23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Mwaka mmoja wa Magufuli alikotoka, alipo na anakoelekea

0d6a8358
Rais Dk. John Magufuli

 

Na WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

JANA Rais Dk. John Magufuli alitimiza mwaka mmoja madarakani tangu  aapishwe Novemba 5, mwaka jana huku akionekana kupata mafanikio na changamoto katika maeneo kadhaa.

Ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, mwenendo wa utawala wake katika kipindi cha mwaka mmoja na kauli za wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na watu wa kada mbalimbali yote hayo yametoa taswira nzima ya alikotoka, alipo na anakoelekea.

Magufuli aliapishwa baada ya kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana ulioshirikisha pia wagombea saba wa vyama vya upinzani akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyegombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

MAENEO ALIYOFANIKIWA

UDHIBITI WA FEDHA

Hili ni eneo ambalo katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake Rais Dk. Magufuli anaonekana kufanikiwa na hata kusifiwa na wapinzani wake.

Hatua hiyo inaelezwa imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa Serikali yake kuhamisha uwekaji wa fedha za mashirika yake kutoka katika benki binafsi na kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huku sababu kubwa ikiwa ni kuweka wazi mapato na matumizi.

Si hilo tu, uamuzi wa Rais Dk. Magufuli mwenyewe kufuta safari za nje kunaelezwa kuipunguzia mzigo wa gharama Serikali huku yeye mwenyewe akisema katika kipindi cha mwaka mmoja kati ya mialiko 47 aliyoipata ni mitatu tu aliyokubali kusafiri nje ya nchi.

Pamoja na hilo uamuzi wa Serikali yake kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama kufuta shamrashamra za sherehe za kitaifa, mikutano/makongamano ya gharama kubwa nk.

Katika kudhibiti fedha ndiko kunakotajwa kuielekeza Serikali yake kufanya uhakiki wa watumishi wake na kugundua uwepo wa watumishi hewa 17,500 na hivyo kudai kuokoa kiasi cha Sh bilioni 19.

Si hilo tu, kubana kwingine matumizi kunatajwa kutokana na uamuzi wa Serikali yake kupanga kulipa mishahara ya juu kabisa isiyozidi shilingi milioni 15  kutoka milioni 30 -45

Katika kudhibiti hilo, Aprili mwaka huu Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Juliet Kairuki ambaye alitajwa kugoma mshahara wake toka mwaka 2013 kwa madai kuwa ni mdogo.

Pamoja na hayo, Serikali yake imejigamba kutimiza lengo lake la makusanyo ya kodi yanayofikia Sh trilioni 1.2 kutoka Sh bilioni 800.

Ni makusanyo hayo ndiyo ambayo Serikali inasema imeyatumia kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 kutoka nchini Canada kwa malipo ya mkupuo mmoja wa fedha taslimu zaidi ya Sh bilioni 120.

Ndege hizo zimefufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambalo kwa muda mrefu lilidorora na halikuwa na mafanikio yoyote ya kibiashara.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam juzi, Rais Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano Serikali yake itakuwa imenunua jumla ya ndege saba.

Alizitaja aina ya ndege inazotarajia kuzinunua kuwa ni pamoja na Jet, Bombardier na Boeing.

Si hayo tu katika kubana huko matumizi, Serikali yake imefanikiwa kununua madawati mengi, vitanda katika hospitali ya Taifa Muhimbili, kupanua barabara ya Mwenge-Morocco.

NIDHAMU

Hili ni eneo jingine ambalo wengi wanaona Rais Magufuli amefanikiwa wakiwamo wanasiasa, wasomi na watu wa kada mbalimbali.

Watu ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa utendaji wa Rais Magufuli, wanasema pamoja na changamoto zilizojitokeza lakini hatua yake ya kuwaondoa kazini watumishi wasio waadilifu takribani 150 imerudisha nidhamu ya utumishi wa umma.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili Jaji mstaafu, Amiri Manento, alimsifu Rais Magufuli katika eneo hilo akisema amerejesha nidhamu kama ile iliyokuwapo wakati wa ukoloni na kwamba kwa sasa watu wanathamini kazi na si fedha tena kama ilivyokuwa mwanzoni.

Kauli inayofanana na hiyo ilitolewa pia na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), James Seka, ambaye anasema: “Kwenye mahakama zetu tunaona watumishi wa umma wanafanya kazi kwa uadilifu na vile visingizio visivyo na kichwa wala miguu vimepungua, watu wanawahi makazini na wanakaa hadi muda sahihi wa kutoka, unaona hata majaji na mahakimu wako makini katika kutimiza malengo.”

Katika eneo hilo la nidhamu na maadili, Rais Magufuli anaelezwa kutekeleza ahadi yake ya kuanzisha Mahakama ya Mafisadi itakayoendesha kesi za rushwa na wahujumu uchumi.

Mahakama hiyo tayari imekwishaanza kazi wiki hii baada ya majaji wake 14 kupatiwa mafunzo Lushoto mkoani Tanga.

KUHAMIA DODOMA

Uamuzi mwingine ambao unatajwa kama sehemu ya mafanikio katika utawala wa Rais Magufuli ni kuhamishia Serikali yake mkoani Dodoma.

Ingawa zoezi hilo bado halijakamilika, baadhi ya wachambuzi wanasema kutokana na hulka ambayo Rais Magufuli mwenyewe ameionyesha muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani na uthubutu wake wa kuhamishia baadhi ya ofisi mkoani humo kunaweza kutimiza ndoto ya muda mrefu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

ELIMU BURE

Pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, uamuzi wa Serikali yake kutangaza kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne inaelezwa kuwa ni hatua kubwa.

Tangu Desemba, mwaka jana hadi Mei, mwaka huu Serikali ilisema imetoa kiasi cha Sh bilioni 94.2 katika shule mbalimbali nchini.

Pamoja na hilo, Serikali kwa kushirikiana na watu binafsi imetekeleza kampeni kubwa ya kutengeneza madawati 552,630 ambayo yamepelekwa katika shule mbalimbali nchini.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti, viongozi wa dini akiwamo Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi, Mdhamini wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste nchini, Askofu David Mwasota, wamesema Rais Magufuli amethubutu kusimamia na kutekeleza mambo magumu.

Wakati Askofu Kilaini akisema anafahamu changamoto zipo huku akiulinganisha utawala wake na ule wa Mwalimu Julius Nyerere au aliyepata kuwa Waziri Mkuu Hayati Moringe Sokoine, kwa upande wake Mufti Zuberi, alisema alimsifu kwa kuhakikisha watu wanapata vipato vya haki na hivyo nchi kujipatia baraka.

Askofu Mwasota yeye alisema: “Najua tunaumia kwa sasa kwa sababu ya mazoea lakini tukubali utendaji wake utaliweka taifa sehemu nzuri ya vizazi vyetu kuishi.”

CHANGAMOTO

Licha ya watu wengi kusifu utendaji wake katika usimamizi wa fedha na nidhamu, hata hivyo Rais Magufuli amenyooshewa kidole hususani jinsi anavyoshughulikia masuala yanayogusa demokrasia, sheria, uchumi na jinsia.

DEMOKRASIA

Uamuzi wa kupiga marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano yake hadi mwaka 2020, kupoka kile kinachodaiwa kuwa ni mamlaka ya Bunge ikiwa ni pamoja na kuzuia matangazo ya moja kwa moja, kumemjengea taswira ya kiongozi mbabe.

Ingawa yeye mwenyewe juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari alikana kuminya demokrasia, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu, anautazama mwaka mmoja wa Rais Magufuli kama mchungu kwa upinzani na mustakabali mzima wa taifa.

