30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Morogoro yatakiwa kuandaa maonyesho ya madini

Mwandishi Wetu -Dodoma

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na wizara yake kuandaa maonyesho ya madini yenye lengo la kutoa elimu kwa umma, hasa katika mkoa huo, kuhusu sheria, kanuni na fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Agizo hilo alilitoa jana mjini hapa, katika kikao cha pamoja baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Madini, Mtumba jijini hapa.

“Nichukue fursa hii kuwaelekeza wataalamu wote wa Wizara ya Madini na taasisi zake kuhakikisha wanashirikiana na Mkoa wa Morogoro kuzitangaza fursa zinazopatikana katika sekta ya madini mkoani Morogoro kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kuandaa maonyesho yatakayopelekea kuelimika kwa wananchi wa mkoa huo,” alisema Waziri Biteko. 

Aidha, alisisitiza ushirikiano katika kusimamia sekta ya madini kati ya wizara na Mkoa wa Morogoro na kumpongeza Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Shija kwa kazi nzuri anazozifanya katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Waziri Biteko alisema maendeleo ya sekta ya madini katika Mkoa wa Morogoro yatatokana na wachimbaji wenyewe, hivyo wizara na mkoa wanapaswa kuwalinda na kuwalea wachimbaji na wadau wote wa madini mkoani humo.

Akizungumzia changamoto inayowakabili wananchi wa Morogoro, Biteko alisema ni pamoja na uelewa mdogo walionao juu ya masuala yanayohusiana na sekta ya madini kuwa ni kikwazo katika kupeleka maendeleo mkoani humo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameonyesha kufurahishwa na kitendo cha Mkoa wa Morogoro kuonyesha mafanikio makubwa katika makusanyo ya mapato ya Serikali kutoka Sh 811,714,294.12 kwa mwaka 2017/18 hadi kufikia Sh 1,031,865,068.41 kwa mwaka 2018/19.

“Madini ya ujenzi, vito na dhahabu tukiyasimamia vizuri hakika yatatuingizia fedha nyingi watu wa Morogoro, hivyo nikuombe mkuu wa mkoa ukalifanyie kazi hilo, pia sisi kama Wizara ya Madini tutashirikana na Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wawekezaji wanakuja kuwekeza katika sekta ya madini,” alisema Nyongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles