31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wateketeza hosteli UDSM

NA MICHAEL SARUNGI, Dar es Salaam
WANAFUNZI wawili wanaosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wameumia baada ya moto kuteketeza hosteli za Mabibo Dar es Salaam, walikokuwa wakiishi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema moto huo uliteketeza ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa na wanafunzi wa kike.
“Tunamshukuru Mungu hakuna maafa yaliyotokea ingawa kuna wanafunzi wawili wamepata matatizo na tayari tumeshawakimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
“Mmoja alijirusha kutoka ghorofa ya tatu kuokoa maisha yake baada ya kuona hakuwa na njia mbadala na mwingine alipoteza fahamu ghafla baada ya moto kuanza kuwaka katika jengo alimokuwa akiishi.
“Kwa hiyo kwa sasa tunafanya utaratibu wa kuangalia jinsi tutakavyowasaidia wanafunzi waliopatwa na matatizo ya kupotelewa na vifaa na nasema chuo kitahakikisha wanapatiwa huduma zote muhimu,” alisema Profesa Mukandala.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi wa Kinondoni, Camillus Wambura, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, ulinzi uliimarishwa kudhibiti wizi na uharibifu mwingine ambao ungefanywa na watu wasiokuwa waaminifu.
“Taarifa ninazo na tayari ulinzi tumeshauweka kwa kushirikiana na polisi jamii.
“Pamoja na hayo, nawashauri wanafunzi wote waliopoteza mali zao waende kituo cha polisi kutoa taarifa na ikiwezekana wapatiwe msaada wowote watakaouhitaji.
“Nasema hivyo kwa sababu wakati wa uokoaji, baadhi ya mali zilikuwa zinatupwa nje kupitia madirishani na hali hiyo ilisababisha baadhi yake kupotea ila vinaweza kupatikana kwa msaada wa polisi,” alisema Kamanda Wambura.
Kutokana na hali hiyo, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuweka ulinzi eneo la tukio hadi uongozi wa chuo utakapowapatia wanafunzi wote maeneo mengine salama ya kuishi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo Kibangu zilipo hosteli hizo, Deusderi Ishengoma, alisema madhara yaliyotokea yangekuwa makubwa kama moto huo ungewaka usiku.
“Kama unakumbuka siku za nyuma wanafunzi hawa walishaandamana kuilalamikia TANESCO kwamba inashindwa kuimarisha mfumo wa umeme katika hosteli hizo na kusababisha ukatikekatike mara kwa mara.
“Kwa hiyo inawezekana yale malalamiko ndiyo yamesababisha madhara kwa sababu inaonekana tatizo halijatatuliwa,” alisema Ishengoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles