25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MPENZI WA NONDO ASHINDWA KUJUA MTAA IRINGA

FRANCIS  GODWIN NA RAYMOND MINJA, Iringa


USHAHIDI wa  kesi inayomkabili mwanafunzi, Abdul Nondo  umeendelea  kutolewa kwa  upande wa Jamhuri kupeleka  mashahidi  wengine wawili  kati ya wa nne.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi jana, ni pamoja na aliyekuwa mpenzi wa zamani wa Nondo  ,Veronica  Fredy (22) mkazi wa Igunga mkoani Tabora.

Shahidi  huyo ambaye  alifikishwa mahakamani hapo  akiwa  amefichwa sura yake kwa kufunikwa na polisi aliingizwa moja kwa moja mahakamani.

Baada ya kutoa ushahidi wake, alitolewa nje ya mahakama hiyo, chini ya ulinzi mkali wa polisi  ambapo alipandishwa kwenye gari pa polisi lenye vioo vyeusi. Mbele  ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, John  Mpitanjia, shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa aliwahi kusoma  na Nondo  Shule ya Sekondari Igunga.

Alidai wakiwa shuleni, walikuwa kipindi chote cha masomo yao, huku Nondo akiwa kiongozi wake,baadaye waliingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kabla ya  kuachana muda  mrefu.

Katika  mahojiano yake na  wakili wa Jamhuri,Alex Mwita na shahidi alisema elimu yake ni  kidato cha  sita na  sasa anajishughulisha na kazi ya ususi wa nywele  kijijini kwao Igunga.

Vero, alidai alimfahamu  Nondo tangu Agosti,2014  na kuwa mazingira ya kufahamiana  yalikuwa  ya shuleni  kama kiongozi  wake na  kuwa uhusiano wao wa mapenzi ulianza  mwaka 2015 hadi mwaka 2017 mwanzoni,baada ya hapo  wakaendelea na uhusiano wa kawaida.

Alisema njia  ambazo   walikuwa wakitumia kuwasiliana ni simu na  mitandao ya kijamii, hasa  Whatsapp na kusisitiza kuwa anachokumbuka  ni Machi 7, mwaka huu saa 9 usiku,  Nondo  alimpigia  simu.

“Ulikuwa usiku wa pekee  nikiwa nasumbuliwa na mafua, nilipigiwa  simu na Nondo akaniuliza  uko wapi, nikamjibu nipo nyumbani  Igunga,akaniuliza  unaishi na nani, nikamweleza naishi pekee yangu, akaniomba  aje kwangu ana matatizo nikamkatalia na kumkatia simu.

“Baada ya  kukata  simu,  niliendelea  kulala, ilipofika saa 10 usiku, simu  yangu iliita nilipoitazama nikaona ni namba ya   Nondo, safari  hii  akiomba  nimpe namba ya  rafiki yake  Masumbuko,  nikamwambia sina…baada ya hapo alikata simu,”alisema .

Akijibu  swali  la wakili  upande wa utetezi, shahidi  huyo  alisema  anatambua wapo  watu wanaoigiza sauti mbalimbali, lakini alimtambua Nondo kupitia  sauti yake namba  yake.

Alisema wakati wakizungumza, Nondo alikuwa ni mtu anayeongea  haraka haraka, huku akitumia  namba  ya mtandao wa Tigo inayoishia 25.

Alisema  alitumia  muda wa dakika  tatu mara ya kwanza  kuongea na Nondo  usiku huo na mara ya pili,  alitumia dakika kama nne hivi .

Hata   hivyo,wakili wa upande  wa  utetezi, Kambone Jebra  alihoji mtu anayesafiri  kutoka Dar es salaam  kwenda Igunga mkoani Tabora,lazima  afike mkoani Iringa, kama ni hivyo aliwezaje  kuitambua  sauti ya Nondo kwa njia ya  simu  wakati  inaweza kuigizwa   kwa mfano, msanii  Steve Nyerere  amekuwa akiingiza sauti nyingi analitambua  hilo.

Alisema naalitambua, lakini alipohojiwa kuwa hakuumia alipoachana na Nondo kama mpenzi wake, alisema hakuumia.

Akijibu  maswali ya  wakili  huyo, shahidi huyo  alikiri mtu  anayekwenda  Tabora,  si  lazima  apite Iringa  na  kuwa anakubaliana kuwa  wapo  wanaoweza  kuigiza  sauti  za watu kama  anavyofanya msanii Nyerere.

Alipoulizwa kama bado anampenda Nondo, alikataa kuendelea  kumpenda, lakini alibanwa zaidi kuwa imekuwaje  kama hampendi amekwenda mahakamani kumtolea ushahidi.

Shahidi huyo alijibu kuwa  anampenda kama binadamu mwingine na si mpenzi.

Veronica ambaye ni shahidi wa tatu  katika kesi hiyo,  alisema  amepata  kuishi Mtaa wa Semtema eneo la Kihesa katika nyumba ya mzee Chusi  na wakati  huo  alikuwa  akisoma  chuo  cha  Kikuu cha Tumaini, japo  alisema katika kuishi kwake Iringa hafahamu hata uwanja wa Somora.

Naye shahidi wa nne,PC  Abdul  karim kutoka Kitengo cha  Makosa ya Mtandao  makao makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam,  alieleza mahakama kuwa alipokea vielelezo kutoka kwa Koplo John, vikiwamo kompyuta mpakato na simu ya mkononi.

Alisema  baada ya kupokea vifaa hivyo, alivihifadhi ndani ya kabati lake,baadae alifanyia uchunguzi na kubaini vitu kadhaa ndiyo amevikisha  mbele ya mahakama ili vitumike kama vielelezo vya ushahidi .

Hata hivyo, upande wa utetezi kupitia wakili Kambone aliomba mahakama kutokupokea kilelezo hicho kwa kuwa kina upungufu  mwingi.

Hakimu Mpitanjia, aliitaka Jamuhuri iwe na muda mzuri wa kupitia  vielelezo ili kujiridhisha na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles