimsikiliza mmoja wa wanufaika wa mradi nje ya mfumo wa shule, Neema Naaman anayefuga kuku wa nyama kutokana na uwezeshwaji wa mtaji kutoka mradi wa Timiza Malengo wakati wa ziara ya kamati hiyo wilayani Iramba mkoani Singida.

Mhagama amesema kuwa Mradi huo umeanzia katika mikoa mitano ya mfano ikiwa na lengo la kuwafikia vijana wote wa kitanzania wenye sifa zinazoendana na mradi huu,ili waweze kupata elimu itakayowawezesha kujitambua na kuepukana na vishawishi vinavyweza kuwapelekea kupata maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.

Akitaja mikoa hiyo ni pamoja na Morogoro, Dodoma, Singida, Geita na Tanga ambapo wamelenga kundi la wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walio ndani ya mfumo wa shule,kuendelea na masomo na kufikia ndoto zao wakiwa salama bila maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Aliongeza kuwa ni muhimu jamii kubadili mtazamo juu ya wasichana balehe na wanawake vijana ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi ili wajikwamue na kuinua wengine.

“Tumeona hapa vijana wawili waliotoa ushuhuda juu ya Mradi huu namna ulivyowasaidia na wengine wakajiongeza hadi kununua Mbuzi, bati, kuku na mwingine anaweza hata kununua chakula kupitia pesa hii wanayoipata ya mradi huu ambapo pia kuna vijana wengine wameweza kulea wadogo zao ambao wameachwa na wazazi wao na kuweza kujenga nyumba ambazo hadi sasa zipo kwenye renta,” amesema Mhagama.

Ameagiza halimashauri kuanza kutengeneza mpango wa ndani kupitia mapato ya ndani kuona namna ya kuhuisha katika hii programu.

“Pia idara ya maendeleo ya jamii na vijana tuwaombe kuunga juhudi za Rais anapofanya kazi nzuri ya namna hii kwa kushirikiana na wadau kupitia familia lengwa waanze kuwajenga, kuwaandaa ili wajenge uchumi wenyewe hata mradi ukiisha ile miradi inayokuwa imeanzishwa inakuwa tayari imeimarika na yule mbuzi aliyenunuliwa leo atakuwa tayari kazaa na kuna ongezeko la mbuzi wengi, kesho na keshokutwa familia hizo zinaweza kusaidiana zenyewe,” amesisitiza Mhagama.

Aidha, amewaelekeza watendaji wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanakuwa na kanzudata ya wanufadika ili kusaidia uendelevu wa programu na kuhakikisha waelimisha rika wanapatiwa ushirikiano wa kutosha ili wafikie kundi kubwa lililoachwa nyuma.

Awali, akitoa ufafanuzi Kaimu Mkurugenzi wa Mwitikio wa Taifa wa TACAIDS, Audrey Njelekela amesema Mradi wa Timiza malengo unaratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na kutekelezwa na Serikali kupitia Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto, Wizara ya Elimu Sayansi na Technolojia, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini(TASAF), AMREF na TAYOA.

Kaimu Mkurugenzi wa Mtikio wa Taifa kutoka TACAIDS, Audrey Njerekela akifafanua jinsi mradi wa Timiza malengo unavyotekelezwa wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI wilayani Iramba Mkoani Singida Oktioba 16, 2021

Aliongeza kuwa mradi huo umetekelezwa tangu Januari 2018 hadi 2020 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na welengwa wakiwa ni wasichana balehe na wa wanawake vijana waliopo katika vijiji 50 vinavyotekeleza Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) Wilayani humo.

Naye mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI, Fatma Taufiq alisema kuwa ni muhimu serikali kuendelea utoaji elimu kuyafikia makundi ya wasichana balehe na wanawake vijana, kwa kuzingatia ndio kundi lililokatika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Fatma Taufiq akizungumza na wanakazi wa Iramba wakati kamati hiyo ilipotembelea Wilaya hiyo kwa lengo la kukagua Utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo, kushoto kwake ni Waziri Nchi, Jenista Mhagama na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda.

Aidha, amewahasa vijana kutumia miradi hiyo kama chachu ya kujikwamua kiuchumi na kutumiza ndoto zao huku wakichangia maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Katika ziara hii tumoena namna serikali inavyotekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha kundi la vijana linalotajwa kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU yanahudumiwa ipasavyo na kufikia Tanzania isiyo na maambukizi mapya. Pia miradi hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa usahihi ili kuleta tija katika jamii zetu na kuhakikisha inawekewa mpango endelevu na kufikia mikoa yote ili kuwa na vijana wenye kujitambua na kutimiza ndoto zao,” amesema Taufiq.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akieleza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI kabla ya kutembelea miradi ya Timiza Malengo inayoratibiwa Wilayani hapo mkoa wa Singida.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ameishukuru serikali kwa kutoa kipaumbele kwa Wilaya hiyo katika utekelezaji wa Mradi huo ambao umeweza kuchangia kuinua maendeleo ya vijana wengi japo bado kuna uhitaji,pia aliishukuru kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya Bunge kutembelea na kuona utekelezaji wa Programu ya Timiza malengo na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maeneo yote muhimu yanayohusu mradi yanaedelea vyema.

Pia alitoa ahadi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,kazi,Ajira na wenyeulemavu Mhe Jenista Mhagama kwa kuendelea kutunza kanzi data ya wanufaika wa mradi ili matunda ya mradi huu yasipotee.

Wilaya itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha kunakuwa na bajeti ya kutosha katika kuyahudumia makundi haya muhimu kwenye jamii,alisema Mwenda.

Sehemu ya washiriki wa Mpango huo.

Ziara hii imetekelezwa na kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kwa lengo la kukagua miradi inayotekelezwa na TACAIDS hususani utekelezaji wa Mradi Timiza Malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) wenye lengo la kinga dhidi ya Maambukizi ya VVU kwa kundi hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles