25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mpishi anayedumbukiza mikono kwenye mafuta ya moto bila kuungua

Superhands
Kann Trichan akiweka mikono yake kwenye mafuta

 

NA JOSEPH HIZA,

SIKU moja iwapo utanunua chakula katika genge moja la vyakula katika mtaa mmoja wa jiji kubwa la kaskazini mwa Thailand la Chiang Mai wakati unakula tegemea kuhisi kitu fulani kisicho cha kawaida kikiwa kimekwama katikati ya meno yako.

Wakati ukidhani pengine ni kipande cha mfupa wa kuku, utakapokitoa, utashangaa kukutana na kucha za binadamu!

Kwanini? Mpishi katika genge hilo hutumia mkono wake kukaangia kuku hao, kwa maana hiyo kucha hizo zitakuwa bila shaka zimenyofoka kutoka moja ya mikono yake na kuchanganyika na kuku hao!

Hahahahaa, si kweli bali huo ni utani tu. Lakini tunakusimulia kuhusu jamaa mmoja katika mtaa huo jijini humo, ambaye hutumia mikono yake tupu kukaangia kuku. Je, inawezekana?

Unaweza usiamini hilo lakini ndio ukweli. Mpishi wa mitaani humo mwenye umri wa miaka 54, Kann Trichan anaweza kupika kwa kuzamisha vidole vyake katika chombo kinachochemka mafuta hadi nyuzi joto 480 bila kudhurika popote.

Uwezo wake huo wa kushangaza, umemjengea umaarufu mkubwa duniani.

Watu kutoka kona zote za dunia hutembelea katika genge lake lijulikanalo ‘Kuku wa Kukaanga kwa Binadamu wa Mikono ya Chuma’ ili kumshuhudia Kann akitumia mikono yake kuopoa kuku kutoka mafuta yachemkayo.

Kwa umaarufu huo, yeye na mkewe wamepata fursa ya kusafiri huko na huko kuonesha maajabu hayo ya dunia.

Yeye mwenyewe hafahamu imekuaje akawa na uwezo huo, lakini anafuraha kwa alichobarikiwa kwani kimempatia umaarufu na kumletea wateja wengi.

Uzuri zaidi wa hilo ni kwamba wateja hao wanazidi kuongezeka siku hadi siku katika genge lake hilo la biashara.

Simulizi za jinsi alivyojigundua kuwa na uwezo huo wa ajabu inafurahisha.

Kann Trichan kwanza aligundua kuwa na kipaji hicho kisicho cha kawaida miaka 11 iliyopita wakati akiwa na umri wa miaka 43, wakati kwa bahati mbaya aliporukiwa na mafuta yachemkayo mwilini mwake.

Ilikuaje? Wakati akiwa kazini amekaa chini ya mti wa mwembe alisikia kelele za parakachaa! Parakachaa! zikitokea juu ya mti huo na alipoangalia juu akamuona kuchakuro akila embe katika tawi la mti huo.

Katika harakati zake hizo, mnyama huyo akasababisha kuanguka kwa tunda kubwa, ambalo moja kwa moja liliangukia usawa wa chombo kikubwa kichemkacho mafuta.

Akiopoa vipande vya kuku kwa vidole
Akiopoa vipande vya kuku kwa vidole

Lilipotua katika kikaangio hicho kikubwa na kutoa ukelele wa chubwi! mafuta yakaruka na kumwagikia Trichan mwilini na kichwani, ambapo alipiga ukelele kwa hofu.

Teksi likaja na kumkimbiza nyumbani na wakati alipoinuka siku iliyofuata akijiandaa kwenda kuonana na daktari, kwanza alichukua kioo na kujiangalia na kwa mastaajabu hakuona majeraha yoyote yanayotokana na kuungua.

Na wekundu wa ngozi ulikuwa ukiondoka na ngozi yake ilikuwa ile ile na hivyo hakuona umuhimu tena wa kwenda hospitali badala yake akarudi kazini, kwa mastaajabu ya wachuuzi wenzake wengi mtaani hapo.

“Hawakuweza kuamini kuwa nimerudi kazini mara ile,” anasema na kucheka. Kuanzia hapo kila mtu akataka kumuona mtu huyu aliyenusurika baada ya kuoga mvua ya moto ya mafuta yanayochemka vikali.

Trichan akaanza kufanya majaribio kwa kuchukua vipande vya kuku wanaochemka kutoka chombo chenye mafuta kwa mikono yake.

“Sikujua kama nilikuwa na uwezo huo, ni kama wazimu, lakini uwezo nilionao umefanya genge langu kuwa na shughuli nyingi kila siku huku watalii na wateja wakitaka kuniona,” anasema baba huyo wa watoto wawili.

Genge lake hilo dogo maarufu liko nje ya Chuo Cha Ufundi Chiang Mai, maili 470 kaskazini mwa Bangkok.

Anasema: “Usisahau, wakati ukiwa eneo hili njoo na unione na jaribu kuonja kuku wangu – kuku waliokaangwa kwa binadamu wa mikono ya chuma.”

Trichan pia anashikilia rekodi katika kitabu cha maajabu ya dunia cha Guinness Record kwa kuchukua vipande 20 vya kuku kutoka mafuta yanayochemka katika nyuzi joto 480 kwa dakika moja tu.

Kuhusu nini anahisi anapoingiza mkono katika mafuta, anakiri kwamba huhisi joto la mafuta lakini halimwathiri wala kumwachia majeraha ya moto.

Naweza kupika wali, kuku na vitu vingine vingi kwa mikono yangu mitupu, anajigamba.

Bintiye Supalak mwenye umri wa miaka 37 na mwane wa kiume Jessada (30), nao wana haya ya kusema;

“Kamwe hatukuwahi kukinai kumwangalia baba yetu akifanya maajabu, inashangaza kwa kweli,” anasema Jessada. “Tunajivunia kuwa na baba kama huyu.”

Wanasayansi bado hawajaweza kubainisha sababu ya mpishi huyu kuwa na uwezo huo wa ajabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles