27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wavuta pumzi tuhuma za mauaji ya Dk. Slaa

kovaJonas Mushi na Asifiwe George, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limesema linaendelea na uchunguzi wa tuhuma za mauaji dhidi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilibrod Slaa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na utakapokamilika taarifa kamili itatolewa kwa umma.
Kova ametoa kauli hiyo huku Watanzania wakiwa bado na shauku ya kujua hatima ya tuhuma hizo ambazo hadi sasa giza limetanda baada ya polisi kumuachia kwa dhamana mlinzi wa Dk. Slaa, Khalidi Kangezi wakati walinzi wa Chadema wakisota rumande.
“Tunaendelea na uchunguzi na kwa sasa hatuwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu tunaweza kuharibu sehemu ya upelelezi wetu, lakini utakapokamilika tutaita vyombo vya habari na kutoa taarifa,” alisema Kova.
Jeshi la Polisi kimekwisha kutoa taarifa ya kufunguliwa mashtaka mawili kuhusiana na suala hilo.
Shitaka la kwanza ni lile la kutekwa na kuteswa kwa aliyekuwa mlinzi binafsi wa Dk. Slaa, Kangezi, ambako watuhumiwa watatu wa kesi hiyo tayari wamekwisha kufikishwa mahakamani.
Shitaka la pili ni lile alilofunguliwa Kangezi kuhusiana na tuhuma za kufanya njama za kutaka kumuua Dk. Slaa kwa kumwekea sumu katika chakula au kinywaji.
Hadi sasa watuhumiwa wa kumteka na kumtesa Kangezi wako mahabusu katika gereza la Keko kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana huku Kangezi akiwa hajafikishwa mahakamani.
Aliachiwa na polisi kwa dhamana katika Kituo cha Polisi Oysterbay wakisema upelelezi unaendelea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilitangaza kuanza kumchunguza Josephine Mushumbusi, mke wa Dk. Slaa, anayetuhumiwa kula njama za kumuangamiza.
Uchunguzi dhidi ya Mushumbusi ulitangazwa na Kova alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Kova alisema kuanzishwa kwa uchunguzi huo ni matokeo ya maelezo ya Kangezi ambaye alifikishwa polisi baada ya kutekwa na kuteswa kwa tuhuma za kushiriki mipango ya kumuua Dk. Slaa.
Alisema Kangezi baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, katika maelezo yake, aliwataja Mushumbusi na mchungaji mmoja ambaye jina lake halijawekwa hadharani, kuwa ndiyo waliokuwa na mpango huo lakini yeye aliuzuia.
Mbali na wawili hao, Kamanda Kova alisema uchunguzi huo pia utawagusa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, ambaye ametajwa na baadhi ya makada wa Chadema kuwa mmoja wa wahusika wa mpango wa mauaji ya Dk. Slaa.
Dk. Slaa alifunguka kwa mara ya kwanza kuhusu suala hilo la kutaka kuuawa akisema ilikuwa awekewe sumu katika maji au chakula.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Posta Isaka, wilayani Kahama Jumamosi iliyopita, Dk. Slaa alimtuhumu moja kwa moja kiongozi wa juu wa CCM kuwa ni miongoni mwa watu waliofanya jaribio la kutaka kumuua kupitia kwa mlinzi wake binafsi, Kangezi.
Dk. Slaa alisema jaribio la kutaka kuuawa kwa sumu lilipangwa kutekelezwa nyumbani kwake Februari 28 mwaka huu.
Alidai kiongozi huyo kwa kushirikiana na viongozi wengine wa juu ndani ya CCM walimtumia Kangezi kutimiza azma yao ya kuhakikisha wanakatisha uhai wake.
Mbali na kumshutumu kiongozi huyo, pia alimtuhumu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na mtu mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ngowi, kuwa ni wahusika wakuu wa njama hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles