Na Safina Sarwatt
-Moshi
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imepokea tuzo mbili kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kutokana na kufanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2018, ikishika nafasi ya pili kitaifa na ya kwanza kimkoa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, Ofisa Elimu Msingi wa manispaa hiyo, Patrick Leana, alisema nafasi ya kwanza kitaifa ilishikwa na Jiji la Arusha.
“Manispaa ya Moshi ilifaulisha kwa asilimia 96.21 na kushika nafasi ya pili kitaifa na ya kwanza kimkoa, Jiji la Arusha ambao walifaulisha kwa asilimia 97.4, walikuwa wa kwanza,” alisema Leana.
Alisema tuzo ya pili ilitolewa kwa manispaa hiyo kwa ajili ya pongezi ya kufaulisha watahiniwa kwa asilimia 99.6 katika upimaji wa kitaifa kwa darasa la nne mwaka 2018 ambapo ilishika nafasi ya tatu kitaifa na nafasi ya kwanza kimkoa.
Leana alisema Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kwa kutambua juhudi zinazofanywa na walimu, ilitunuku vyeti vya pongezi shule zilizofaulisha watahiniwa wote kwa asilimia 100.
Alisema Idara ya Elimu Msingi katika halmashauri hiyo, imekuwa ikifanya vizuri katika utoaji wa taaluma kwa wanafunzi wake kwa muda mrefu.
“Manispaa ya Moshi imekuwa katika nafasi 10 bora kitaifa ambapo kwa miaka miwili mfululizo imeshika nafasi ya pili kitaifa na nafasi ya kwanza kimkoa, na mafanikio hayo yanatokana na juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali pamoja na Serikali.
“Lengo tulilonalo kwa sasa ni kuhakikisha tunafaulisha watahiniwa wetu wote ili turudishe heshima yetu tuliyokuwa nayo mwaka 2013 ya kuwa nafasi ya kwanza kitaifa,” alisema Leana.