Lissu ambaye kwa taaluma ni mwanasheria na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amerejea kauli ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara akimtaja Rais Magufuli kama mtu asiyejali utawala wa sheria na demokrasia.

Kauli inayolandana na hiyo imetolewa pia na Mwenyekiti wa Chama cha  ACT- Wazalendo, Anna Mghwira, Rais wa (TLS), Seka, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo- Bisimba na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Si hao tu Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo, licha ya kusifu uthubutu wa Rais Magufuli kupambana na watu waliozoea kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa, alimtaka kutoa wigo kidogo wa kusikiliza kelele za wapinzani wenye hoja zenye mashiko.

“Mwaka mmoja wa Magufuli umeonyesha kuwa ni Rais tishio kwa nchi yetu,” anasema Lissu.

Lissu anasema katika kipindi cha mwaka mmoja Rais Magufuli ameonyesha kuhodhi mamlaka ya kila jambo ikiwamo uidhinishaji wa malipo mbalimbali ya Serikali.

“Ni Rais ambaye anadhani kuwa ana  mamlaka ya kila jambo, kwa mfano hivi sasa malipo yote ya Serikali anayapitisha yeye mwenyewe, huu ni utawala wa aina gani?” alihoji Lissu.

UTAWALA BORA

Pamoja na Lissu, Rais wa TLS, Seka licha ya kumsifu kurejesha nidhamu kazini ameonyesha shaka kama hatua ya kuwaondoa watumishi wanaodaiwa kutokuwa na maadili ilifuata sheria.

“Kwenye suala la haki za binadamu bado tuna tatizo kubwa na watu wengi hasa hawa ambao wametumbuliwa hatuna uhakika sana kama utumbuaji huo ulifuata kanuni na sheria za utumishi wa umma, hawajapata fursa ya kujitetea kwa hiyo kwenye eneo hilo kidogo kuna walakini,” anasema.

Kauli kama hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa LHRC, Bisimba ambaye anasema: “Tunapoangalia utumbuaji, sisi wa haki za binadamu tunaona kuna sheria na haki za binadamu hazikutumika. Wengi wanaotumbuliwa wana mkataba kama wamekosea kuna njia ya kisheria, lakini tulikuwa tunaona katika mikutano ya hadhara mtu anaambiwa ametumbuliwa, huo si utaratibu,” anasema.

AFYA/MIKOPO ELIMU/WAFANYAKAZI

Kukosekana kwa dawa huku baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu kumlalamikia Rais Magufuli kushindwa kutimiza ahadi yake ya kusomesha watoto wa masikini, ni changamoto ambayo baadhi wanaona imeonekana wazi katika utawala wake wa mwaka mmoja.

Ingawa Rais Magufuli mwenyewe ameeleza sababu zilizochangia uhaba wa dawa ni pamoja na kubadili mfumo wa kuziagiza kwa kuachana na mawakala.

Kuhusu mikopo ya elimu ya juu licha ya yeye mwenyewe kulitolea ufafanuzi suala hilo huku akisema ameongeza fedha kutoka Sh bilioni 340 hadi kufikia Sh bilioni 473, bado wanafunzi wengi wamebaki na kilio huku hatima yao ikiwa haijulikani.

Takribani wanafunzi 3,000 waliokuwa wakipatiwa mikopo wameondolewa kwa madai ya kukosa sifa huku wanafunzi 66,000 wameripotiwa kukosa mkopo.

Hadi sasa Serikali inaelezwa kufanikiwa kuwakopesha wanafunzi 25,000 tu wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea.

TUCTA/CWT

Kwa upande wake vyama vya wafanyakazi (TUCTA) kikiwamo kile cha walimu (CWT), vimesema mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli umeleta mwelekeo kwa upande wao.

Katibu Mkuu wa CWT, Alhaji Yahaya Msulya, alisema walimu bado wana imani na Serikali ya Awamu ya Tano ingawa matatizo yao muhimu yakiwamo malimbikizo ya madeni bado hayajatatuliwa.

Msulya alisema hadi sasa walimu wanaidai Serikali Sh bilioni 56 ya madeni ya mishahara na upandishwaji wa madaraka wakati Sh bilioni 26 zikiwa ni za malimbikizo ya likizo.

UJENZI WA VIWANDA

Kuhusu ujenzi wa viwanda wakati baadhi wakiona bado ahadi yake hajaonyesha kuitekeleza sawa sawa, Wizara ya Viwanda imesema tayari viwanda vipya vidogo 3,800 vimejengwa nchi nzima kikiwamo kile cha chaki na maziwa kilichopo Meatu mkoani Simiyu.

Akizungumzia viwanda juzi, Rais Magufuli alisema ametekeleza ilani ya CCM inayotaka mchango wa viwanda upande kutoka asilimia 15 na kuzalisha ajira asilimia 45 na kusisitiza kuwa Serikali haiwezi kuvijenga bali itashirikisha sekta binafsi.

UCHUMI/WAFANYABIASHARA

Pamoja na Rais Magufuli kusifu Serikali yake kwa kukusanya mapato na kudhibiti fedha, baadhi wamekuwa wakilalamikia makali ya maisha kutokana na mzunguko mdogo wa fedha.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, anakiri kuwapo kwa mzunguko mdogo wa fedha na hivyo kusababisha biashara kuwa ngumu huku Serikali ikiwa imewarundikia mzigo wa kodi.

“Hali ya kibiashara imekuwa ngumu lakini tunaelewa imesababishwa na mipango au utaratibu uliokuwa umezoeleka siku za nyuma, baadhi walikuwa hawalipi kodi, inawezekana mambo yakaja kuwa mazuri,” anasema Minja.

Pamoja na hilo hatua yake ya kubadili msimamo na hata kuagiza sukari iliyodaiwa kufichwa ya bilionea Said Bakhressa iachiwe kwa sababu tu ya kufurahishwa na juhudi za mfanyabiashara huyo katika ujenzi wa viwanda, inaelezwa na baadhi kujenga taswira mpya ya Rais Magufuli.

Hatua hiyo ya kubadili msimamo inatajwa kuchukua sura tofauti na ile ya mwanzo akifahamika kama mtu asiye na masihara na mfanyabiashara asiyelipa kodi na anayekwenda kinyume na maagizo ya Serikali yake.

USAWA WA KIJINSIA

Miongoni mwa changamoto ambayo baadhi ya wafuatiliaji wakiwamo wasomi wanaona imeonekana wazi katika utawala wa Rais Magufuli, ni suala la usawa wa jinsia katika uteuzi wa nafasi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa LHRC, Bisimba, wamebaini katika eneo la wakuu wa mikoa kati ya 26 ni wanne tu ndio wanawake na kuna mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida, hakuna mkuu wa mkoa au wa wilaya mwanamke.

Katika ngazi ya wakuu wa wilaya, Bisimba anasema kati ya 134 wanawake ni 25 tu huku wakurugenzi wa jiji, manispaa na miji 185 wanawake ni 33 tu.

“Amepatikana Makamu wa Rais mwanamke ila Spika amerudia mwanamume na Naibu ndio mwanamke. Mawaziri kipindi kilichopita wanawake walikuwa asilimia 31.3 kwa sasa ni asilimia 21.0. Naibu mawaziri wameongezeka hadi kufikia asilimia 31.3 tofauti na kipindi kilichopita ambapo walikuwa asilimia 24.0. Makatibu wakuu wanawake ni asilimia 7.1 kwani wapo wawili kati ya 28 wakati kipindi kilichopita walikuwa asilimia 18.2 na manaibu katibu wakuu kipindi kilichopita walikuwa asilimia 40.7 wanawake na sasa ni asilimia 38.1,” anasema Bisimba.

Habari hii imeandaliwa na Markus Mpangala, Agatha Charles, Evans Magege, Rachel Mrisho na Aziza Masoud

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles