23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

UGONJWA WA MNYAUKO WAHAMIA KWENYE KOROSHO

NA FLORENCE SANAWA-LIWALE


UGONJWA wa mnyauko fusari umekausha zaidi ya mikorosho 136 wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi na kuzua taharuki kwa wakulima wa zao hilo.

Ugonjwa huo ulianza kujitokeza mwishoni wa mwaka 2016 wilayani humo. Hivi sasa Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Mary Mwanjelwa, ametembelea eneo hilo kuona athari zilizojitokeza.

Akizungumza baada ya kutembelea Kijiji cha Legezamwendo wilayani humo, Dk. Mwanjelwa, alisema ugonjwa huo lazima upatiwe ufumbuzi wa haraka ili usienee kwa kasi.

“Nimekuja hapa Legezamwendo, nimekagua mashamba, kwa kweli nimejionea kwa macho athari kubwa zilizojitokeza kwenye korosho ambalo ni zao la mkakati miongoni mwa mazao matano ambayo yanafanya vizuri sokoni.

“Tunapopata taarifa hii lazima tushtuke na lazima tutambue kuwa kinga ni bora kuliko tiba, unashangaa kuona mti mzima wa korosho unageuka kuwa kuni, hii ni hatari zaidi, lazima ufumbuzi utafutwe.

“Tunawaambia wakulima wakiona majani yamebadilika rangi na kuwa kahawia waukate na kuuchoma pamoja na vitendea kazi ikiwa ni sehemu ya kuua vijidudu vilivyopo kwenye ugonjwa huo,” alisema Dk. Mwanjelwa na kuongeza:

“Taasisi yetu ya Naliendele inapaswa kufanya kazi usiku na mchana  kupata ufumbuzi wa ugonjwa huo na kuhakikisha hauenei.”

Zainabu Nyanga mkazi wa kijiji hicho, alisema ugonjwa huo ulianzia shambani kwake.

Alisema alikuwa akipata magunia 28 hadi 30, lakini baada ya kuingia ugonjwa huo msimu uliopita aliambulia magunia 10 pekee hali ambayo imemsababishia kuyumba kiuchumi.

Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Joseph Mhagama, Ofisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri hiyo, Mustapha Maghembe, alisema ugonjwa huo ulianza wilayani humo mwaka 2016 na dalili za mwanzo ilikuwa ni kukauka   mikorosho mitatu katika shamba la Abdallah Njawike.

“Baada ya hali hiyo tulimshauri mkulima huyo kutumia viuatilifu  kudhibiti mbu wa mikorosho baada ya kudhani kuwa ndiyo chanzo cha ugonjwa huo.

“Kuenea kwa ugonjwa huo kuliwaibua wataalamu wa Naliendele kufika na kuchukuwa sampuli mbalimbali kupata ufumbuzi wa ugonjwa huo ambao unaelekea kuwa wa kudumu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles