32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI MANGROVES CAPITAL AFRICA KUTOA MBADALA KIUCHUMI KULINDA HAZINA

NA JOSEPH LINO


UTAJIRI uliyojificha katika misitu ya mikoko ya Rufiji Delta ina thamani ya kiuchumi na maendeleo na hivyo ni hazina kubwa kwa Taifa hili.

Fursa za uchumi zilizopo katika Msitu wa Rufiji unahitaji juhudi za pamoja katika kuhamasisha na kuwezesha jamii inayotegemea mikoko kutafuta njia mbadala ya kuzalisha kipato bila kuathiri mikoko ambayo ni miti adhimu na pendwa.

Rufiji Delta namna ilivyo kiasilia ni mto huo katika upevu wake na hivyo kujigawa kama vidole kuashiria kufika mwisho wa mto na kutengeneza visiwa vingi ambako watu wanaishi kwenye misitu ya mikoko maeneo yote.

Rasilimali iliyopo Rufiji Delta bila kuelewa umuhimu wake inaendelea kuharibiwa kila siku na kusababisha kutoweka kwa rasilimali hizo.

Kwa mujibu wa Wetlands International, Rufiji Delta ina eneo la ukubwa hekari 53,225 ambapo zaidi asilimia 40 misitu ya Rufiji Delta tayari imeharibiwa kutokana na shughuli za kilimo cha umwagiliaji, mashamba ya mpunga, uvunaji wa mbao na uvuvi kwa sababu ya kukosekana shughuli  mbadala za kuwaingizia kipato jamii ya maeneo hayo.

Kutokana na uharibifu huo unaotishia kutoweka kwa misitu ya mikoko nchini, Wetlands imezindua mradi wa Mangroove Capital Africa Tanzania unaolenga  kutunza na kuhifadhi misitu ya mikoko nchini.

Mradi wa Mangroove Capital Africa utaanza kutekelezwa misitu ya mikoko ya Rufiji Delta  na utagharimu Euro milioni sawa na Sh bilioni 5.9 kwa miaka miwili ya awamu ya kwanza na unafadhiliwa na DOB Ecology.

Mratibu wa mradi huu kwa upande wa Afrika Mashariki, Julie Mulonga, anasema mradi wa misitu ya mikoko unaanzia  Rufiji Delta kutokana  na kushamiri kwa uharibifu wa mikoko unaondelea maeneo hayo.

“Lengo kuu ni kuangalia namna tunaweza kuendeleza na kutunza mikoko na kuiwezesha jamii inayotegemea mikoko na kuishi maeneo hayo,” anasema.

Anasema umuhimu wa misitu ya mikoko ni sehemu ya mazalia ya samaki na viumbe wengine majini.

Julie anafafanua namna  wavuvi wa Rufiji hawapati samaki wa kutosha kutokana na uharibifu wa mikoko uliokithiri maeneo mengi.

“Wananchi wanaoishi katika maeneo ya pwani lazima watunze na kuhifadhi mikoko kwa maendeleo ya kizazi kijacho,” anaelezea Julie.

Anafafanua kuwa misitu ya Rufiji Delta ndio eneo peke ambako watu wanaishi ndani yake, hivyo maisha yao yote  hutumia mikoko  katika shughuli za kila siku.

Mratibu  huyo anaelezea kuwa katika awamu ya kwanza watashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ili kuandaa  na kuhakikisha kuna mpango  wa usimamizi ambao utakuwa mwongozo wa uhifadhi wa misitu ya mikoko ya Rufiji Delta.

“Mradi wa Mikoko utajikita katika utafiti wa kuangalia taarifa sahihi za maeneo husika ambazo zitatuwezesha kuanza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo  kutoa elimu na miradi ya uwezeshaji kwa jamii,” anaelezea.

Julie anasema jamii yote inayozunguka maeneo ya misitu ya Rufiji Delta watapatiwa mafunzo na kuwawezeshwa na kuunda makundi kama ‘vicoba’ na shughuli za kutengeneza bidhaa  za  mikono ili waepuke kuharibu mikoko hasa wakina mama. Pia kufanya miradi ya kurejesha misitu katika upandaji  wa maeneo ambayo mikoko ilishakatwa.

Anafafanua kuwa nchini Senegal wakinamama walipatiwa mafunzo na kuwezeshwa katika vikundi vya vikoba ili waendeleze maisha yao.

Naye Meneja wa Mradi wa Mangroves Capital Africa nchini, Ismail Saidi, anaelezea changamoto kubwa ambazo zinatishia uhai wa misitu ya mikoko Rufiji Delta.

“Changamoto kubwa ni shughuli ambazo zinahusiana  na matumizi ambayo si endelevu kwa misitu kama kilimo cha kuhamahama ikiwemo mpunga  pamoja na uvunaji wa kibiashara wa mbao ambazo zinasafirishwa kwenda Uarabuni kupitia Zanzibar,” anasema Saidi.

Kwa upande wake, Ofisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Froliana Mkei, anasema hali ya misitu ya mikoko imekuwa ni mbaya kwa kiasi kikubwa kutokana shughuli za binadamu zinaoendelea  katika maeneo hayo.

“Wananchi wengi wanakata mikoko kiholela wakiwemo wale ambao wana leseni na maisha yao yote wamekuwa wakitegemea mikoko,”

Anaelezea hali ilivyo katika maeneo ya pwani hasa Dar es Salaam ambako mikoko imeathiriwa kutokana na shughuli za ujenzi wa makazi na hoteli.

Pia idadi ya watu inaongezeka wanaoishi na kutegemea misitu kama Rufiji Delta.

“Uharibifu huu wa mikoko umesababisha samaki  kutoweka na wavuvi wengi  kwa sasa wamehamia kuchoma mkaa wa mikoko ambao ni bora sana,” anasema Mkei.

Kwa mujibu wa Mkei, wanashindwa kufuatilia na kusimamia  kuzuia uharibifu huo kutokana na ukosefu wa vifaa kama maboti na vizuizi vya mahakama kutokana na  kesi mbalimbali  ambazo zinachangia katika uharibifu wa mikoko hasa Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles