24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Moshi wapata tuzo kwa kufanya vizuri elimu

Na Safina Sarwatt

-Moshi

HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imepokea tuzo mbili kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kutokana na kufanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2018, ikishika nafasi ya pili kitaifa na ya kwanza kimkoa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, Ofisa Elimu Msingi wa manispaa hiyo, Patrick Leana, alisema nafasi ya kwanza kitaifa ilishikwa na Jiji la Arusha.

“Manispaa ya  Moshi ilifaulisha kwa asilimia 96.21 na kushika nafasi ya pili kitaifa na ya  kwanza kimkoa, Jiji  la Arusha ambao walifaulisha kwa asilimia 97.4, walikuwa wa kwanza,” alisema Leana.

Alisema tuzo ya pili ilitolewa kwa manispaa hiyo kwa ajili ya pongezi ya  kufaulisha watahiniwa kwa asilimia 99.6 katika upimaji wa kitaifa kwa darasa la nne mwaka 2018 ambapo ilishika nafasi ya tatu kitaifa na nafasi ya kwanza kimkoa.

Leana alisema Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kwa kutambua juhudi zinazofanywa na walimu, ilitunuku vyeti vya pongezi shule zilizofaulisha  watahiniwa wote kwa asilimia 100.

Alisema Idara ya Elimu Msingi katika halmashauri hiyo, imekuwa ikifanya vizuri katika utoaji wa taaluma kwa wanafunzi wake kwa muda mrefu.

“Manispaa ya Moshi imekuwa katika nafasi 10 bora kitaifa ambapo kwa miaka miwili mfululizo imeshika nafasi ya pili kitaifa na nafasi ya kwanza kimkoa, na mafanikio hayo yanatokana na juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali pamoja na Serikali.

“Lengo tulilonalo kwa sasa ni kuhakikisha tunafaulisha  watahiniwa wetu wote ili turudishe heshima yetu tuliyokuwa nayo mwaka  2013 ya  kuwa nafasi ya kwanza kitaifa,” alisema Leana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles