27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Washauriwa kulima kahawa inayotunzwa na mikojo ya wanyama

Safina Sarwatt -Moshi 

WAKULIMA wa zao la kahawa mkoani Kilimanjaro, wameshauriwa kulima kilimo cha asili ambacho hakitumii madawa ya viwandani na badala yake kinatumia mikojo ya wanyama wanaofugwa.

Imeelezwa kuwa kahawa hiyo inayolimwa kwa njia ya asili ina bei nzuri katika soko la dunia ikilinganishwa na ile inayotumia madawa ya viwandani.

Kauli hiyo imetolewa na mkulima wa kahawa ambaye pia ni Meneja wa Muungano wa vyama 32 vya kahawa mkoani Kilimanjaro – G-32, Gabriel Ulomi, wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake. 

Alisema kahawa ambayo imezalishwa kwa njia ya asili ina soko kubwa na uhitaji wake ni mkubwa katika soko la dunia ambapo kwa sasa bei yake ni Sh 7,1250 kwa kilo ya kahawa ambazo hazijamenywa. 

Ulomi alisema G-32 imeendelea kuwahamasisha wakulima kulima kilimo cha asili kwa kuwa kina faida na hakina gharama tofauti na kahawa zinazolimwa kwa kutumia madawa ya viwandani. 

“Uhitaji wa soko la kahawa kwa sasa ni kahawa iliyozalishwa kwa njia ya asili ambayo haijapigwa madawa,” alisema Ulomi. 

Alisema mwaka 2018/2019 waliingia kwenye kilimo hai ambapo wanatumia alizeti mwitu, mkojo wa ng’ombe, punda na mbuzi kuua wadudu na kutu za majani kwenye kahawa.

“Sasa hivi mkulima hahitaji kutumia dawa na hivyo gharama za uzalishaji ni ndogo na ina bei kubwa ambapo kilo moja ni Sh 7,125 baada ya kuondoa gharama zote za usafirishaji magunia, ukilinganisha na kahawa zilizozalishwa kwa madawa ambazo kilo ni Sh 3,000. 

“Madawa ya viwanda yanaua viumbe hai kama nyuki ambao wana faida kubwa  katika uchafushaji,” alisema Ulomi. 

Hansi Mangowi ambaye ni mkulima kutoka Chama cha Msingi cha Ushirika Mamba Kusini wilayani Moshi, pia alisema kahawa zinazozalishwa kwa njia  ya asili zina faida na bei nzuri sokoni. 

“Kilimo hai kinalipa, tumefaidika. Sisi tangu mwaka 2017/18 hatujawahi kutumia madawa ya viwandani na tunauza kahawa yetu moja kwa moja nje kwa bei nzuri,” alisema Mangowi. 

Alisema kilo ya kahawa ambayo haijalimwa kwa madawa inauzwa kwa Sh 7,250 hadi 8,000, ambapo kahawa zilizozalishwa kwa madawa ni Sh 3,000 hadi 3,500.

Alisema uhitaji wa kahawa inayozalishwa kwa njia ya kilimo hai ni kubwa na soko lake linapanda siku hadi siku. 

“Hata gharama za uzalishaji ni ndogo na ina faida kubwa, unatumia majivu, mkojo wa punda na mg’ombe kuua wadudu kwenye kahawa,” alisema Mangowi,

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles