27.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Mpira wa kikapu unavyolala wakati kunakucha

kikapu

Na MARTIN  MAZUGWA

UKIACHANA na  mchezo wa soka, mchezo mwingine unaoongoza kwa kuingiza fedha nyingi duniani ni mpira wa kikapu ambao unapendwa zaidi nchini Marekani na duniani kwa ujumla.

Mchezo huu ulijipatia umaarufu mkubwa hapa nchini kupitia kwa mkongwe na mchezaji bora wa muda wote wa mchezo huo  Michael Jordan, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kufunga  zaidi.

Mbali na Jordan ambaye ndiye kioo cha mchezo wa kikapu duniani, lakini pia kuna baadhi ya nyota ni vigumu  kuwasahau  kutokana na mchango wao katika mchezo wa kikapu.

Nyota kama vile Allen Iverson, Karim Abdul Jabal, Shaquille O’neal, Wilt Chamberlain na Larry Bird ni baadhi  ya nyota waliofanya vizuri katika mchezo huu maarufu.

Ligi ya kikapu nchini Marekani (NBA) inakusanya  nyota  wengi kutoka  pande mbalimbali  za dunia ili kuongeza mvuto na ushindani  ili kuwavutia  wadau na wapenzi wa mchezo huu.

Nyota kama vile Yao Ming kutoka nchini  China, Žydrūnas Ilgauskas, raia wa Lithuania, Hedo Turkoglu raia wa Uturuki, Luol Deng raia wa Sudan ambao wanafanya vizuri nchini Marekani.

Haikuwa ajabu kuona pia  nyota Mtanzania Hasheem Thabit  akichezea ligi hiyo alipoonekana kwa mara ya kwanza akiwa na timu ya Memphis Glizzlies msimu wa 2011-12 iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ya kikapu nchini Marekani  ambapo siku za hivi karibuni amepotea katika mchezo huo.

Mbali na kucheza katika Oklahoma, nyota huyo amezunguka baadhi ya timu kama vile Dakota Wizards, 2011–2012 Houston Rockets, 2011 Rio Grande Valley Vipers,  2012 Portland Trail Blazers, 2012–2014  Oklahoma City Thunder  pamoja na  2014–2015  Grand Rapids Drive.

Timu kama vile Cleverland, Miami Heart, Golden  State, Los Angeles Lakers, Oklahoma City Thunder, Chicago Bulls, San Antonio Spurs, Philadephia 76ers  ni baadhi ya timu zilizojizolea mashabiki  wengi nchini kutokana  na uwezo wao zinazouonyesha katika ligi ya (NBA).

Mchezo huu hivi karibuni umekuwa ukipendwa zaidi kutokana na uwezo unaoonyeshwa na nyota kama Le bron James wa Cleverland Cavariells, ambaye ni mchezaji bora wa msimu huu (MVP) pamoja na nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry ambaye alinyakua tuzo ya mchezaji bora msimu uliopita.

Wakati mpira wa kikapu ukizidi kufanya vizuri  duniani, hali ni tofauti na nchini ambapo mchezo huu umepoteza mvuto kutokana na kukosa  makampuni ya kuudhamini na hivyo kuufanya udumae licha ya kuwa na mashabiki wengi.

Mchezo huu nchini ulikuwa na wapenzi wengi pamoja na timu zilizokuwa zikichuana katika mashindano mbalimbali lakini hivi sasa kasi imepungua tofauti na zamani.

Mashabiki wengi walikuwa wakijitokeza kushudia michezo ya timu kama vile Savio, JKT Stars, ABC na Kurasini  ambazo baadhi zilifanya vizuri lakini kwa sasa zinajikongoja.

Miaka inavyozidi kuendelea kuna hatihati tukapotea katika mchezo huu iwapo tutakosa wadhamini ambao watazihudumia timu kwa kuzipa mahitaji muhimu ili ziendelee kufanya vizuri.

Hali imekuwa tofauti kabisa kwani mashabiki wanaojitokeza hivi sasa viwanjani ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo mashabiki wengi walikuwa wanajitokeza viwanjani kuupa sapoti mchezo huu.

Licha ya Savio kubeba taji la Ligi ya Taifa ya mpira wa kikapu  Tanzania Bara (RBA), lakini haijaongeza mvuto wowote kwa mashabiki  tofauti na ligi nyingine za nje ya nchi ambazo zimekuwa zikipewa kipaumbele katika matangazo kutokana na ubora wa ligi hizo.

Mchezo huu utaendelea kubaki hivi mpaka lini?

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), linapaswa

kujiuliza swali hili na jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili na Tanzania isonge mbele zaidi ya hapa.

Makampuni  makubwa ya uwekezaji yanapaswa  kutupia jicho na upande huu na kuwekeza katika mchezo huu  kwani ikiwa mpira wa kikapu utapewa kipaumbele, ipo siku tutashuhudia Tanzania ikimpata mrithi wa Hasheem Thabit ndani ya (NBA.

Wahenga wanasema kuteleza sio kunguka, TBF inapaswa kuinuka na kuendelea na safari huku wakiangali walipojikwaa ili makosa waliyoyafanya yasijirudie na hivyo mchezo huu uweze kupata mafanikio kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles