Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MRADI wa kuchunguza ugonjwa wa selimundu kuanzia kipindi cha ujauzito (new born screaming) uliokuwa uanze kufanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesitishwa.
Hayo yalielezwa juzi na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Selimundu ambaye pia ni mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS), Profesa Julia Makani, alipozungumza na MTANZANIA Jumamosi.
“Tulitarajia kuanza mradi huu baada ya kuisha kwa ule wa awali ambapo watu wapatao 6,000 waligundulika kuwa na ugonjwa wa selimundu, katika huu mradi mpya tulitaka kuanza kupima ugonjwa tangu mtoto akiwa tumboni.
“Kwa sababu inawezekana kugundua tatizo katika kipindi hicho cha ujauzito inasaidia mtoto atakapozaliwa kuanza kupatiwa matibabu mapema,” alisema.
Alisema mradi huo ulisitishwa Agosti mosi, mwaka huu na kwamba bado Muhas inaendelea kutafuta wafadhili ili kuanza rasmi uendeshaji wake.
Katika mradi wa awali ambao ulihusisha zaidi masuala ya utafiti ambapo jumla ya wagonjwa 6,000 waliogundulika kuwa na ugonjwa huo walipewa matibabu ya bure chini ya mradi huo.
Mradi huo wa awali ulidumu kwa miaka 10 na kuhitimika rasmi Machi, mwaka huu.