27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bandari yajitapa kuingiza meli kubwa

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko

Na Mwandishi Wetu,

BANDARI ya Dar es Salaam imetangaza kufungua milango kwa meli kubwa zaidi kutia nanga katika bandari hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam mara baada ya manahodha wa Mamlaka hiyo kufanikiwa kuingiza meli kubwa zaidi katika historia ya bandari hiyo yenye urefu wa mita 261.

Alisema meli hiyo iitwayo MV Hammonia Grenada, ina uwezo wa kubeba makasha 4,256, imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na kushusha makasha 483 na kupakia makasha 656 kabla ya kuelekea nchini Thailand.

“Milango sasa ipo wazi kwa meli kubwa zaidi kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, kwani teknolojia ya meli za kisasa inaruhusu,” alisema.

Alisema mbali na teknolojia iliyotumika kutengeneza meli hizo, Mamlaka imeboresha ujuzi wa manahodha wake baada ya kuwapeleka katika nchi za Afrika Kusini, Denmark na Ufaransa kupata mafunzo jinsi ya kuingiza meli za aina hiyo bandarini.

Alisema kuingia kwa meli hiyo ya MV Hammonia Grenada na kutia nanga ni uthibitisho tosha kwamba bandari ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa kwa kutumia miundombinu iliyopo na kwa ufanisi mkubwa.

“Bandari yetu ina uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa huo katika gati zake nne, gati hizo ni namba 8, 9, 10 na 11 ambazo zina kina chenye urefu mita 11,” alisema.

Alisema meli za aina ya Hammonia Grenada awali zilikuwa zikiishia bandari ya Mombasa pekee.

“Wapo waliokuwa wakifikiri kwamba bandari yetu sasa haifanyi kazi lakini ukweli ni kwamba bandari yetu ipo sawa na inaendelea kupokea meli kama kawaida.

“Na kuwathibitishia hilo, hata Rais John Magufuli wakati alipokuja kufanya ziara hapa bandarini kulikuwa na meli nyingine saba zimetia nanga.”

Naye Nahodha Mkuu wa Mamlaka, Kapteni Abdullah Mwingamno, alisema meli hiyo ndiyo kubwa kuliko zote ambazo zimewahi kuingia katika bandari ya Dar es Salaam.

“Hapo mwanzo mlango wa bandari yetu ulitengenezwa kuweza kuhudumia meli zenye urefu wa mita 234 tu, lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia na jinsi meli zenyewe zinavyojengwa imeweza kuingiza hata meli za urefu mkubwa zaidi,” alisema Mwingamno ambaye ndiye aliyeingiza meli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles